Jun 01, 2022 01:20 UTC
  • Jumatano, 01 Juni, 2022

Leo ni Jumatano tarehe Mosi Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1443 Hijria mwafaka na tarehe Mosi Juni 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1270 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya wanahistoria, alizaliwa Bibi Fatima Maasuma, binti yake Imam Musa al-Kadhim (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Bwana Mtume (SAW). Fatima Maasuma (as) alikuwa hatibu hodari, mwalimu mahiri, zahidi na mcha-Mungu mkubwa. Alipatwa na maradhi alipokuwa njiani kuelekea Khorasan huko Kaskazini Mashariki mwa Iran kwa ajili ya kumtembelea kaka yake yaani Imam Ali bin Musa al Ridha (as) na akafariki dunia katika mji mtakatifu wa Qum baada ya kukaa hapo kwa siku 17. Leo hii ziara la mtukufu huyo linatembelewa na mamilioni ya waumini kila mwaka kutoka pembe mbalimbali za dunia. ***

Kaburi la Bibi Fatma Maasuma (as) mjini Qum

 

Katika siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, aliaga dunia John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alizaliwa 20 Oktoba mwaka 1859 na alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri alivyoviandika katika kipindi cha uhai wake ni pamoja na "How we think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture." John Dewey alifariki dunia mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93. ***

John Dewey

 

Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Chama cha Jamhuri ya Kiislamu kilichokuwa chama kikukwa na jumuishi zaidi baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, kilivunjwa kwa pendekezo la wajumbe na makada wake. Chama cha Jamhuri ya Kiislamu kilitangazwa kuanzishwa na Ayatulla Sayyid Hussein Beheshti, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani na Dakta Muhammad Javad Bahonar ikiwa ni wiki moja tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979. Lengo la kuanzishwa chama hicho lilikuwa ni kuwa na kikundi chenye nguvu na kuleta harakati amilifu sambamba kuleta mshikamano na nidhamu. Katika kipindi cha harakati zake, chama hiki kilikuwa na ushiriki mkubwa katika harakati za kijamii na katika medani zote za kisiasa. ***

 

Na katika siku kama ya leo miaka 23 iliyopita, Dakta Mahdi Roshan Zamir mwanafasihi na mtalamu wa lugha wa Kiirani aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1298 katika mji wa Tabriz kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kupitisha kipindi cha masomo ya msingi na kisha masomo ya kati, Mahdi Roshan Zamir mwaka 1316 alielekea Tehran mji mkuu wa Iran kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Baada ya hapo, aliondokea kuwa mwalimu huku akiendelea na masomo pia. Alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tabriz kwa muda wa miaka 27. Mahdi Roshan Zamir ameandika vitabu vingi kama ambavyo ametarjumu vitabu kadhaa. Mtaalamu huyu wa lugha aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 80. ***

Dakta Mahdi Roshan Zamir (wa kwanza kushoto)