Oct 30, 2021 06:25 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (31)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa uwezo na tawfiki ya Allah tumekutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na kazi na athari zao. Tulisema katika kipindi kilichopita kuwa, Qadhi Nurullah Shushtari alizaliwa mwaka 956 Hijria katika mji wa Shushtar nchini Iran. Baada ya kukamilisha masomo ya msingi katika mji wa Shushtar alielekea mjini Mash’had na mwaka 993 Hijria Qadhi Shushtari alihajiri na kuelekea India na kuuchagua mji wa Agra kuwa makazi yake. Tulieleza pia kuwa, umahiri wa Kadhi Nurullah kuhusu masuala ya kifikihi ya madhehebu mengine ya Kiislamu. Sehemu ya 31 ya kipindi chetu juma hili  itamzungumzia alimu na msomi mwingine mashuhuri wa Kishia wa karne ya 11 Hijria ambaye ni Sheikh Bahai. Jiungeni nami hadi tamati ya kipindi hiki.

Muhammad bin Hussein bin Abdul Swamad Harithi, mashuhuri zaidi kwa majina ya Bahau Din au Sheikh Bahai ni mmoja wa Maulamaa wakubwa na watajika katika ulimwengu wa Kishia na Kiislamu. Sheikh Bahai alizaliwa mwaka 953 Hijria na inasemekana kuwa ilikuwa ni tarehe 17 Mfunguo Tatu Dhul-Hija, huko katika mji wa Baalbek nchini Lebanon. Baba yake ni Izzuddin Hussein Amili ambaye alitambulika nchini Lebanon kama msomi na mwanazuoni mahiri na mtajika na mwanafunzi wa Shahidi Thani. Nasaba yake inaishia kwa Harith Hamedani, sahaba mtukufu wa Amirul-Muuminina Ali bin Abi Twalib (a.s).

Sheikh Bahai alikipitisha kipindi chake cha utoto katika kitongoji cha Mashia cha Jabal Amil nchini Lebanon. Akiwa na umri wa miaka 13 Bahau Ddin alihajiri pamoja na familia yake na kuja Iran. Katika zama hizo Waturuki wa Kiseljuki walikuwa wakiidhibiti Lebanon na walikuwa wakiwabana na kuwawekea mazingira magumu sana wafuasi na wapenzi wa Ahlul-Baiti (a.s). Badala yake, hali ya mambo nchini Iran ilikuwa kinyume kabisa, kwani baada ya kuingia madarakani utawala wa Kisafavi uliokuwa ukidai kuwa mfuasi wa Ushia na kuwapenda wasomi na wanazuoni wake, palikuwa mahala mwafaka kabisa kwa ajili ya kueneza madhehebu ya Ahllul-Baiti (a.s). Katika zama hizo Iran palikuwa mahala na kituo cha kukusanyika wasomi na wanazuoni wa Kishia. Baba yake Sheikh Bahai kutokana na kuwa na elimu, maarifa na fadhila aliteuliwa na Sultan Muhammad Khodabandeh kuwa Sheikhul Islami wa Harat. Baadaye cheo hicho alikuja kupatiwa Sheikh Bahai.

Sheikh Bahai

 

Sheikh Bahai mbali na kubobea na kutabahari katika elimu na maarifa ya Kiislamu alikuwa hodari pia na mwalimu katika taaluma rasmi na elimu mashuhuri katika zake kama vile hisabati, usanifu majengo, uhandisi, jiografia na nujumu. Athari zake za usanifu majengo licha ya kupita karne nyingi, hadi leo zingali zinasifiwa na wasomi na waalimu na wabobezi wa taaluma hii.

Baadhi ya athari za Sheikh Bahai za usanifu majengo zina umashuhuri kimataifa kama vile minara ya Isafahan ambapo ukiutikisa mnara mmoja na ule wa pili unatikisika,  mnara wa Msikiti wa Imam Khomeini huko Isafahan ambao unaakisi sauti mara saba, ubunifu wa eneo la ndani la Imam Ali bin Mussa al-Ridha (a.s) mjini Mash’had na kusanifu kuta za Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) huko Najaf kiasi kwamba, zinaainisha wakati wa Swala ya Adhuhuri katika kipindi chote cha mwaka.

Kupitia kipaji cha Sheikh Bahai katika mji wa Isfahan ambao ulikuwa mji mkuu wa Shah Abbas  aliyekuwa mtawala wa 5 wa ukoo wa Safavi nchini Iran, kulijengwa misikiti, majengo, madaraja, barabara na mabustani mengi na ni wakati huo ndipo kilipoanza kipindi cha dhahabu cha usanifu majengo cha Safavi na kwa utaratibu huo, sanaa hii ikawa moja ya sanaa na ubunifu muhimu unaotambulisha sanaa na usanifu majengo wa Iran.
 

