May 29, 2022 03:25 UTC
  • Jumapili, 29 Mei, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 27 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria mwafaka na tarehe 29 Mei mwaka 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1102 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa malenga wa Kiirani Abu Is'haq Kesa-i Marvazi. Kipindi cha ujana wake kiliambatana na kumalizika kwa kipindi cha utawala wa Wasamani na mwanzoni mwa zama za utawala wa Waghaznavi. Kwa sababu hiyo malenga huyu Mfarsi alitunga mashairi kadhaa ya kusifu tawala hizo mbili. Fauka ya hayo Marvazi alitunga beti kadhaa za mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad na (sww) na kizazi chake hasahasa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Kesa-i Marvazi mbali na kusifika kwa utunzi wa mashairi, lakini pia alitoa waadhi na hekima kupitia mashairi yake ya Kifarsi. Malenga huyu mkubwa wa Kiirani ameandika ya mashairi. ***

Kesa-i Marvazi

 

Siku kama ya leo miaka 569 iliyopita sawa na tarehe 29 Mei 1453 vikosi vya Sultani Muhammad Fatih, mtawala wa dola ya Othmaniya vilidhibiti bandari ya Constantinople iliyokuwa makao makuu ya Mfalme wa Roma ya Mashariki. Amri ya kwanza iliyotolewa na Muhammad Fatih baada ya kuudhibiti mji huo ilikuwa ni kudhaminiwa usalama na uhuru wa wakazi wake. Mfalme huyo alitoa amri ya kukarabatiwa mji huo na kujengwa msikiti, ambao leo hii unajulikana kwa jina la Msikiti wa Sultan Muhammad. Mwaka 1930 mji wa Constantinople ulibadilishwa jina na kuitwa Istanbul, lenye maana ya "mji wa Uislamu" na ni miongoni mwa miji muhimu zaidi ya Uturuki. Mji huo uko magharibi mwa nchi hiyo. ***

Bandari ya Constantinople

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 321 iliyopita, sawa na tarehe 29 Mei mwaka 1701 alizaliwa Anders Celsius mwanafizikia na mtafiti wa Sweden. Familia yake ilikuwa ya wasomi na baba na babu yake walikuwa wanahisabati. Celsius alivutiwa sana na elimu ya nujumu na mwaka 1730 alifanikiwa kuwa mwalimu wa somo hilo katika Chuo Kikuu cha Uppsala. Mwaka 1742 alipendekeza kutumika daraja ya kipima joto kwa mujibu wa Celsius, iliyoitwa kwa jina lake. Mpangilio huo ulikubaliwa rasmi na kuanza kutumika duniani mwaka 1945, mwaka mmoja baada ya kufariki dunia mwanafizikia huyo. ***

Anders Celsius

 

Miaka 113 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 29 Mei 1908 helikopta ya kwanza iliruka angani kwa mafanikio. Mtengenezaji wa helikopta hiyo alikuwa Igor Sikorsky, raia wa marekani mwenye asili ya Poland. Utengenezaji wa chombo hicho cha angani ulifungua ukurasa mpya katika mawasiliano na safari za anga. Chombo hicho kilikuwa na sifa kadhaa maalumu zikiwemo za kupaa angani kwa kwenda mbele na kurudi nyuma na pia kuweza kutua na kupaa kikiwa wima. Helikopta hiyo pia iliweza kutulia sehemu moja angani bila kufanya harakati yoyote ile. ***

Helikopta

 

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita muwafaka na tarehe 29 Mei 1953, Edmund Hillary mpanda milima kutoka New Zealand na Tenzing Norgay mpanda milima kutoka Nepal walifanikiwa kufika kilele cha mlima Everest, ambao ni mlima mrefu zaidi duniani. Mlima wa Everest wenye urefu wa mita 8,848, ni kilele kirefu zaidi cha silsila ya milima ya Himalaya nchini Nepal. Baada ya Hillary na Norgay kufanikiwa kupanda mlima huo mwaka 1953, makundi mengine ya wapanda milima kutoka katika nchi nyingine duniani pia yaliweza kukwea kilele cha mlima huo katika miaka iliyofuata. ***

Kilele cha mlima Everest

 

Na miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 8 Khordad mwaka 1368 Hijiria Shamsia alifariki dunia Ayatullah Mir Sayyid Ali Fani Isfahani msomi wa Kiislamu. Alizaliwa katika mji wa Isfahan mwaka 1294 Hijira Shamsia na alianza kujifunza elimu ya msingi ya Kiislamu akiwa na miaka 9. Alimu huyo alistafidi na maulama wakubwa na kufikia daraja ya ijtihad ambapo alihamia Najaf nchini Iraq na kwa muda wa miaka 30 alifundisha kwenye mji huo masomo ya fikih, usul, ilmul qalam na akhlaq. Mwaka 1352 Hijria Shamsia alirejea Iran na kuendelea kufundisha mjini Qum. Miongoni mwa vitabu vya Ayatullah Mir Sayyid Ali Fani Isfahani ni Sheria za Haja na Umrah, Fawaidul Rijaliyah, Arubain Hadith na Tafsiri ya Suratul Faatiha. ***

Ayatullah Mir Sayyid Ali Fani Isfahani

 

Tags