Nov 20, 2021 04:46 UTC
  • Jumamosi, 20 Novemba 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1443 Hijria sawa na tarehe 20 Novemba 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita Mukhtar bin Abi Ubaida al-Thaqafi alianza mapambano ya kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein bin Ali (a.s), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Mwaka 61 Hijria Imam Hussein AS akiwa pamoja na wafuasi na watu wa familia yake, aliuawa shahidi na jeshi la Yazid akiwa katika harakati za kuilinda dini tukufu ya Uislamu. Mukhtar alianzisha harakati zake za mapambano katika mji wa Kufa. Kabla yake, kulijitokeza kundi la 'Tawwabiin' ambalo lilipigana na utawala wa Bani Umayyah, kwa lengo la kulipiza kisasi cha damu ya Imam Hussein AS. Mukhtar Thaqafi alitawala Kufa kwa kipindi cha karibu mwaka mmoja na mwishowe alishindwa na jeshi la Mus'ab bin Zubair na kuuawa shahidi. ***

Kaburi la Mukhtar bin Abi Ubaida al-Thaqafi

 

Katika siku kama ya leo miaka 111 iliyopita alifariki dunia mwandishi mashuhuri wa Kirusi, Leo Tolstoy. Mwandishi huyo alizaliwa mwaka 1828 na aliondokewa na baba na mama yake akiwa bado mdogo. Alifanya safari za kitalii na uchunguzi katika jamii nyingi za Ulaya na mambo aliyoyashuhudia katika safari hizo yalimfanya achukie ustaarabu wa kimaada wa nchi za Magharibi. Tolstoy alilipa umuhimu mkubwa suala la kuwapa elimu na malezi watoto wadogo na alikuwa akijitahidi mno kusaidia matabaka ya watu maskini na wasiojiweza. Leo Tolstoy ameandika vitabu vingi kikiwemo kile cha "Kiyama", "Kipindi cha Utotoni" na riwaya ya "Vita na Amani". ***

Leo Tolstoy

 

Tarehe 20 Novemba miaka 101 iliyopita mapambano makubwa ya wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni wa Kiingereza yalishindwa. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na kusambaratika utawala wa Kiothmania, serikali za Ufaransa na Uingereza ziligawana ardhi za utawala huo katika Mashariki ya Kati. Kwa msingi huo Uingereza ilichukua Iraq na kukabiliwa na mapambano makali ya wananchi tangu hapo mwanzoni. Mapambano hayo yaliongozwa na wanazuoni wa Kiislamu waliotoa wito wa kufukuzwa wakoloni wa Kiingereza na kuundwa serikali huru itakayozingatia sheria za Kiislamu. ***

 Kuingia wanajeshi wa Uingereza katika mji wa Baghdad 1917

 

Siku kama ya leo miaka 86 iliyopita, aliuawa shahidi Sheikh Izzuddin Qassam ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati ya mapambano ya ukombozi wa wananchi wa Palestina dhidi ya uvamizi wa Wazayuni maghasibu na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali huko Syria, Sheikh Qassam aliendeleza masomo yake katika Chuo Kikuu cha al Azhar huko Misri. Wananchi wa Palestina walianza mapambana dhidi ya mkoloni Mwingereza mwaka 1930 chini ya uongozi wa Sheikh Izzuddin Qassam. Hata hivyo baada ya kupita miaka kadhaa Wazayuni maghasibu walishirikiana na wakoloni Waingereza na kumuua kigaidi kiongozi huyo wa harakati ya mapambano ya Palestina. ***

Sheikh Izzuddin Qassam

 

Na katika siku kama ya leo miaka 71 iliyopita majeshi ya Marekani na China yalipambana uso kwa uso kwa mara ya kwanza kabisa katika vita vya Korea. Mapigano hayo yalitokana na himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa Korea Kusini na uungaji mkono wa China na Urusi kwa Korea Kaskazini. Vita vya Korea vilisababisha hasara kubwa mno kwa pande zote mbili. Vita hivyo vilisimama kutokana na upatanishaji wa Umoja wa Mataifa na hadi sasa Korea Kaskazini na Kusini zimebakia nchi mbili zilizojitenga. ***

Bendera za Korea Kaskazini na Korea Kusini

 

Tags