UNICEF: Mlipuko wa Ebola umewaweka Watoto hatarini
-
Wasiwasi wa Unicef kuhusu hatari ya Ebola kwa watoto
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu mlipuko wa Ebola unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC na Uganda, huku likionya kuwa watoto wako kwenye hatari kubwa zaidi.
Katika taarifa ,UNICEF imesema, “kila mlipuko wa Ebola huwaweka watoto hatarini si tu kutokana na ugonjwa wenyewe, bali pia kuvurugika kwa huduma muhimu kama afya, lishe, elimu na ulinzi.”
Shirika hilo linaeleza kuwa linashirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha juhudi za kudhibiti maambukizi zinafanyika haraka, huku likisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii na uratibu wa mipakani.
UNICEF tayari imechukua hatua kadhaa za haraka kukabiliana na mlipuko huo.
“Hatua za haraka, ushirikiano wa jamii, na kuimarisha nguvu ya wahudumu wa afya ni muhimu ili kulinda watoto na kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huu.”
Kasi ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Bundibugyo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC vinavyosababisha ugonjwa wa Ebola inazidi kuongezeka wakati huu ambapo idadi ya watu wanaoshukiwa kuambukizwa ni zaidi ya 500, wanaoshukiwa kufa ni 130 huku watu waliothibitshwa kufa kwa ugonjwa huo ni 30.
Mwakilishi wa WHO nchini DRC Dkt. Anne Ancia, amesema “tuna hali kubwa ya kutokuwa na uhakika kuhusu idadi ya maambukizi na jinsi virusi vilivyosambaa.”
Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi, kutoka Bunia mji mkuu wa jimbo la Ituri, ambako wagonjwa wamegunduliwa awali, Dkt. Ancia amesema kuwa mlipuko huo umefika pia jimbo la Kivu Kaskazini, huku wagonjwa waliothibitishwa wakirekodiwa Butembo na Goma jimboni humo. Uganda pia imethibitisha wagonjwa wawili waliowasili kutoka nje ya nchi hiyo.
Jumapili asubuhi, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, alitangaza mlipuko huo kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa, akieleza wasiwasi kuhusu “ukubwa na kasi ya janga hilo”.