Sibtain katika Qur'ani
Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza sehemu ya 18 ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi, ambapo leo bado tutaendelea kujadili suala la neema kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewajalia waja wake humu duniani nayo ni neema ya Ahlul Bait (as), ambao ni kizazi kitoharifu cha Mtume Mtukufu (saw).
Kati ya Aya zinazozungumzia neema katika Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani ni hizi za 19 hadi 23 za Surat ar-Rahman ambapo Mwenyezi Mungu anasema: Anaziendesha bahari mbili zikutane; Baina yao kipo kizuizi, haziingiliani. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili? Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili?
Ndudu wasikilizaji, wataalamu wa lugha ya Kiarabu na wafasiri wa Qur'ani Tukufu wanasema kuwa makusudio ya bahari mbili hizi ni bahari ya maji tamu na maji ya chumvi ambazo maji yake huwa hayachanganyiki licha ya kukutana sehemu moja na kwamba yote ni maji, bali kati yazo kuna kizuizi kisichoonekana kwa macho ambacho huyazuia maji hayo ya bahari mbili za maji tamu na ya chumvi kuchanganyika. Jambo hilo huzuia kuvurugika mfumo wa uhai na maisha duniani.
Miongoni mwa manufaa ya bahari hizo mbili ni kupatikana ndani yake lulu na marijani. Hii ndio maana ya dhahiri ya Aya hizi. Je, maana yazo ya batini ni ipi? Kuna rai na maoni mengi yaliyotolewa na wanazuoni wajuzi kuhusiana na suala hili. Baadhi ya maoni hayo ni kwamba bahari mbili zilizokusudiwa katika Aya hizo ni bahari ya mbinguni na ya ardhini, baadhi wanasema ni bahari ya maji tamu na ya maji ya chumvi na wengine wanasema ni bahari ya Utume na bahari ya Ukhalifa na Uimamu. Ili tupate kufafanua zaidi suala hili, tunakuombeni tupate kupitia kwa pamoja Riwaya zifuatazo:
*********
Tunasoma katika kitabu cha Durr al-Manthur cha Hafidh as-Suyuti as-Shafi' akimnukuu Ibn Murdawaih kutoka kwa Ibn Abbas akisema kuhusu maana ya Aya hii inayosema: Anaziendesha bahari mbili zikutane; kuwa ni Ali na Fatuma, Baina yao kipo kizuizi, haziingiliani; ni Mtume (saw) na kwamba Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani; ni Hassan na Hussein…….'
At-Tabarsi ameinukuu katika tafsiri yake ya Majmaul Bayaan kupitia Salman Farsi, Said bin Jubair na Sufyan ath-Thauri na wengine kdhaa. Al-Hasakani al-Hanafi pia ameinukuu Hadithi hii katika kitabu chake cha Shawahid at-Tanzil Liqawaid at-Tafdhil kutoka kwa adh-Dhwahhak na mwanazuoni mwingine wa Kihanafi as-Shaikh Salman al-Qunduzi katika kitabu cha Yanabiul Mawadda kutoka kwa masahaba Abu Said al-Khidri, ibn Abbas na Anas bin Malik wakisema kwamba: 'Sufyan bin Uyyaina alimnukuu Imam as-Swadiq (as) akisema katika kufasiri Aya hii: Ali na Fatima ni bahari mbili ambazo moja haiingilii nyingine, Baina yao kipo kizuizi, ni Mtume (saw) na Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani ni Hassan na Hussein (as).'
