Aug 04, 2022 06:46 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni kusikiliza sehemu ya 41 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani Tukufu na Hadithi ambavyo huzungumzia na kufafanua sifa na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) ambao si wengine bali ni Imamain al-Hassan na al-Hussein (as) na ambao wana heshima na nafasi kubwa tukufu katika Uislamu. Ni matumaini yetu kuwa mtakuwa pamoja n

 

Ndugu wapendwa, Mtume Mtukufu (swala na salamu zimshukie yeye na aali zake), mara nyingi aliwaarifisha jamaa zake, (amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yao), mbele ya Waislamu, ikiwa ni katika kufuata maagizo na amri ya Mwenyezi Mungu, subhanahu wa taala. Alikuwa akiwalingania Waislamu kuwafuata Maimamu wa uwongofu (as), ili wapate kuwachukua kwa mikono yao wenyewe hadi kwenye pwani ya wokovu, na kuwapeleka kwenye pepo ya furaha, saada na usalama, iliyojaa mapenzi na radhi za Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, na hivyo kupata humo raha na neema ya milele. Na Pepo, enyi ndugu wema, ina wenyewe, ambao kwa ajili yao iliumbwa, nao ndio wenyeji wake, na kwa baraka, wema na ulezi wao, waumini hupata heshima na fursa ya kuingia na kuishi humo milele.

Je, unadhani ni nani hao watakaokuwa wa kwanza kuingia Peponi?

Al-Hafidh Ibn Asakir ad-Dimashqi al-Shafi' ananunukuu katika kitabu chake cha Taarikh Madinat ad-Dimashq Hadithi kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliwaambia maswahaba zake: ''Enyi watu, je, mnataka nikwambieni watu walio na babu na bibi (nyanya) bora zaidi, .. Je, nikwambieni mtu aliye na baba na mama bora zaidi? Watu hao ni Hassan na Hussain''.. Hadi aliposema: ''Babu yao yuko Peponi, baba yao yuko Peponi, mama yao yuko Peponi..wote wawili wapo Peponi, na anayewapenda yuko Peponi"

Ewe Mola! tujaalie tuwe miongoni mwa wanaowapenda, na wanaowapenda babu yao na wazazi wao. Eeh Mola! Tujaalie tuishi na kufa kwenye hilo.

Naye al-Hafidh al-Khatib al-Baghdadi, as-Shafi’, ameandika katika kitabu chake mashuhuri cha Taarikh Baghdad kwamba Ibn Abbas alisema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: “Ule usiku nilipopaishwa mbinguni, niliona kwenye lango la Pepo kumeandikwa: “Hapana mungu anayestahiki kuabudiwa ila Mungu, Muhammad ni Mtume wake, Ali ni kipenzi cha Mungu (yaani anapendwa na Mwenyezi Mungu), Hassan na Hussein ni wateule wa Mungu, Fatimah ni mbora wa Mwenyezi Mungu. Laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya wale wanaowachukia."

Na katika Hadithi nyingine inayokaribiana na hiyo al-Khawarazmi, ambaye ni wa madhehebu ya Hanafi, aanamnukuu Imam Ali (as) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: "Nilipopaishwa kwenda mbinguni, niliona kwenye mlango wa Pepo pameandikwa kwa dhahabu: Hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, Muhammad ni kipenzi cha Mungu, Ali ni walii wa Mungu, Fatimah, mja wa Mungu na Hassan na Hussein ni wateule wa Mwenyezi Mungu. Mungu awalaani wale wanaowachukia." Amina.

Hivyo watukufu hao wapendwa na wateule (as) ndio wenye Pepo bali wao ndio Pepo yenyewe, ambao Pepo imeumbwa kwa ajili yao, na ambao ndio wabora na wa kwanza kuingia humo. Hivi ndivyo anavyoandika al-Khawarazmi katika kitabu cha Maqtal al-Hussein (as) ambapo anasema kuwa Mtume Mtukufu (saw) alimwambia wasii wake Imam Ali al-Mrtadha: "Ewe Ali! Wa kwanza kuingia Peponi ni wanne: Mimi na wewe, al-Hassan na al-Hussein…."

Nam ndugu wapenzi, je, kuna yeyote anayedhani kwamba kuna mwanaume anayeweza kuwatagulia watukufu hawa katika kuingia Peponi? Ama kumuhusu Bibi Fatwimah az-Zahra (as), yeye bila shaka ni binti na sehemu ya mwili wa baba yake mteule, hivyo ni lazima awe pamoja naye na pamoja nao, (as).

