Alkhamisi tarehe 9 Disemba 2021
Leo ni Alkhamisi tarehe 4 Jamadil Awwal 1443 Hijria sawa na Disemba 9 mwaka 2021.
Siku kama ya leo miaka 888 iliyopita yaani tarehe 4 Mfunguo Nane Jamadil Awwal mwaka 555 Hijria, Ibnu Athir Jazari mwanazuoni, alimu, mwanahistoria na mwanafasihi mashuhuri wa Kiislamu alizaliwa huko nchini Iraq. Ibnu Athir alisoma masomo yake huko Mosul na Baghdad nchini Iraq na Sham yaani Syria ya leo. Ibnu Athir alikuwa na mapenzi na shauku kubwa na mutwalaa na kufanya utafiti katika uga wa historia. Miongoni mwa kumbukumbu muhimu na yenye thamani kubwa ya mwanazuoni huyo ni kitabu chake mashuhuri cha al-Kamil Fi al Tarikh.

Siku kama ya leo miaka 279 iliyopita Carl Wilhelm Scheele mwanakemia mashuhuri wa Sweden na mmoja kati ya waasisi wa elimu ya kemia ya leo alizaliwa huko Stockholm mji mkuu wa nchi hiyo. Mwanakemia huyo aliendelea na masomo yake kutokana na jitihada na hamu yake kubwa aliyokuwanayo licha ya familia yake kuwa duni. Carl Wilhelm ambae aliishi katika zama za kuchanua kwa elimu ya kemikali, mwezi Oktoba mwaka 1772 alifanikiwa kugundua gesi ya chlorine baada ya juhudi za miaka mitano. Gesi hiyo ni moja kati ya mada muhimu za kemikali na inatumika sana viwandani. Mbali na hayo mwanakemia huyo aligundua pia manganese na Glicerine.
Miaka 263 iliyopita vilianza vita vya miezi 13 vya Madras. Vita hivyo vinahesabiwa kuwa mojawapo ya vita vikali zaidi vya kikoloni kati ya Uingereza na Ufaransa huko India. Vita hivyo vilianza baada ya Ufaransa kuishambulia bandari ya Madras huko kusini mwa India, ambayo ilikuwa ikidhibitiwa na Waingereza. Ufaransa ilipigana ikiwa na wanajeshi elfu tatu dhidi ya Uingereza iliyokuwa na wapiganaji elfu 22. Mwezi Januari mwaka 1761, Ufaransa ilisalimu amri mbele ya Uingereza baada ya kikosi cha dhiba kushindwa kufika vitani.
Tarehe kama ya leo mwaka 1961 ardhi ya Tanganyika ambayo hii leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijikomboa na kupata uhuru. Tanganyika ilianza kukoloniwa na Ujerumani mwaka 1880 hadi mwaka 1919 wakati ilipoanza kukoloniwa na Uingereza na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa mkoloni huyo hadi ilipojipatia uhuru wake wa kujitawala katika tarehe kama ya leo. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na baadaye akachaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika.
Siku kama hii ya leo miaka 34 iliyopita, yalianza mapambano yasiyo na kikomo ya wananchi wa Palestina dhidi ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza. Mapambano hayo ya ukombozi ambayo ni mashuhuri kwa jina la "Intifadha ya Kwanza" yalianzishwa baada ya kushadidi mauaji na ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina na pia kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na utawala huo ghasibu. Hayo yalijiri baada ya wananchi Waislamu wa Palestina kukatishwa tamaa na hatua zilizokuwa zikichukuliwa na nchi za Kiarabu na taasisi nyingi za Palestina kwa ajili ya kurejeshewa haki zao.

Miaka 30 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti na kuutangaza utawala wa Baath wa Iraq kuwa ndio ulioanzisha vita vya miaka minane dhidi ya Iran. Katika siku hiyo, Javier Perez de Cuellar Katibu Mkuu wa wakati huo wa Umoja wa Mataifa alitangaza katika ripoti yake kuwa Iraq iliivamia Iran tarehe 22 Septemba mwaka 1980. Miji na vijiji vingi vya mpakani mwa Iran vilitekwa na kukaliwa kwa mabavu huku wanawake, watoto na wanaume wengi wakiwa wahanga wa vita hivyo vikubwa katika uvamizi huo ambao uliungwa mkono kwa hali na mali na nchi za Magharibi.

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia. Alizaliwa mjini Golpayegan moja ya miji ya Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi. Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mjini Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali.