Sibtain katika Qur'ani na Hadithi
Assalaam Alaikum Wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kwamba hamjapo popote pale mlipo wakati huu ambapo tunakuleteeni sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi.
Ndugu wasikilizaji, neema ya Mwenyezi Mungu ni jambo lenye umuhimu mkubwa mbalo mwanadamu kesho Siku ya Kiama ataulizwa juu yake, swali ambalo bila shaka halitakuwa ni la kutaka kujua jambo fulani, bali la kuwajibishwa na kutaka ajieleze ni kwa nini hakutekeleza mambo aliyopaswa kuyatekeleza. Mwenyezi Mungu anasema mwishoni mwa Surat al-Kauthar: Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema. Aya hii imebeba ujumbe mzito na muhimu unaomtanabaisha mwanadamu kwamba kuna watu ambao licha ya kuishi umri wao wote humu duniani huku wakineemeka na neema za Mwenyezi Mungu Muumba, lakini huwa hawachukua hata hatua moja ya kumshukuru Mungu kwa neema hizo. Hii ni pamoja na kuwa kushukuru neema ni jambo la wajibu na ni ibada, na ibada ni lengo la mwisho na kuu katika kuumbwa mwanadamu kama anavyosema Mwenyezi Mungu katika Aya ya 56 ya Surat adh-Dhaariyaat: Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.
Neema hizi wapenzi wasikilizaji ni nyingi mno kiasi kwamba hatuna uwezo wa kuzihesabu. Miongoni mwazo ni imani juu ya Mwenyezi Mungu, utume wa Mtume wake na Uimamu wa Maimamu watoharifu na ambao ndio makhalifa wa Mtume huyu Mtukufu (as). Neema nyingine muhimu ni kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake al-Mustafa pamoja na kizazi chake kitoharifu. Ni wazi kuwa miongoni mwa misingi ya mapenzi na mahaba kwa mtu na hasa watukufu wa kidini ni kutii na kuwafuata katika kila jambo wanalotuamrisha kulifanya au kuachana nalo. Bila shaka kila mja ataulizwa siku ya Kiama kuhusiana na suala hilo. Alkhawarazmi al-Hanafi anasema katika kitabu chake cha al-Manaqib na vilevile Ibn al-Maghazili as-Shafi' katika kitabu cha Manaqib Ali bin Abi Talib kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: 'Ninaapa kwa jina la yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake! Siku ya Kiama mja hatapiga hatua yoyote ila baada ya kujibu maswali manne atakayoulizwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu: Aliutumia umri wake kwenye mambo gani, alitumia vipi ujana wake, alipata vipi mali yake na kuitumia kwa njia gani na hatimaye kuhusiana na mahaba na mapenzi yake kwetu Ahlul Bait.'
***********
Ndugu wasikilizaji, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewahutubu wanadamu kwa kusema: Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema. Bila shaka ni haki ya Mwenyezi Mungu, mjuzi na mwenye hekima kuuliza, na pia ni haki ya waja wake kuuliza lakini swali watakalouliza kuhusiana na suala hilo ni hili kwamba: Je, ni neema zipi hizo tutakazoulizwa juu yazo, na kuwajibika kupata adhabu iwapo hatukunufaika nazo kama tulivyotakiwa kufanya?! Na hapa wapenzi wasikilizaji udharura wa kuwauliza Ahlul Bait wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) unadhihiri tena, ili wapate kutufahamisha ni neema gani hizo ambazo wanadamu wataulizwa na kuadhibiwa juu yazo?! Imam Ali Amir al-Mumineen (as), ambaye ni katika Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) anatujibu swali hili kwa kusema: 'Sisi ndio hizo neema ambazo zimekusudiwa kwenye Aya hii.' Sheikh Suleiman al-Qunduzi al-Hanafi anaashiria suala hili katika kitabu chake cha Yanabiul Maddati Ladhawil Qurba na pia al-Hakim bin Ahmad al-Baihaqi amenukuliwa akisema kwamba Mtume (saw) alisema: 'Ewe Ali! Jambo la kwanza atakaloulizwa mja baada ya kifo chake ni: Shahada ya La Ilaha Ila Allah, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwamba wewe ni Walii wa Waumini kwa kile alichokijaalia Mwenyezi Mungu na nikakijaalia mimi pia.' Hii ni katika hali ambayo al-Kulaini anamnukuu Abu Khalid al-Kabuli katika kitabu chake cha al-Kafi baada ya kula chakula katika nyumba ya Imam Baqir (as) akisema: 'Nifanywe kuwa fidia kwako! Nilikuwa sijawahi kula chakula kitamu na kisafi kama hiki, lakini nikasoma Aya inayosema: Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema. Imam (as) akajibu kwa kusema: La sivyo, atakuulizeni kuhusu haki mnayoifuata, yaani Wilaya (uongozi/ukhalifa), yaani Wilaya!' Imam Baqir (as) anamjibu mtu ambaye huenda akadai kwamba neema iliyotajwa kwenye Aya hii ni chakula na kinywaji kwa kusema: 'Wallahi! Sio chakula wala kinywaji bali ni Wilaya (uongozi) yetu.' Haya ndiyo yaliyotajwa na al-Hafidh bin Asakir ad-Dimeshqiy as-Shafi' katika kitabu cha Tarikh Madinat ad-Dimeshq. Kuna ufafanuzi mwingine ambao umenukuliwa katika Tafsir al-Qummi ambapo Imam Ja,ffar as-Swadiq (as) ananukuliwa akifafanua maana ya neena iliyonukuliwa kwenye Aya tunayoijadili kwa kusema: 'Umma huu utaulizwa kuhusiana na neema ambayo Mwenyezi Mungu ameuneemesha kwayo kupitia Mtume wake na kisha Ahlul Bait wake (Mtume).' Al-Kulaini pia ananukuu ufafanuzi mwingine wa Imam Ja'ffar katika kitabu cha al-Kafi akisema: 'Mwenyezi Mungu ni mkarimu na mtukufu zaidi kuliko kwamba akulisheni na kukuruzukuni chakula na kisha akuulizeni juu ya chakula hicho, bali atakuulizeni juu ya kile alichokuneemesheni kupitia Muhammad na Aali za Muhammad (saw).'
