Jumanne, 31 Mei, 2022
Leo ni Jumanne tarehe 29 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria sawa na tarehe 31 Mei 2022.
Siku kama ya leo miaka 1493 iliyopita, sawa na tarehe 31 Mei 529, dini ya Ukristo ilitambuliwa rasmi huko Roma kwa amri ya Constantine, mfalme wa wakati huo wa Roma. Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wakifanya ibada zao kwa siri huko Roma. Mwaka 324 Miladia Mfalme Constantine aliamua kuhamia Byzantine, mji ambao alikuwa ameutangaza kama mji mkuu wa ufalme wake ambao uliojengwa na Wagiriki yapata karne nane kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (as). Miaka sita baadaye na baada ya kuhamia huko mfalme huyo, dini ya Ukristo ikatangazwa na kutambuliwa rasmi na wafuasi wake wakaruhusiwa kuabudu kwa uhuru. ***
Katika siku kama ya leo miaka 238 iliyopita, Ayatullah Agha Muhammad Baqir Wahid Bahbahani fakihi mkubwa wa Kishia aliaga dunia. Allama Bahbahani ni mmoja wa mafakihi wakubwa zaidi ambaye licha ya kupita miaka mingi angali anahesabiwa kuwa msomi mbobezi wa taaluma mbalimbali. Allamah Bahbahani aliweka jiwe jipya la msingi la elimu ya Usul na akaihuisha elimu hii muhimu. Msomi huyu alifanya hima na juhudi kubwa kulinda Ijitihadi na alisimama imara kupambana na mrengo wa Akhbariyuun. ***

Miaka 190 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Évariste Galois, mwanahisabati aliyekuwa na kipawa cha juu wa Ufaransa. Alizaliwa tarehe 26 Oktoba mwaka 1811 karibu na mji wa Paris. Hadi anafikia umri wa miaka 12 hakuwa na mwalimu mwingine ghairi ya mama yake na kutokana na kipawa cha hali ya juu cha elimu alianza kusoma vitabu mbalimbali vya historia na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo. Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha Ukweli wa Hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa. Galois aliuawa akiwa na umri wa miaka 21 sawa na tarehe kama ya leo mwaka 1832 Miladia, baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa. Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani. ***

Katika siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, yaani tarehe 31 Mei mwaka 1910, nchi ya Afrika Kusini iliundwa katika eneo la kusini mwa Afrika kwa kuunganishwa makoloni mawili ya Uingereza na kupewa uhuru. Muungano huo ulipata uhuru kamili mwaka 1931. Hata hivyo hatamu za madaraka ya nchi zilikuwa mikononi mwa wazungu wachache. Mwaka 1991 wazungu makaburu walilazimika kuhitimisha mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid katika nchi hiyo baada ya mapambano ya miaka mingi ya Waafrika Kusini wazalendo wakiongozwa na shujaa Nelson Mandela. ***

Na siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 31 Mei 2010, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel walishambulia msafara wa meli zilizosheheni misaada ya kibinadamu kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza waliozingirwa na utawala huo. Shambulio hilo lilipelekea watu 9 kuuawa na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa. Msafara huo uliokuwa na wanaharakati 663 kutoka nchi 37 duniani, ulikuwa umebeba shehena ya misaada ya dawa na chakula kwa ajili ya wananchi wa Ukanda wa Ghaza wanaokabiliwa na mzingiro wa kidhulma wa Wazayuni. Shambulio hilo la kinyama lililaaniwa vikali na mataifa mbalimbali duniani, na hatimaye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likatoa azimio la kufanyika uchunguzi wa haraka na usiopendelea upande wowote kwa lengo la kubaini na kuwekwa wazi wahusika wa jinai hizo. ***