 

Usanifu majengo wa Safavi ulikuwa na taathira kubwa pia katika duru zilizofuata  kama ambavyo uliathiri sanaa ya usanifu majengo ya mataifa kama India, Iraq, Caucasia, Uzibekistan, utawala wa Othmania (Ottoman Empire), Lahore na Florence italia. Ni kwa kuzingatia mchango na nafasi hiyo, ndio maana kumbukumbu ya kuzaliwa Sheikh Bahai imepewa jina nchini Iran la Siku ya Usanifu Majengo.

Licha ya kuwa Sheikh Bahai alikuwa amebobea na kutabahari katika elimu mashuhuri katika zama zake, lakini umuhimu wa mwanazuoni huyu mkubwa katika Ulimwengu wa Kishia ni zaidi ya kutabahari katika usanifu majengo, nujumu na hisabati.

Sheikh Bahai ni mwanazuoni mahiri na mkubwa pia katika maarifa ya Kiislamu kama Fikihi, maarifa ya Qur’ani, Tafsiri, misingi ya itikadi, dua na minong’ono (munajaat) na falsafa. Sheikh Bahai anahesabiwa kuwa mmoja wa Maulamaa waliokuwa na hima kubwa katika kualifu na kuandika vitabu.  Sheikh Bahai ana athari na kumbukumbu zipatazo 123 ambazo ni majimui ya vitabu, makala na kadhalika. Kitabu cha Jamiu Abbasi, ndicho kitabu mashuhuri zaidi cha fikihi ambacho hakina mithili.

Sheikh Bahau au Bahauddin kama anavyojulikana pia akiwa fakihi mahiri wa Kishia alikuwa akizingatia mno vyanzo viwili vya asili katika fikihi yaani Qur’ani na Sunna za Bwana Mtume (s.a.w.w).

 

Sanamu la Sheikh Bahai mjini Isafahan

Mtindo wa Sheikh Bahai katika kubainisha nadharia na mtazamo wa Kifikihi na kunyambua sheria za dini kutoka katika vyanzo ulikuwa kwamba, awali  alikuwa akizirejea Aya za Qur'ani kuhusiana na maudhui aliyokuwa akiihitaji na kusoma tafsiri yake kwa umakini, kisha hatua ya pili huzirejea riwaya na hadithi na kuchunguza pande zake zote. Hatua ya tatu ilikuwa ni kusoma kwa umakini na kuchambua mitazamo na nadhari za Mafakihi wengine kuhusiana na jambo hilo na kisha kutoa mtazamo wake kuhusiana na kadhia hiyo. Kitabu cha Mashraq al-Shamsin kimeandikwa kwa mtindo huu.

Sheikh Bahai alikuwa pia na mapenzi makubwa na elimu ya Irifan kuliko wasomi na wanazuoni wengine wa zama zake. Upande mwingine muhimu wa maisha ya Sheikh Bahai pamoja na shakhsia yake ni nafasi na mchango wake wa kisiasa na kijamii nchini Iran katika zama hizo. Kawaida Maulama wa Kishia hawakuwa na uhusiano wa karibu na utawala wa wafalme, kwani walikuwa wakiamini kuwa, kumtegemea dhalimu na kuwasaidia madhalimu na madikteta ni dhambi. Hata hivyo katika baadhi ya zama, kama katika kipindi cha utawala wa Safavi nchini Iran, baadhi ya Maulamaa wakubwa wa Kishia walikuwa na uhusiano wa karibu na utawala.

Hata hivyo uhusiano huo haukuwa na maana ya kutaka madaraka na jaha au kupenda dunia, bali wanazuoni hao kwa kudiriki na kusoma vizuri alama za nyakati pamoja na mazingira ya zama, waliamua kuanzisha uhusiano huo kwa ajili ya kuboresha hali ya jamii ya Waislamu.

Kaburi la Sheikh Bahai mjini Mash'had, Iran

 

Sheikh Bahai Amili aliaga dunia mwaka 1031 Hijria baada ya miaka 78 ya umri wake uliojaa hima, jihadi na idili katika njia ya kueneza mafundisho ya Ahlul-Baiti (a.s) na kuzikwa katika mji wa Mash'had nchini Iran.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nakomea hapa, kutokana na kumalizika muda wa kipindi chetu,, hivyo msikose kuwa nami tena juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo wa vipindi hivi vya Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

Tags