Jun 27, 2022 01:20 UTC
  • Jumatatu tarehe 27 Juni 2022

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Dhulqaada 1443 Hijria sawa na Juni 27 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita inayosadifiana na 27 Juni 1977, nchi ya Djibouti iliyoko karibu na eneo la Pembe ya Afrika ilipatia uhuru  kutoka kwa mkoloni Mfaransa baada ya kupita miaka kadhaa ya harakati ya kupigania uhuru. Tokea mwaka 1896 nchi hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Somalia Ufaransa na kuwa chini ya himaya ya Ufaransa, lakini baada ya kupita miongo minane, hatimaye nchi hiyo ilipata uhuru. Djibouti ilikuwa nchi ya mwisho kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na inahesabiwa kuwa nchi muhimu iliyoko katika eneo la kiistratijia kwa kuwa inapakana na Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi, kwenye eneo la lango bahari la 'Bab Mandab'. 

Bendera ya Djibouti

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, sawa na tarehe 6 Tir 1360 Hijria Shamsia, Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akiwa mjumbe wa Imam Khomeini katika Baraza Kuu la Ulinzi na Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran, alinusurika kifo baada ya kundi la kigaidi la MKO Munafikiin kumtegea bomu wakati alipokuwa akitoa hotuba katika mojawapo ya misikiti ya Tehran. Kwenye tukio hilo la kigaidi, Ayatullah Khamenei alijeruhiwa vibaya mkono wake wa kulia. 

Ayatullah Ali Khamenei

Tarehe 27 Juni 1993, Marekani ilirusha makombora 23 huko Baghdad mji mkuu wa Iraq na pambizoni mwa mji huo. Shambulio hilo lilifanyika kwa kisingizo kwamba viongozi wa utawala wa zamani wa Iraq walitaka kumuuwa George Bush 'baba', Rais wa zamani wa Marekani wakati alipokuwa safarini nchini Kuwait mwezi April mwaka huo huo. Shambulio hilo lilipelekea watu sita kuuawa na jengo la makao makuu ya Taasisi ya Usalama ya Iraq liliharibiwa kabisa. 

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita Sheikh Hamad bin Khalifa Aal Thani aliyekuwa mrithi wa Amir wa Qatar alifanya mapinduzi dhidi ya baba yake. Sheikh Hamad alimuondoa madarakani baba yake, Sheikh Khalifa bin Hamad Aal Thani wakati Amiri huyo wa zamani wa Qatar alipokuwa safarini nchini Uswisi. Sheikh Khalifa ambaye alikuwa kiongozi wa Qatar tangu mwaka 1972 alifanya jitihada kubwa za kurejea madarakani lakini hakufanikiwa. Nchi ndogo ya Qatar iko kusini mwa Ghuba ya Uajemi na inapakana na Saudi Arabia. Nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.

Sheikh Hamad bin Khalifa Aal Thani

Na miaka saba iliyopita katika siku kama ya leo yaani 27 Dhulqaada mwaka 1436 Hijria Qamaria winchi kubwa ya ujenzi ilianguka katika eneo moja la Msikiti Mtakatifu wa Makka na kuua idadi kubwa ya mahujaji wa Baitullah al-Haram yaani Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Tukio hilo lilijiri Ijumaa saa 17:10 alasiri  Septemba 11 mwaka 2015 ambapo winchi hiyo ilipelekea watu 107 kupoteza maisha na wengine 238 kujeruhiwa. Aghalabu ya waliopoteza maisha walikuwa ni mahujaji kutoka nchi za India, Pakistan, Indonesia na Iran. Wakuu wa Saudia walisema winchi hiyo ilianguka kutokana na upepo mkali. Tukio hilo la kusikitisha lilionyesha uzembe wa hali ya juu wa utawala wa Saudia. Tukio hilo la kuanguka winchi na maafa ya Mina wakati wa Sikukuu ya Idul Adha mwaka huo huo ni kati ya matukio machungu zaidi yaliyoshuhudiwa katika ibada ya Hija.