Hivi ndivyo anavyosimulia al-Khawarazmi kutoka kwa Abu Said al-Khudri, ambapo anasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alisema: “Katika ule usiku niliopaishwa mbinguni sikupitia kitu chochote katika ufalme wa mbinguni, wala kilichoko kwenye ufalme wa pazia juu yake, ila nilikuta kimejaa utukufu wa Malaika wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, wakaniambia: Hongera kwako, ewe Muhammad! Umepewa kile ambacho hakuna yeyote kabla yako alipewa, na wala hatapewa yeyote atakayekuja baada yako: Umepewa Ali bin Abi Talib kuwa ndugu yako, Fatwimah ambaye ni mke wake kuwa binti, Hassan na Hussein watoto wako, na wapenzi wao ni Mashia. Ewe Muhammad! Hakika wewe ni mbora wa Mitume, naye Ali ni mbora wa mawasii, na Fatimah ni kiongozi (mbora) wa wanawake wa ulimwengu wote, na Hassan na Hussein ni watukufu zaidi kati ya watoto wa Mitume walioingia Peponi, na wafuasi wao ndio bora zaidi kati ya wale waliopata dhamana ya kukingwa na mafadhaiko ya Kiyama."

********

Nam ndugu wapenzi, hiyo ndiyo nafasi ya Ahlul-Bayt wa Mtume Mtukufu (saw), kwani wao ndio wateule kutokana na ukweli kuwa ndio wabora, na wao ndio walio mbele zaidi, kutokana na kuwa wao ndio walio mstari wa mbele zaidi katika tabia na heshima.. Al-Tabari Abu Jaafar Muhammad bin Abi al-Qassim anasimulia katika kitabu chake cha Bisharat al-Mustafa Lishiat al-Murtadha kwa upokezi wa Asim bin Damrah kwamba Imam Ali (as) alisema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) aliniambia kuwa mtu wa kwanza kuingia Peponi ni mimi, wewe, Fatwimah na Hassan na Hussein.” Nikasema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Na je, wale wanaotupenda (wafuasi wetu)? Akasema (saw): Watakuwa nyuma yenu."

Eeh Mwenyezi Mungu! Tujaalie daima tuwe miongoni mwa wapenzi na wafuasi wao. Tuarifishe ubora wa mambo yao, kwani wao ndio mabwana wa viumbe na uwepo, na katika Pepo wao ndio mabwana mbele ya utukufu wa Mola Muabudiwa…. Anas bin Malik ananukuliwa katika Hadithi akisema Mtume Mtukufu (saw) alisema: "Sisi wana wa Abdul Muttalib ndio mabwana wa Peponi: Mimi na Ali, Hamza na Jaffar, Hassan na Hussein, na Al-Mahdi)."

Hassan na Hussein si tu wako Peponi, bali ni miongoni mwa mabwana wa watu wa Peponi, na ni sababu mbili za kuingia Peponi. Wao wana fadhila za hali ya juu kutoka kwa Muumba wa Pepo, na kama walivyokuwa hapa duniani, ndivyo hivyo watakuwa Peponi.

Na hiyo ndugu wapendwa, ni moja ya dalili za Uimamu, kwani ni nafasi ambayo Mwenyezi Mungu mwenyewe aliwaainishia Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) miongoni mwao wakiwemo al-Hasaan na al-Husssein na akawafadhilisha kwayo juu ya viumbe wake wote. Kwa kuzingatia hilo, Mwenyezi Mungu alimuamuru Mtume wake alitangaze hilo kuwa hoja kwa waja wake.

Katika kitabu cha al-Tarf, Sayyid Ibn Tawoos, ananukuu Hadithi kutoka kwa Imam al-Kadhim, kutoka kwa baba yake as-Swadiq (as) kwamba Mtume (saw) alimwambia binti yake Fatwimah, akimtuliza kabla ya kifo chake alipokuwa kwenye kitanda cha mauti: "Ewe Fatwimah! Naapa kwa jina la aliyenituma kwa haki kuwa Nabii! Hakika Pepo imeharamishiwa viumbe wote hadi niingie mimi na bila shaka wewe utakuwa wa kwanza kati ya viumbe wa Mwenyezi Mungu kuiingia baada yangu… Hongera eeh Fatwimah! Naapa kwa jina la aliyenituma kwa haki! Bila shaka wewe ni kiongozi wa wanawake watakaoingia humo…. Naapa kwa jina la aliyenituma kwa haki! Bila shaka Hassan na Hussein wataingia humo. Utaandamana nao huku Hassan akiwa upande wako wa kulia naye Hussein upande wako wa kushoto, hadi mtakapofika katika sehemu ya juu kabisa kwenye Pepo mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Sehemu yenye utukufu mkubwa kabisa na kukaa pembeni ya Ali bin Abi Talib.."

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji hatuba budi kukuageni kutoka studio zetu za hapa mjini Tehran, tukitumai kuwa mtajiunga nasi tena juma lijalo kusikiliza kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi. Hivyo basi kutoka Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hatuna la ziada ila kukutakieni kila la heri maishani, Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.