Jul 14, 2022 09:36 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tunatumai hamjambo kabisa na mko tayari kujinga nasi tena kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi, karibuni.

Mwenyezi Mungu Mtukufu alipenda kuwepo viumbe bora, wakamilifu, wema na waliotukuka zaidi ulimwenguni, ambao wanatokana na nuru yake mwenyewe na kuwepo uzingatiaji na msaada wake maalumu kwao. Riwaya za Kiislamu zinatubainishia wazi kwamba watukufu hao hawakuwa wengine bali ni Muhammad na kizazi chake kitoharifu (as). Nuru na roho za watukufu hao ziliumbwa hata kabla ya kuumbwa Nabii Adam na hivyo kuwa katika nafasi iliyo juu na adhimu zaidi kuliko ya Adam, ambapo utukufu wao ndiyo iliyokuwa njia na wasila alioutumia Nabii Adam (as) kumuumba toba Mwenyezi Mungu alipomuasi kwa kuacha kufanya jambo bora zaidi alilotakiwa kulifanya kwa maslahi yake mwenyewe. Kwa kutumia majina ya watukufu hao kutubu na kuomba msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, Nabii Adam (as) alifaulu na kupata fahari ya watukufu hao kuwa katika kizazi chake.

Khawarazmi al-Hanafi anaandika katika vitabu vyake vya Maqtal al-Hussein (as) na al-Manaqib, Ibn Hajar al-Asqalani as-Shafi' katika Lisan al-Mizan, Sheikh al-Qunduzi al-Hanafi katika Yanabiul Mawadda na wengineo kama vile Nabati al-Bayadhi katika as-Swiraat al-Mustaqeem ila Mustahiq at-Taqdeem kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: "Mwenyezi Mungu alipowaumba Adam na Hawaa (as), walitembea peponi huku wakiwa wanajigamba. Adam (as) akamwambia Hawaa: Mwenyezi Mungu hakuumba kiumbe mwingine yeyote bora kutuliko sisi.  Mwenyezi Mungu akamwambia Malaika Jibril: Wapeleke waja wawili wangu hawa mbele ya yule Bibi ambaye yuko kwenye pepo ya juu zaidi, Firdousi. Adam (as) na Hawaa walipoingia kwenye pepo walimwona huko binti ambaye alikuwa amevishwa kichwani taji la nuru na kwenye masikio yake pia herein zeye nuru, ambapo pepo ilikuwa iking'ara kutokana na uzuri wa sura yake. Adam akasema: Ewe mpendwa wangu Jibril: Ni nani huyu binti ambaye pepo inang'ara kutokana na uzuri wa sura yake? Jibril akajibu: Huyu binti ni Fatwimah binti wa Muhammad (saw) ambaye ni katika watoto wake na ambaye atadhihiri mwishoni mwa zama (atakuwa ndiye Mtume wa mwisho). Adam (as) akauliza:  Je, taji hili lililo kichwani kwake ni nini? Jibril akajibu: Ni mume wake Ali bin Abi Talib (as). Adam (as) Akauliza: Je, hereni mbili hizi zilizoko kwenye masikio yake ni nini? Jibril (as) akajibu: Ni watoto wake wawili Hassan na Husssein (as).

Adam (as) akauliza: Ewe mpendwa wangu Jibril! Je, waliumbwa kabla yangu mimi? Jibril akasema: Waliumbwa na kuwa katika maficho (siri) ya elimu ya Mwenyezi Mungu, miaka elfu nne kabla ya kuumbwa wewe."

**********

Hatimaye Adam (as) akawa amepewa mtihani mkubwa na mgumu ambapo alikosea na kutakiwa atubu. Hapo akawa anahitajia dhamana ya kukubaliwa toba hiyo ili aweze kupata radhi za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hapo viumbe hao watukufu na watakatifu wakawa ndio njia pekee ya kuwezesha kukubaliwa toba yake kwa Mwenyezi Mungu. Hivi ndivyo vinavyonukuu vyanzo vya Kiislamu vikiwemo vitabu vya Faraid as-Simtain cha al-Juwaini as-Shafi', Ar'jah al-Matwalib cha Amir Tasri al-Hanafi na Ghayatul Maraam cha Sayyid Hashim al-Bahrani wote wakimnukuu Abu Huraira kwamba Mtume (saw) alisema: 'Mwenyezi Mungu Mtukufu alipomuumba baba wa wanadamu (Nabii Adam as), na kupuliza ndani yake roho yake, alitazama (Adam) upande wa kulia wa Arshi na hapo akaona pepo tano za nuru zikiwa zimesujudu na kurukuu! Adam akasema: Ewe Mola! Je, uliwahi kuumba yeyote kabla yangu kutokana na udongo? Akasema, hapana ewe Adam….. Akasema, basi ni nani hawa watano ambao ninawaona wakiwa katika umbo na sura yangu? Akasema: Hawa watano ni katika kizazi chako. Kama wasingekuwa wao, nisingeumba pepo wala moto, Arshi wala Kiti cha Enzi, mbingu wala ardhi Malaika wala mwanadamu wala jini…. Mimi ni Mahmoud na huyu hapa ni Muhammad, Mimi ni Aali (wa juu zaidi) na huyu hapa ni Ali, mimi ni Fatwir (Muumba) na huyu hapa ni Fatwimah, Mimi ni Ihsan na huyu hapa ni Hassan na mimi ni Muhsin na huyu hapa ni Hussein…..Ninaapa kwa utukufu wangu! Mtu yeyote atakayenijia hali ya kuwa ana chembe ndogo kabisa ya chuki mithili ya hardali, dhidi ya mmoja wao, nitamtupa kwenye moto bila kujali (bila kusita)…. Ewe Adam! Hawa ni wateule wangu; nitaokoa na kuhilikisha watu kupitia kwao. Hivyo ikiwa utakuwa na haja na mimi basi tawasali nao (omba haja hiyo kupitia kwao).

