Oct 29, 2021 23:13 UTC
  • Jumamosi, 30 Oktoba, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 23 Mfungo Sita Rabiu-Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe 30 Oktoba 2021.

Siku kama ya leo miaka 1242 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Bibi Fatma Maasuma dada wa Imam Ali bin Mussa al-Ridha (AS) aliwasili katika mji wa Qum, Iran. Mwaka mmoja baada ya safari ya kubaidishiwa kaka yake huko katika mji wa Marv, Bibi Maasuma alifunga safari kwa ajili ya kwenda kuonana na kaka yake. Baada ya kuwasili Qum, aliishi katika mji huo kwa siku 17 na katika wakati huo alijishughulisha na ibada, dua na kujikurubisha kwa Mola Muumba. Eneo alilokuwa akifanyia ibada bibi huyo mtukufu hadi leo linajulikana kama 'Baitul Nur, na hadi leo linatembelewa na wapenzi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (SAW). Mwishowe tarehe 10 Rabiul Thani mwaka 201 Hijiria, ikiwa ni kabla hajakutana na kaka yake  Imam Ridha AS, Bibi Fatima Maasuma alifariki dunia huku akiwa katika upweke na majonzi makubwa. Hii leo haram ya BibI  Fatma Maasuma AS mjini Qum ni moja ya maeneo matakatifu ambapo watu kutoka katika maeneo mbalimbali ya ulimwengu wa Kiislamu huenda kufanya ziara katika eneo hilo.***

Haram ya Bibi Fatima Maasuma (a.s) mjinii Qum

 

Miaka 111 iliyopita katika siku kkama ya leo ya tarehe 30 Oktoba 1910 alifariki dunia Henri Dunant, mwasisi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Dunant alizaliwa Geneva, Uswisi na mwaka 1828, aliamua kuanzisha Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kwa shabaha ya kuokoa maisha ya majeruhi wa vita. Kutokana na hatua yake hiyo ya kibinadamu, Henri Dunant alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1901, na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Aban 1359 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Muhammad Hussein Fahmideh, kijana shujaa wa Kiirani kwenye vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Shahidi Fahmideh alielekea kwenye medani ya vita akiwa na umri wa miaka 13 tu, ikiwa imepita miezi michache tu baada ya kuanza kwa vita hivyo. Shahidi Fahmideh alijitolea mhanga kwa kujifunga kiunoni maguruneti na kujilaza mahala kilipokuwa kikipita kifaru cha adui na kuwatia kiwewe na hatimaye kuwalazimisha wavamizi kukimbia. Hatua hiyo ilipongezwa na Imam Khomeini ambaye alimtaja kijana huyo kuwa ni kiongozi na kigezo cha kuigwa. ***

Shahidi Muhammad Hussein Fahmideh,

 

Na siku kama ya leo miaka 33 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani alimu na mwanazuoni mchaji-Mungu. Alizaliwa mjini Tehran katika familia iliyokuwa imeshikamana kikamilifu na dini. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali alielekea katika mji wa Qum Iran na baadaye Najaf Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Akiwa katika huko Ayatullah Tehrani alihudhuria darsa na masomo ya walimu mahiri wa zama hizo. Miongoni mwa sifa alizopambika nazo Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani ni uchaji Mungu, kuipa kwake mgongo dunia na mapenzi yake makubwa kwa Ahlul-Beit AS. Msomi huyo wa Kiislamu hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu. ***

Ayatullah Mirza Javad Agha Tehrani