Jumatatu tarehe Mosi Novemba 2021
Leo ni Jumatatu tarehe 25 Rabiul Awwal 1443 Hijria sawa na tarehe Mosi Novemba 2021.
Katika siku kama ya leo miaka 1007 iliyopia sawa na tarehe 25 Rabiul Awwal mwaka 436 Hijiria alifariki dunia Sayyid Murtadha Alamul Huda mwanafunzi mashuhuri wa Sheikh Mufid. Alizaliwa mwaka 355 Hijiria huko Baghdad na alijifunza elimu za zama zake. Baadaye alianzisha kituo cha elimu ambacho kilikuwa kikihudhuriwa na watu wenye itikadi na mielekeo tofauti. Sayyid Murtadha ameacha vitabu vingi na miongoni mwa vitabu hivyo ni Tanzihil Anbiyah, Taqribul Usul pamoja na kitabu cha maashairi chenya beti elfu 20.
Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, serikali ya wakati huo ya Iran ilitangaza kutofungamana na upande wowote katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Hata hivyo udhaifu wa kisiasa wa watawala wa wakati huo, matatizo ya ndani, matatizo ya kivita na kupenda kujitanua kwa nchi zilizokuwa zikipigana katika vita hivyo ni mambo yaliyopelekea nchi hii kwenda kinyume na ahadi yake ya kutofungamana na upande wowote katika vita hivyo. Ni kutokana na hali hiyo ndipo Iran ikajikuta katika hujuma na mashambulizi ya majeshi ya Uingereza, Urusi ya zamani na jeshi la Othmania na kuisababishia hasara kubwa.

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita utawala wa kifalme nchini Uturuki ulihitimishwa rasmi na Kemal Ataturk. Baada ya kumalizika kwa Vita vya Kwanza vya Dunia sanjari na kudhoofika na kupoteza ushawishi wa utawala wa Othmania, Atatürk aliamua kuvunja utawala huo wa kifalme na kutwa uongozi. Hata hivyo haikuwa rahisi kwa Mustafa Kemal Atatürk kumaliza utawala wa kifalme wa Othmania ambao ulikuwa na misingi ya kidini. Hivyo mwanzoni alitenganisha baina ya utawala wa kisultani na cheo cha ukhalifa wa Waislamu na tarehe Mosi mwaka 1922 akavunja rasmi utawala wa kifalme huku cheo cha ukhalifa kikibakia kama cheo cha heshima tu. Suala hilo liliharakisha kuporomoka kwa utawala wa kifalme wa Othmania uliodumu kwa kipindi cha miaka 600. Baada ya kuporomoka utawala huo, uliundwa utawala wa Jamhuri na wa kisekulari hapo tarehe 29 Oktoba mwaka 1923.
Katika siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, vilianza vita vya ukombozi wa Algeria baada ya kuundwa Harakati ya Ukombozi wa Algeria chini ya uongozi wa Ahmed ben Bella. Baada ya kupita miaka 132 ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria, hatimaye mwaka 1962 mapambano ya ukombozi ya wananchi Waislamu wa Algeria yalizaa matunda na nchi hiyo kujipatia uhuru wake. Baada ya kutangazwa uhuru wa Algeria, Ahmed ben Bella alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo. Utawala wa Ahmed ben Bella ulidumu kwa miaka mitatu tu, kwani ulipofika 1965 alipinduliwa na Kanali Houari Boumediene aliyekuwa waziri wake wa ulinzi.