Al-Kharkushi anaandika katika vitabu vyake viwili vya al-Lu'lu' na Sharaf al-Mustafa akiwanukuu Salman al-Farisi, Abu Bakr as-Shirazi katika kitabu chake akiwanukuu Abu Swaleh, ath-Tha'labi, Ali bin Ahmad atw-Twaai na Abu Muhammad bin al-Hassan al-Qatwani katika Tafsiri zao wakimnukuu Said bin Jubair na Sufyan ath-Thauri na kadhalika Abu Naim al-Isfahani katika kitabu chake cha Nuzul Qur'an kutoka kwa Hamid bin Salma, kutoka kwa Thabit kutoka kwa Anas bin Malik, kutoka kwa Abu Malik kutoka kwa Ibn Abbas naye al-Qadhi an-Natanzi amemukuu Sufyan bin Uyyaina akimnukuu Ja'ffar bin as-Swadiq (as) akizungumzia Hadithi hii ambayo imenukuliwa pia na Abu Muawiyya adh-Dhurair kutoka kwa al-A'mash kutoka kwa Abu Swaleh kutoka kwa Ibn Abbas… kuwa lulu hapa ni Hassan na marijani ni Hussein kwa sababu lulu ni kubwa nayo marijani ni ndogo. Amesema: 'Si jambo la kushangaza kuona Ali na Fatwimah wakifananishwa na bahari mbili kutokana na fadhila, utukufu na wingi wa heri zao kwa sababu bahari imeitwa bahari kutokana na upana wake (utoaji wake wa heri nyingi).'
***********
Baada ya haya yote wapenzi wasikilizaji, tunapenda kaushiria maoni na kauli za maulama na wanazuoni wengine wa Kiislamu kuhusu fadhila na utukufu wa Ahlul Bait wa Mtume (as) akiwemo Hassan na Hussein (as). Watukufu hawa wana fadhila nyingi sana kiasi kwamba al-Hafidh al-Hasakani ambaye ni mwanazuoni wa madhehebu ya Hanafi anatolea hoja mamia ya Aya kuhusiana na fadhila za watukufu hawa na kuthibitisha kwamba ni bora kuliko viumbe wengine, kupitia kitabu chake cha Shawahid at-Tanzil Liqawaid at-Tafdhil. Anamnukuu Ibn Abbas akisema kuwa bahari mbili kwenye Aya tunayoijadili ni: Ali na Fatwimah (as) na kizuizi kati yazo ni mapenzi na mahaba ya kudumu milele na ambayo hayana mwisho juu ya wapendwa hawa. Ama lulu na marijani ni Hassanain yaani Imam Hassan na Imam Hussein (as).
Ibn Abbas alikuwa karibu mno na mazingira ya tafsiri ya Qur'ani kati ya masahaba na aliyekuwa karibu zaidi yake ni Abu Said al-Khidri, ambaye aliishi na Mtume (saw) na kupokea Hadithi nyingi kutoka kwake. Ibn Maghazili as-Shafi' amemnukuu katika kitabu chake cha Manaqib Ali bin Abi Talib akisema kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema, Anaziendesha bahari mbili zikutane kuwa: Ni Ali na Fatwimah, Baina yao kipo kizuizi, haziingiliani; ni Muhammad (saw) na Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani ni Hassan na Hussein.
Sayyid Hashim al-Bahrani (MA) ameorodhesha katika kitabu chake cha Ghayat al-Maram Hadithi saba kutoka vitabu vya Kisuni na Hadithi tano katika vitabu vya Kishia ambazo zote zinaashiria na kusisitiza maana tuliyotangulia kuitaja kuhusiana na lulu na marijani na vilevile bahari na kizuizi zilizotajwa katika Aya hizo.
Allama al-Hilli anazungumzia suala hilo katika kitabu chake cha Minhajul Karama kwa kusema jambo na fadhila hizo hazikuhusishwa na mtu mwingine yoyote isiyekuwa Imam na kuwa hiyo ni moja ya dalili zinazothibitisha Uimamu.
Al-Qunduzi pia analizungumzia suala hilo katika kitabu chake cha Yanabiul Mawadda akimnukuu Imam Swadiq (as) anayesema: 'Abu Dharr (MA) alikuwa akisema: Aya hizi za, Anaziendesha bahari mbili zikutane; Baina yao kipo kizuizi, haziingiliani. Basi ni ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha nyinyi wawili? Katika hizo bahari mbili zinatoka lulu na marijani, zilitemka kuhusiana na Mtume (saw), Ali, Fatwimah Hassan na Hussein (as). Basi hawapendi isipokuwa Mu'mini na hawachukii isipokuwa kafiri. Hivyo, kuweni waumini kwa kuwapenda na wala msiwe makafiri kwa kuwachukia msije mkutupwa Motoni.'
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji, ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana nanyi tena juma lijalo wakati na siku kama ya leo, tunakutakieni nyote wakati mwema, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.