Jumapili tarehe 28 Novemba 2021
Leo ni Jumapili tarehe 22 Rabiuthani 1443 Hijria sawa na tarehe 28 Novemba mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 264 iliyopita, alizaliwa William Blake mshairi na mchoraji wa Kiingereza. Blake alikuwa na mapenzi na sanaa tangu akiwa mdogo na alipofikisha rika la ubarobaro alijihusisha na kusoma vitabu vya falsafa na mashairi. Athari za mshairi huyo zilikuwa zikipingana wazi na kanisa, hali ambayo iliwakasirisha mno viongozi wa dini ya Kikristo na watawala wa Uingereza. Hadi anaaga dunia mwaka 1827, msomi huyo wa Uingereza alikuwa ameandika vitabu 13. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni The Marriage of Heaven and Hell, The Tiger, The Chimney Sweeper na The Lamb.
Tarehe 28 Novemba mwaka 1820 alizaliwa mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani Friedrich Engels. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani kwa jina la Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomunisti iliyotangazwa na vyama vya kikomunisti katika mkutano wao wa kwanza hapo mwaka 1848. Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kubuni nadharia za kikomunisti ambazo ziliugawa ulimwengu katika kambi mbili za kisoshalisti na kibepari.
Katika siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, nchi ya Albania ilipata uhuru. Nchi hiyo ilikuwa huru miaka mingi kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih AS, lakini baada ya kuasisiwa ufalme wa Roma ilikaliwa kwa mabavu na utawala huo. Mwaka 1501 Albania ilidhibitiwa na utawala wa Othmaniya. Mwanzoni mwa karne ya 19 utawala huo ulidhoofika na kupoteza nchi za Balkan ilizokuwa ikizitawala na kwa juhudi za wapigania uhuru, hatimaye mwaka 1912 Albania ikajipatia uhuru.

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita Mauritania ilitangaza rasmi uhuru wa nchi hiyo. Mauritania ilikuwa ikikoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 Miladia. Baadaye Uholanzi na Uingereza ziliivamia nchi hiyo na mwaka 1903 Mauritania ikawa koloni la Ufaransa. Katika nusu ya pili ya karne ya ishirini wananchi wa Mauritania walipiga kura ya maoni wakitaka kuasisiwa utawala wa jamhuri ya mamlaka ya ndani. Na hatimaye mwaka 1960 Mauritania ilipata uhuru kamili baada ya kusainiwa makubaliano kati yake na serikali ya Ufaransa.
Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo Iran ilidhibiti visiwa vitatu vya Tombu Kubwa, Tombu Ndogo na Bu Musa baada ya kuondoka vikosi vamizi vya Uingereza katika maeneo hayo. Uingereza iliondoka katika visiwa hivyo vitatu vya Iran vilivyoko katika Ghuba ya Uajemi katika fremu ya mpango wa nchi hiyo wa kuondoa wanajeshi wake katika eneo la Bahari ya Mediterranean na Ghuba ya Uajemi kutokana na matatizo ya kisiasa na kiuchumi yaliyokuwa yakiisumbua nchi hiyo.

Katika siku kama ya leo 41 iliyopita, vikosi vya majini vya Iran vilifanya ooperesheni katika maji ya Ghuba ya Uajemi na kufanikiwa kuvisambaratisha vikosi vya majini vya Iraq. Tukio hilo lilitokea takribani miezi miwili tu baada ya kuanza vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran. Operesheni hiyo ilipelekea kutokea mapigano makali kati ya meli za kivita za pande mbili na meli nyingi za kivita za Iraq ziliteketezwa. Kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa vikosi vya majini katika operesheni hiyo, siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la “Siku ya Jeshi la Majini”.
Na siku kama ya leo mwaka mmoja uliopita Mohsen Fakhrizadeh Mahabadi aliyekuwa Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran aliuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi. Mohsen Fakhrizadeh alizaliwa mwaka 1336 Hijria Shamsia huko Qum na alikuwa mwanachama wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) tangu lilipoundwa. Alitambulia kuwa msomi wa ngazi za juu wa Wizara ya Ulinzi na Kituo cha Utafiti wa Fizikia hapa nchini (PHRC). Shahidi Fakhrizadeh alikuwa na mchango mkubwa sana katika juhudi za pamoja za Wizara ya Afya na Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuzalisha vifaa vya kupambana na maambukizi ya corona ikiwa ni pamoja na kuzalisha chanjo ya virusi hivyo. Hatimaye Ijumaa ya tarehe 7 Azar 1399 (27 Novemba 2020) aliuawa shahidi katika hujuma iliyotekelezwa eneo la Absard na kupata daraja ya juu ya kuuliwa shahidi. Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Iran alisema kuna ushahidi madhubuti unaothibitisha kuwa Israel ilihusika na mauaji hayo ya kigaidi.