Jun 22, 2022 07:53 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi 13

Assalaama Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Hii ni sehemu ya 13 katika mfululuzi wa vipindi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambavyo vinazungumzia na kujadili sifa na fadhila za Imam Hassan na Hussein (as) katika Qur'ani na Hadhithi, watukufu wawili ambao ni wajukuu wa Mtume wa Uislamu, Muhammad al-Mustafa (saw).

Karibuni tuwe pamoja hadi mwisho wa kipindi hiki ambapo tutajadili angaa kwa ufupi, ubora wa watukufu hawa pamoja na Mtume (saw) juu ya viumbe wote kama Qur'ani Tukufu na Riwaya za Kiislamu zinavyotuthibitishia hilo. Tunaanza kipindi cha leo kwa kujadili waliokusudiwa katika kauli ya Mwenyezi Mungu katika Aya ya 119 mwishoni mwa Sura ya Tauba inayosema: Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli.

Wapenzi wasikiliza, wito huu mtakatifu wa mbinguni bali taklifu takatifu inaelekezwa kwa watu wenye imani, hisia safi na watiifu kwa Muumba wao na hilo linatokana na mambo mawili muhimu. Jambo la kwanza ni takwa juu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa maana ya kutekeleza mambo ya wajibu na kuacha yaliyoharamishwa na kujiepusha na yale yote yanayomghadhabisha na yasiyomridhisha, bali anachukia kuona yakitekelezwa na waja wake. Ni wazi kuwa jambo hilo halifikiwi ila na wale walio na bahati na hadhi ya hali ya juu kiimani. Ama jambo la pili, wapenzi wasikilizaji, ni kuandamana na kuwa pamoja na watu wakweli, hili likiwa na maana ya kushirikiana na kusuhubiana na watu wema na wakweli katika kila jambo wanalofanya. Usuhuba huu pia imearifishwa kuwa ni kuiga na kuwafuata watu hao wema na wakweli, wakiongozwa na Mtume Mtukufu (saw), kwa maneno na matendo pamoja na kuwapenda na kuwanusuru katika kila jambo linalofungamana na mafundisho ya dini bila kuwafanyia hiana. Watukufu hao wanapasa kutiiwa kwa kila njia na kutopingwa amri na makatazo yao kama inavyosema Aya ya 7 ya Surat al-Hashr: Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho.

*************

Na sasa, ndugu wasikilizaji, swali hili muhimu linajitokeza hapa kwamba je, ni nani hawa ambao wametajwa na kuarifishwa na Mwenyezi Mungu kuwa ni wakweli na ambao waumini wameamrishwa kuwa pamoja nao daima na kutofarakiana nao maishani? Hili, bila shaka, ni swali muhimu mno linalohitajia utafiti na uchunguzi mkubwa wa kielimu kwa sababu amri ya Mwenyezi Mungu ni taklifu ya kidini ambayo inaainisha mustakbali na maisha ya mja. Hii ni kutokana na ukweli kuwa kupinga amri ya Mwenyezi Mungu ni maasi na dhambi kubwa inayotokana na ukaidi na upotovu, na tunamwomba Mwenyezi Mungu atuepushie mbali hilo!

Uchunguzi mfupi na wa haraka haraka tu wa Aya za Qur'ani Tukufu zinazozungumzia sifa za wakweli unabaini wazi kwamba wao ni watu walio na imani thabiti na ya dhati kuhusiana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Siku ya Mwisho, Malaika, Vitabu vya mbinguni na Mitume (as), imani ambayo hailegilegi wala kuingiwa na shaka na kusitasita. Kwamba wao ni watu wanaojitolea na kuwekeza kwenye njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali na nafsi zao, husimamisha Swala, hutoa Zaka na kutekeleza ahadi za Mwenyezi Mungu na Mtume wake, huwa pamoja na watu na ni wenye kusimama imara wakati wa shida na vita, ni wenye kupigana jihadi kwa njia ya Mwenyezi Mungu kama anavyotaka yeye Mungu Muumba ambapo matokeo yake huwa ni kuwaletea heri wanadamu na kuwakinga na shari.

Wapenzi wasikilizaji, ni wazi kuwa sifa hizi zilizokamilika, za kipekee na za hali ya juu kimaanawi hazipatikani ila kwa maasumina ambao wametakazwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe na kuwapa fadhila za kipekee na kuwafanya kuwa viumbe bora zaidi wanaopaswa kuwa ruwaza njema inayostahiki kuigwa na kufuatwa na waja wengine wote.

