Aug 04, 2022 07:20 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tuna furaha kujiunga nanyi tena kusikiliza yale tuliyokuandalieni katika sehemu hii ya 49 katika mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani na Hadithi, ambavyo kama mnavyojua huchambua na kuzungumzia sifa na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu ambao ni Imamain al-Hassan na al-Hussein (as).

Huenda habari muhimu na kubwa zaidi ambayo imepokelewa kuhusu kuuawa shahidi kwa Maimamu wetu watukufu wanaotokana na Mtume (saw), ni ile inayohusiana na kuuawa shahidi kwa Imam Hussein Abu Abdillah, Bwana wa Mashahidi (as). Pengine hii ni kutokana na ukweli kwamba kuuawa kwake shahidi kulitimia katika mazingira ya kinyama na ya kutisha zaidi kuwahi kuripotiwa katika historia ya mwanadamu na bila shaka tukio kama hilo halitashuhudiwa tena hadi mwisho wa dunia. Ni tasnifu ya kipekee ambayo Mwenyezi Mungu aliipa uzingatiaji wa kipekee, naye Mtume wake (saw), akaizungumzia na kuifafanua kwa urefu na mapana katika kipindi chote cha maisha yake. Katika tukio la Taff katika Siku ya Ashura, umma ulikumbwa na mtihani mkubwa ambao ulikuwa na taathira kubwa ambazo zitaendelea kubakia katika historia ya mwanadamu hadi mwisho wa dunia. Katika tukio hilo la kusikitisha, aliuawa ndani yake walii wa Mwenyezi Mungu na Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) wakateswa, kudhalilishwa na kuchukuliwa mateka. Pamoja na hayo lakini kulikuwa na watu wachache shupavu ambao licha ya uchache wao lakini walijitokeza na kusimama imara katika kutetea Uislamu na Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) hadi dakika ya mwisho ya maisha yao.

Haya, ndugu wapenzi, ni kwa mujibu wa wahyi uliomteremkia Mtume (saw) ukimtaka abashiri na kuwaonya watu ili hoja ya Mwenyezi Mungu ipate kuwathibitikia kikamilifu na kwa kina. Malaika Jibril (as) aliteremka kutoka mbinguni na kumwambia Mtume (saw): "Kwa hakika mjukuu wako huyo, hapo akawa anamuashiria Hussein, akiwa ameandamana na watu wengine kutoka kizazi, watu wa nyumba na wabora wa umma wako, atauawa katika ukingo wa Mto Furati, katika ardhi inayoitwa Karbala... Kisha Mwenyezi Mungu atawatuma watu kutoka kaumu yako.... ambao watazika miili yao, na kuweka kwenye kaburi hilo la Bwana wa Mashahidi alama ambazo zitawaongoza wanaotafuta haki na kuwa sababu ya kuongoka wenye imani…."

Kuna riwaya nyingi mno ambazo zimepokelewa kuhusiana na suala hilo kutoka kwa Mama wa Waumini Ummu Salamah, Ibn Abbas, Imam Ali (as), Anas bin al-Harith, Maadh bin Jabal, Aisha, Zainab bint Jahsh, Ummu al-Fadhl bint al-Harith, Anas bin Malik, Abu al-Tufail na al-Miswar bin Mukhrima, Asma binti Umays na Khalid bin Arfata na wengineo wengi. Ni riwaya chungu nzima, ambazo zimenukuliwa kwenye makumi ya kurasa, zikieleza juu ya habari za Jibril na Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kwamba Hussein angeliuawa huko Karbala. Miongoni mwa riwaya hizo ni ile iliyonukuliwa na Bibi Aisha akisema: "Siku moja Hussein aliingia kwa Mtume Mtukufu (saw) hali ya kuwa anateremshiwa wahyi. Akamrukia Mtume (saw) mabegani hapo Jibril akamuuliza (Mtume): Je, unampenda, ewe Muhammad? Akasema: Ewe Jibril! Ni vipi nitakosa kumpenda mwanangu? Akasema: Hakika umma wako utamuua baada yako. Basi Jibril akanyoosha mkono wake na kumletea udongo mweupe, na akasema: Katika ardhi hii atauawa mwanao - Ewe Muhammad - na jina lake (la ardhi hiyo) ni al-Taff!"

