Jan 31, 2022 03:58 UTC
  • Jumatatu tarehe 31 Januari 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 28 Jamadithani 1443 Hijria sawa na 31 Januari 2022.

Katika siku kama hii ya leo na miaka 853 iliyopita alifariki dunia Abul-Qasim al-Shatibi, msomi mashuhuri wa Qur'ani aliyekuwa maarufu kwa jina la Imamul Qurra. Abul-Qasim alizaliwa mwaka 538 Hijiria. Mbali na kuwa mtaalamu mkubwa katika taaluma ya usomaji wa Qur'ani, alikuwa pia mtaalamu wa elimu ya tajweed, tafsiri ya Qur'an, hadithi, sarufi ya lugha ya Kiarabu na elimu nyinginezo za kipindi hicho. Licha ya kuwa kipofu lakini alisifika kwa kuwa hodari na alifanikiwa kuhifadhi hadithi nyingi kifuani mwake. Msomi huyo wa Kiislamu ameacha athari kwa vizazi vya baada yake na miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kitabu kiitwacho "al Qasidatus Shatwibiyyah" kilichokusanya masuala yanayohusiana na elimu ya tajweed.

Siku kama ya leo miaka 423 iliyopita, ilianzishwa kampuni ya kwanza ya Uingereza ya India Mashariki nchini India kwa amri ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza. Kampuni hiyo iliimarisha ukoloni wa Uingereza katika maeneo yenye utajiri huko kusini mwa Asia na baada ya hapo shughuli za ukoloni zikaimarika zaidi katika mataifa ya kusini mwa Asia kupitia kampuni hiyo. Baada ya kuasisiwa kampuni hiyo, nchi nyingine kama vile Uholanzi, Ureno na Ufaransa zilielekeza nguvu zao katika bara Hindi kwa lengo la kuhudumia ukoloni wao. Baada ya karne 3 za kuanzishwa shirika hilo, ushawishi na kuimarika utawala wa Uingereza nchini India vilisababisha nchi hiyo kutangazwa kuwa sehemu ya Uingereza na Malkia Viktoria akavikwa taji la kuwa mtawala wa India na Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 172 iliyopita, ilianzishwa harakati kubwa ya uasi wananchi wa China iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Taiping. Harakati hiyo ilitokana na hali mbaya na umasikini uliokuwa ukiwasumbua wananchi wa nchi hiyo na hasa matabaka ya watu wa vijijini, iliyosababishwa na ukoloni wa kigeni na utawala wa familia isiyofaa ya Manchu. Lengo kuu la harakati hiyo iliyodumu kwa muda wa miaka 14 lilikuwa ni kuwepo usawa katika kugawana ardhi kati ya wanawake na wanaume.

Miaka 141 iliyopita mwafaka na siku kama ya leo, alifariki dunia alim na fasihi wa Kiirani Mirza Muhammad bin Sulaiman Tankabani. Mbali na kubobea katika elimu ya fiq'hi, Tankabani pia alikuwa mtaalamu katika fasihi na mshairi mkubwa katika kipindi chake. Muhammad bin Suleiman ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na "Al Fawaidu fii Usuliddin" na " Qisasul-Ulama." Katika kitabu hicho kilichochapishwa mara kadhaa nchini Iran alizungumzia maisha ya maulama wa kabla yake.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita gwaride la mwisho na kimaonyesho la vikosi vya majeshi ya utawala wa Shah lililokuwa na lengo la kuwatia hofu na woga wananchi Waislamu wa Iran, lilifanyika katika mitaa mbalimbali ya Tehran. Katika gwaride hilo, wanajeshi wengi walionesha mshikamano wao na kuungana na wananchi Waislamu wa Iran na kuamua kuanza mapambano dhidi ya utawala wa kibeberu wa Shah.

Askari wa Shah