***********
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, tungependa kuashiria nukta zifuatazo kutokana na yale tuliyojifunza kutokana na Aya hii na ufafanuzi uliotolewa na Maimamu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (as). Nukta ya kwanza ni uwepo mtakatifu wa neema kubwa miongoni mwa wanadamu ambao ni Mtume Muhammad (saw) pamoja na Aali zake (as). Kwa ibara nyingine ni kuwa Muhammad, Ali, Fatwimah, Hassan, Hussein na Maimamu wengine wema watukufu wanaotokana na kizazi cha Imam Hussein (as) ni Mahujja wa Mwenyezi Mungu juu ya viumbe wake na amana yake katika ardhi yake na ni neema yake kubwa zaidi kwa waja wake.
At-Tabarsi anamnukuu Imam Ali (as) katika kitabu chake cha al-Ihtijaj akisema kuhusiana na watu: 'Na aliwathibitishia kwamba aliwapa maneno ambayo yanathibitisha upweke na Umoja wake (Mwenyezi Mungu), kwamba (Mwenyezi Mungu) ana Mawalii ambao vitendo na hukumu zao zinaenda sambamba na vitendo vyake (Mwenyezi Mungu), hivyo wao ni waja wake waliotukuzwa, na ni neema ambayo watu wataulizwa juu yake… Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ametoa neema kupitia kwao, kwa wale wanaowafuata katika Mawalii zake. Hawazungumzi ila baada ya kuzungumza Yeye, nao hufanya mambo kwa amri Yake na huwaimarisha kwa Roho Yake. Muulizaji akauliza: Muhujja hao ni nani? Amir al-Mu'mineena (as) akamjibu: Wao ni Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na wale waliochukua nafasi yake katika wale aliowatakasa Mwenyezi Mungu na ambao anasema juu yao: Enyi mlioamini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi, na ambao Mwenyezi Mungu amewafungamanisha na nafsi yake mwenyewe na ya Mtume wake na kuwafaradhisha waja wawatii kama alivyowafaradhisha wamtii Yeye mwenyewe.'
Na Tabarsi ananukuu katika Tafsiri yake ya Majmau al-Bayaan fi Tafsiri Qur'an Hadithi kutoka kwa Imam Swadiq (as) kwamba alimuuliza Abu Hanifa ambaye alikuwa mwanafunzi wake: 'Neema ni nini kwako, ewe Abu Nu'man? Abu Hanifa akajibu kwa kusema: Ni chakula na maji baridi. Imam Swadiq (as) akamwambia: 'Lau kama Mwenyezi Mungu atakusimamisha mbele Yake Siku ya Kiama na kukuuliza kuhusu kila chakula ulichokula na kinywaji ulichokunywa bila shaka utachukua muda mrefu sana mbele yake! Abu Hanifa akauliza tena: Basi neema iliyokusudiwa ni ipi, nifanywe kuwa fidia kwako? Imam Swadiq (as) akamjibu kwa kusema: Sisi Ahlul Bait, ndio neema ambayo Mwenyezi Mungu aliwajaalia waja. Ni kupitia sisi ndipo wakaungana baada ya kufarikiana na ni kupitia sisi ndipo Mwenyezi Mungu akaunganisha nyoyo zao na kuwafanya kuwa ndugu baada ya kuwa maadui, na ni kupitia sisi ndipo akawaongoza kwenye Uislamu, nayo ni neema isiyokatika, na Mwenyezi Mungu atakuulizeni kuhusu haki ya neema hii ambayo alikuneemesheni kwayo, nayo ni Mtume na kizazi chake.'
Kuhusu Aya hii, Allama al-Hilli (MA) anasema kwamba neema watakayoulizwa waja Siku ya Kiama ni kuhusu Wilaya na uongozi wa Ahlul Bait wa Mtume (saw) na miongoni mwao ni Imam Hassan na Imam Hussein (as), na kwamba Wilaya hii inapaswa kuwa thabiti na ya wajibu kwao tu, bila kusirikishwa watu wengine wasiofaa kuhusiana na uongozi muhimu kama huo wa mbinguni.
Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha Juma hili ambacho kama kawaida kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikikutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena wakati na siku kama ya leo, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.