Jun 05, 2022 02:35 UTC
  • Jumapili, 05 Juni, 2022

Leo ni Jumapili tarehe 5 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Juni 2022 Miladia.

Miaka 779 iliyopita katika siku kama ya leo, tarehe 5 Dhulqaadah mwaka 664 Hijria aliaga dunia Ridha-ddin, Ali bin Musa, maarufu kwa jina la Sayyid Ibn T'aawus; faqihi, mtaalamu wa Hadithi, mwanahistoria na mwanafasihi wa Kiislamu. Ridha-ddin alizaliwa mwaka 589 katika mji wa Hilla nchini Iraq. Alianza kuchota hazina ya elimu kwa baba yake aliyekuwa alimu mkubwa, Saadu-ddin Abu Ibrahim na pia kwa babu yake Warram Ibn Abi Farras na baadaye akajiongezea maalumati ya elimu za dini kwa maulamaa wengine wa mji wa Hillah. Alijulikana na watu wote kwa uchamungu na zuhdi ya kuipa mgongo dunia na ndiyo maana hakukubali kuhudumu katika cheo chochote alichopewa na watawala wa Bani Abbas. Ibn T'aawus alikuwa na hadhi na itibari kubwa kati ya maulamaa wa zama zake. Athari mbalimbali alizoacha katika Ilmul-kalam, akhlaqi, fiqhi na Hadithi zimesalia hadi leo na nyingi zao zimetarjumiwa na kuchapishwa mara kadhaa. Moja ya vitabu muhimu vya Ibn T'aawus kinaitwa Al-Lahuuf kinachozungumzia matukio ya Siku ya Ashura, ambacho ni miongoni mwa vitabu vya kutegemewa sana kuhusu historia ya Uislamu. Kitabu chake chengine ni Al-Malaahim wal-Fitan kinachohusu yatakayojiri kabla na wakati atakapodhihiri Imam Mahdi (AS). Alimu huyo mtajika aliandaa wanafunzi waliobobea katika elimu, miongoni mwao ni baba yake Allama Hilli na Allama Hilli mwenyewe.

 

Sayyid Ibn T'aawus

Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo yalianzishwa mapambano ya wapigania ukombozi Wairani yaliyoongozwa na Mirza Kuchak Khan Jangali dhidi ya utawala wa kiimla na uliokuwa dhalili wa Qajar na dhidi ya uporaji wa utajiri wa Iran uliokuwa ukifanywa na mkoloni Muingereza; ambapo siku iliyofuata yaani tarehe 6 Juni Mirza Kuchak Khan alitangaza "serikali ya muda ya Jamhuri". Kazi ya kuratibu harakati ya mapambano hayo ilitekelezwa na Kamati ya Umoja wa Uislamu iliyoundwa kwa ilhamu aliyopata katika fikra za wanafikra na warekebishaji umma kama Sayyid Jamaluddin Asad Abadi, Sayyid Abdurahman Kawakibi na Sheikh Muhammad Abdou; lengo likiwa ni kuleta umoja baina ya nchi za Kiislamu kwa madhumuni ya kupambana na watawala madikteta na ushawishi wa maajinabia. Kwa mtazamo wa Mirza Kuchak Khan hali ya Iran ilikuwa ya tafrani; na nchi ilikuwa imedhibitiwa na maajinabia. Kwa kufuata mielekeo ya umoja wa Uislamu alidhamiria kuunda vuguvugu la kijeshi kwa ajili ya kupambana na udikteta wa ndani na ukoloni wa nje ili kuiokoa Iran. Licha ya mapambano yaliyoendeshwa na Mirza Kuchak Khan na wafuasi wake, baadhi ya waungaji mkono wa utawala wa kikomunsti wa Urusi waliokuwemo kwenye safu za wafuasi wake waliifanyia uhaini na usaliti harakati yake. Hatimaye tofauti za baina ya viongozi na njama za wakoloni wa nje ziliivuruga harakati ya Mirza Kuchak Khan na pigo la mwisho lililoizima harakati hiyo lilikuwa ni la kuuliwa Mirza mwenyewe na utawala wa Reza Khan Pahlavi.

