Jun 24, 2022 01:15 UTC
  • Ijumaa tarehe 24 Juni 2022

Leo ni ijumaa tarehe 24 Dhulqaada 1443 Hijria sawa na Juni 24 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1243 iliyopita Imam Ali bin Musa Ridha (a.s) alianza safari yake kutoka Madina kuelekea Marv huko kaskazini mashariki mwa Iran ya zamani. Imam Ridha (a.s) alifanya safari hiyo kwa kulazimishwa na kushinikizwa na Maamun, khalifa na mtawala wa saba wa ukoo wa Bani Abbas. Lengo la safari hiyo lilikuwa kumuweka Imam Ridha chini ya uangalizi. Maamun alitoa pendekezo kwa Imam huko Marv kwamba akubali kuwaa mrithi wake. Maamun alifanya hivyo ili kujionyesha kuwa ni mtu mwenye mapenzi na Watu wa  Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (s.a.w). Hata hivyo katika fursa mbalimbali Imam Ridha si tu kwamba alionyesha kuwa hakubali kushirikiana na  utawala wa Bani Abbas, bali pia aliutambua utawala huo kuwa ni wa kupenda makuu na wa kidhalimu.

Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, Napoleone Bonaparte mtawala wa Ufaransa akiwa na kikosi cha askari 350,000 alianza kufanya mashambulio dhidi ya utawala wa Russia wa Tsar. Miaka mitano kabla ya tukio hilo, nchi mbili hizo zilikuwa zimetiliana saini mkataba wa kutoshambuliana kijeshi. Hata hivyo taratibu uhusiano baina ya tawala mbili hizo ulianza kuharibika, na hivyo kumfanya Bonaparte afikie hatua ya kuandaa jeshi kubwa na kuishambulia Russia na kisha kusonga mbele hadi katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow. Hata hivyo hali mbaya ya hewa yaani baridi kali na kutowafikia wanajeshi wa Kifaransa vifaa muhimu na suhula za kivita, kuliwafanya askari hao wakabaliwe na hali ngumu katika medani ya vita. Hali hiyo ilimlazimisha Bonaparte atoe amri ya kurejea nyuma vikosi vyake. Wakati wa kujiri zoezi hilo, askari jeshi wapatao 30,000 wa Kirusi waliwashambulia askari wa Bonaparte na kuwaua wengi miongoni mwao. Akiwa amebakiwa na askari 30,000 tu, Bonaparte aliikimbia Russia na kufanikiwa kuwasili Paris Ufaransa Desemba mwaka 1812.

Napoleone Bonaparte

Tarehe 24 Juni miaka 210 iliyopita, Caracas mji mkuu wa Venezuela ulidhibitiwa na Simon Bolivar wakati wa mapambano ya mpigania uhuru huyo dhidi ya wakoloni kwa ajili ya kuyakomboa maeneo ya Amerika ya Kusini. Mkoloni Muhispania alishindwa katika vita hivyo vilivyodumu kwa kipindi cha chini ya mwaka mmoja na baada ya ushindi huo Simon Bolivar anayejulikana kama shujaa wa mapambano dhidi ya wakoloni huko Amerika Kusini, aliasisi Shirikisho la Colombia Kubwa. Shirikisho hilo lilijumuisha nchi za Venezuela, Colombia, Panama na Ecuador, na Bolivar alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa shirikisho hilo.

Na siku kama ya leo miaka 179 iliyopita, tanuu za feleji maarufu kwa jina la tanuu za Bessemer zilivumbuliwa. Mvumbuzi wa tanuu hizo alikuwa Mwingereza Henry Bessemer. Tanuu hizo zilitumika huko Uingereza kwa mara ya kwanza na leo hii zinatumika katika masuala mbalimbali viwandani.

Henry Bessemer