Mtume (saw) anasema, kama anavyosema Abu Huraira na kunukuliwa na Mashafi', Mahanafi na Mashia: "Sisi ni safina ya wokovu, kila anayeshikamana nayo huokoka na anayeipuuza huangamia. Hivyo kila aliye na haja kwa Mwenyezi Mungu na aiombe kupitia kwetu Ahlul Bait."

Na mtu wa kwanza kuomba haja yake kupitia watukufu hao hakuwa mwingine bali ni baba wa wanadamu, Adam (as) ambapo wafasiri wote wa Ahlu Suna na Mashia wanasema wao ndio wanaokusudiwa katika Aya ya 37 ya Surat al-Baqarah inayosema: Kisha Adam akapokea maneno kutoka kwa Mola wake, na Mola wake akamkubalia toba yake.

Abdallah bin Abbas amepokelewa akisema kuwa Mtume Mtukufu (saw) aliulizwa kuhusiana na maneno hayo aliyoyapokea Adam (as) kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kuyatumia katika kuomba toba, naye (saw) akajibu kwa kusema: "Aliomba kwa Baraka za Muhammad, Ali, Fatwimah, al-Hassan na al-Hussein naye akawa amekubaliwa toba yake."

*********

Na katika Riwaya zilizopokelewa na Mashia, wapenzi wasikilizaji, ni ile iliyonukuliwa na Sheikh Swadouq katika kitabu chake cha Fadhail as-Shia, al-Istirabadi katika Ta'weel al-Ayaat ad-Dhwahira, Sayyid Hashim al-Bahrani katika al-Lawamiu an-Nuraniyya, al-Majlisi katika Bihar al-Anwaar na wengine wengi wakimnukuu Swahaba Said al-Khidri akisema: "Tulikuwa tumeketi na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alipofika hapo mtu mmoja na kuuliza: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nifafanulie kauli ya Mwenyezi Mungu inayomuhutubu Iblisi kwa kusema: Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli? Je, ni nani hawa ambao waku juu ya Malaika, ewe Mtume? Mtume (saw) akajibu: Ni mimi, Ali, Fatwima, Hassan na Hussein. Tulikuwa eneo la Arshi tukimsabihi Mwenyezi Mungu nao Malaika wakisabihi pamoja na sisi, miaka elfu mbili kabla ya Mwenyezi Mungu kumuumba Adam….Alipomuumba Adam aliwaamuru Malaika wamsujudie nao hawakuamrishwa kumsujusia ila kwa ajili yetu sisi. Malaika wote wakasujudu isipokuwa Ibilisi ambaye alikataa kusujudu! Mwenyezi Mungu akamwambia: Je! Umejiona mkubwa, au umekuwa katika wakuu kweli? Yaani katika hawa ambao majina yao yameandikwa pembeni ya Arshi?

Tunasisitiza kwa mara nyingine hapa wapenzi wasikilizaji kwamba, suala muhimu hapa ni wilaya na uongozi wa Muhammad na Aali zake watoharifu (as). Kwa kitendo hicho Mwenyezi Mungu alitaka kuonyesha umuhimu wa kutiiwa na kufautwa viongozi ambao ni bora katika viumbe, watukufu, watakatifu, na wanaopendwa zaidi na Mwenyzi Mungu kati ya viumbe wake, na ambao kufuata uongozi wao huwafanya wanadamu kuweza kufikia rehema, wokovu na saada ya kudumu milele.

Kuhusiana na hilo, Imam Baqir (as) anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu aliumba nuru kumi na nne kutokana na utukufu wa nuru yake kabla ya kumuumba Adam….. nuru ambazo ni roho zetu….. Muhammad, Ali, Fatwimah, al-Hassan na al-Hussein na wengine tisa katika kizazi cha al-Hussein…" Kisha Imam (as) akawahesabu kwa majina yao na kusema: 'Wallahi! Sisi ndio Mawasii na Makhalifa baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), sisi ndio 'Mathani' (Aya zinazosomwa mara kwa mara) ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Mtume wetu, sisi ndio mti wa Utume na maoteo ya rehema………Sisi Wallahi! Ndio yale maneno aliyoyapokea Adam kutoka kwa Mola wake Naye akawa amemkubalia toba yake.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunamefikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa leo. Basi hadi wakati mwingine tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.