Kwa msingi huo, masahaba na tabeena wote walifahamu kwamba swadiqeen yaani wakweli waliokusudiwa katika Aya tofauti za Qur'ani Tukufu na Hadithi ni Ahlu Bait wa Mtume (saw). Kiasi kwamba al-Khawarazmi al-Hanafi amenukuu katika kitabu chake cha al-Manaqib na al-Qanduzi al-Hanafi katika kitabu cha Yanabiul Mawadda, Al-Hafidh as-Suyuti as-Shafii' katika ad-Durr al-Manthur na wengine wengi kwamba Ibn Abbas alifasiri neno 'as-Swadiqeen' yaani 'wakweli' katika Aya tuliyotangulia kuisoma kuwa ni Ali bin Abi Talib (as). Amenukuliwa katika Riwaya nyingine akisema maana yake ni: 'Kuweni pamoja na Ali.....' Amenukuliwa akisema katika sehemu nyingine: 'Swadiqun katika Aya hii ni Muhammad (saw) na Watu wa Nyumba yake.' Hili ni jambo ambalo ameliashiria pia Hakim al-Hasakani al-Hanafi katika tafsiri yake ya Shawahid at-Tanzil katika kufafanua maana ya 'na kuweni pamoja na wakweli' akimnukuu Malik bin Anas kutoka kwa Nafi' kwamba Abdallah bin Omar bin al-Khattab alisema katika kufafanua suala hili: 'Yaani Muhammad na Ahli zake.' Hii ni katika hali ambayo Sibtbin al-Jauzi al-Hanafi ameandika katika kitabu chake cha Tadh'kirat Khawaas al-Aima kwamba: 'Maulama wanasema kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema, 'na kuweni pamoja na wakweli' kwamba maana yake ni: Kuweni na Ali na Ahli zake (as).'

************

Mambo yaliyosisitizwa na vitabu na marejeo mengine kuhusiana na suala hilo ni mengi mno na muhtasari ni kuwa yote yanasisitiza juu ya maana hii tuliyoiashiria hivi punde. Al-Qanduzi al-Hanafi ananukuu Hadithi iliyonukuliwa na al-Hafidh Abu Naeem kutoka kwa Maimamu wawili Baqir na Ridha (as) kwamba walisema katika kutafsiri maana ya Aya hii: 'As-Swadiqun ni Maimamu wa Ahlul Bait (as).' Al-Muzi amesema katika kitabu cha Tahdhib al-Kamal akimnukuu Imam Swadiq (as) kwamba as-Swadiqun' ni Muhammad na Ali (as).

Ama al-Juwayni as-Shafi' amenukuu katika kitabu chake cha Faraid as-Simtain ukumbusho wa Imam Ali Amir al-Mu'mineen (as) alipowalalamikia wale walioghusubu ukhalifa wake kwa kuwaambia: Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli. Na kwamba Salman al-Farisi aliuliza:  Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, Aya hii inawahusu watu wote au watu maalumu tu? Mtume (saw) akajibu: Ama neno 'Mu'minun' linawahusu waumini wote ambao wameamrishwa kuwa na takwa na kumuogopa Mwenyezi Mungu, lakini neno 'Swadiqeen' linawahusu watu maalumu pekee nao ni Ali na mawasii wake baada yake, hadi Siku ya Kiama.'

Na mwishoni wapenzi wasikilizaji tunatazama baadhi ya rai na maoni ya maulama kuhusiana na Aya ya Swadiqun na dalili zenye nuru wanazotoa kuhusiana na suala hili. Allama Hilli anasema katika kitabu chake cha Minhajul Karama: 'Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuwajibisha kuwa pamoja na watu wanaofahamika kuwa na ukweli ndani yao, na jambo hili haliwezekani ila kwa maasumu, kwa sababu wasiokuwa wao wanaweza kusema uongo.'

Sharaf ad-Deen al-Astar Abadi katika kitabu chake cha Ta'weel al-Ayaat ad-Dhwahira: 'Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaamrisha waja wake wenye taklifu, wawe pamoja na wakweli na kuwafuata. Na mtu mkweli ni yule ambaye maneno na vitendo vyake vinaambatana na ukweli na kamwe hasemi uongo, na bila shaka hizi ni katika sifa za maasumu.'

Ama Sayyid Sharaf ad-Deen al-Musawi anasema katika Murajaat: 'As-Swadiqun' katika Aya hii tukufu ni: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu na Maimamu kutoka kizazi chake kitakatifu kwa mujibu wa vitabu vyetu vingi vya Hadithi.'

Na kufikia hapa ndugu waumini, tunafikia ukweli na uthibitisho wa Aya hii tukufu kwamba wakweli hawa ni watu maasumu ambao hawatendi dhambi kwa vyovyote vile. Aya hiyo hiyo pia inatuamrisha sote Waislamu kuwafuata wakweli hawa ambao ni maasumu kwa sababu kufanya hivyo hakuna matokeo mengine isipokuwa kufikia ukweli, wokovu, heri na fadhila.

Hao ndio Ahlul Bait wa Mtume Muhammad al-Mustafa (saw) ambao ni Ali, Hassan, Hussein na Maimamu wengine tisa wanaotokana na kizazi cha Aba Abdillah Hussein na Bwana wa Wakweli Muhammad al-Amin (saw). Heri kwa wanaowafuata na kuwahutubu kwenye ziara zao kwa kuwaambia: Tuko pamoja na nyinyi, tuko pamoja na nyinyi na sio wasiokuwa nyinyi……tuko pamoja na nyinyi tuko pamoja na nyinyi na sio na maadui wenu!!

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa yake Mola, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.