 

Mirza Kuchak Khan

Miaka 75 iliyopita, yaani tarehe Juni 1947 George Marshall, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Marekani alitangaza mpango wa utoaji mkopo wa dola bilioni tano wa kuzisaidia nchi kadhaa za Ulaya Magharibi zilizokuwa zimeathiriwa na vita. Lengo la mpango huo uliokuwa maarufu kama "Mpango wa Marshall" lilikuwa ni kuzikarabati na kuzijenga upya nchi wafuasi wa Marekani, kufutilia mbali uwezekano wa kujitokeza mielekeo ya Ukomunisti katika nchi hizo; na muhimu zaidi kuliko yote kupanua satua ya kiuchumi na kuhodhiwa Ulaya kisiasa na Marekani. Mkopo huo wa Marekani uliopambwa na nguvu za kijeshi na kipropaganda za serikali ya Washington, uliibadilisha nchi hiyo; na kwa muda mrefu baadaye ikaja ikawa moja ya madola mawili makuu yenye nguvu duniani sambamba na Urusi.

George Marshall

 Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano makubwa ya kuupinga utawala wa Shah baada ya kupata habari kuwa Imam Khomeini (MA) amekamatwa. Siku chache baada ya Imam Khomeini kukamatwa na maafisa wa usalama kwa sababu hotuba kali na ya kihistoria aliyotoa katika chuo cha Fayziyah mjini Qom iliyofichua maovu ya utawala wa Shah, maandamano ya wananchi Waislamu wa Iran ya kupinga kukamatwa kwake yalianza. Askari wa vikosi vya usalama walikabiliana na vuguvugu hilo kubwa la umma kwa mkono wa chuma, kwa kuwashambulia vikali waandamanaji; na matokeo yake, watu wengi wakauawa shahidi na kujeruhiwa. Kwa hakika mapambano hayo ya damu na ya kihistoria ya wananchi Waislamu wa Iran ya Khordad 15, yaliyosadifiana na tarehe hiyo ya kalenda ya Kiirani ya Hijria Shamsia, ilikuwa ndio cheche iliyoanzisha mapinduzi ya umma dhidi ya utawala wa Kipahlavi na ndiyo yaliyokuja kuainisha hatima ya kisiasa na kijamii ya baadaye ya Iran. Baada ya tarehe hiyo mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yakiongozwa na Imam Khomeini yaliendelea hadi ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu tarehe 22 Bahman 1357 Hijria Shamsia (Februari 11, 1979).

Khordad 15, 1342

Na siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, yaani tarehe 5 Juni 1967 vita vya tatu vikubwa kati ya utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel na nchi za Kiarabu vilianza. Katika siku hiyo jeshi la anga la utawala wa Kizayuni lilifanya shambulio la kushtukiza kwa kuvuka mipaka ya nchi tatu za Misri, Syria na Jordan; na kwa muda wa masaa mawili, vikosi vya anga vya nchi hizo vilishambuliwa vikali na takriban vilisambaratishwa kikamilifu. Baada ya hujuma na uvamizi huo, jeshi la nchi kavu la utawala wa kizayuni, likitumai silaha za kisasa na kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani na Uingereza, likafanikiwa ndani ya muda wa siku sita kuyashinda majeshi ya nchi hizo tatu. Katika uvamizi wa pande zote wa Juni 1967, utawala wa kizayuni ulivamia na kukalia kwa mabavu eneo zima la Jangwa la Sahara na kingo za mashariki ya Mfereji wa Suez wa Misri na pia miinuko ya Golan ya Syria; na ni baada ya kuitenganisha Magharibi ya Jordan na nchi hiyo na kuukalia kikamilifu mji wa Baitul Muqaddas ndipo ukakubali usitishaji vita. Kushindwa vibaya Waarabu katika Vita vya Siku Sita kuliwezekana kwa ushirikiano wa karibu uliokuwepo kati ya mashirika ya ujasusi ya Marekani na Uingereza na shirika ujasusi la utawala huo la Mossad.

Vita vya Siku Sita vya Waarabu na Israel

 

Tags