************

Naam ndugu wasikilizaji, ni kutokana na wingi wa habari zilizopokelewa kuhusiana na kuuawa mjukuu wa Mtume (as) al-Imam Hussein (as) ndipo wanahadithi na wanahistoria wakaamua kukusanya na kuandika hadithi hizo kwenye sura na milango maalumu kwenye vitabu vyao.  Kwa mfano mwanachuoni wa Kihanafi Abu al-Muayyad al-Khawarazmi ameandika na kukusanya hadithi hizo kwenye fusulu maalumu katika katika kitabu chake cha Maqtal al-Hussein (as), na vilevile katika sherhe ya kitabu cha Ihqaaq al-Haq kilichoandikwa na Sayyid Shihab ad-Din al-Mar'ashi. Kwenye kitabu hicho kuna fusulu kubwa ambayo imenukuu makumi ya marejeo na vyanzo kutoka katika vitabu vya Masuni kuhusu suala hilo. Kama alivyofanya mwanachuoni al-Amini, mwandishi wa kitabu cha al-Ghadir, ambapo ameandika kitabu maalumu katika uwanja huo na kulizungumzia jambo hilo chini ya anwani mbili ambapo ya kwanza ni:  'Siira na Sunnah zetu, na ya pili ni: Maombolezo ya Imam Hussein (as) kutoka kwa vyanzo vya Sunni, ambapo amekusanya humo makumi ya maombolezo yaliyofanywa (as) katika nyumba za wake zake au miongoni mwa maswahaba zake Mtume, na kuelezea humo kwa muhtasari na kwa marefu na mapana kuhusu kuuawa kwa mwanawe al-Hussein bin Ali (as). Hadithi hizo zote wapenzi wasikilizaji, ambazo alizizungumzia Mtume (saw) katika nyakati na maeneo tofauti, zote zinasimulia kuhusu kuuawa shahidi mjukuu wake al-Hussein (as), kudhulumiwa, mateso na kukandamizwa kwake ambapo alimuomba Mwenyezi Mungu amsaidie na kumnusuru kutokana na hali hiyo ya kusikitisha. Ibn al-Atheer ananukuu katika kitabu cha Usud al-Ghaba al-Asqalani al-Shafi'i katika al-Iswaba al-Muttaqi al-Hindi katika Kanz al-Ummal, al-Muhibb al-Tabari katika Dhakhair al-Uqba, na wengine wengi, Hadithi inayosema kwamba Mtume (saw) aliwaambia masahaba zake:  "Hakika mwanangu huyu atauawa katika ardhi ya Iraq, basi yeyote atakayekutana naye na amnusuru."

Al-Khwarazmi al-Hanafi amesimulia katika kitabu chake cha Maqtal al-Hussein na Ibn A'tham Al-Kufi katika al-Futuh kwamba Mtume (saw), siku moja alirejea nyumbani kutoka katika safari ambayo alikuwa amefaifanya. Alionekana kuwa ni mwenye huzuni ambapo alipanda mimbara na kuwahutubia watu huku akiwa ameyabeba maua yake mawili al-Hassan na al-Hussein. Aliinua kichwa chake mbinguni na kusema. "Ewe Mola wangu! Mimi ni Muhammad, mja na Nabii wako na hawa ndio walio bora katika familia yangu, wateule wa kizazi changu na wema wangu. Ni watu ambao watanirithi katika Ummah wangu. Ewe Mwenyezi Mungu! Jibril amenipasha habari kwamba mwanangu - huku akiwa anamuashiria Hussein – atauawa kwa madhila. Allahumma! Mbariki kwenye mauaji hayo na umfanye awe miongoni mwa Mabwana wa Mashahidi….." Hapo maswahaba wakalia na Mtume (saw) akawaambia: "Je, mnalia na hammunusuru?! Ewe Mwenyezi Mungu! Wewe Mwenyewe kuwa walii na msaidizi wake."

**********

Mtume Mtukufu (saw) alisema kwa mujibu wa Hadithi iliyopokelewa na Ummu Salamah: "Hussein atauawa baada ya kutimia miaka sitini baada ya Hijra." Hii haina maana kuwa watu walikuwa wamesahau yale waliyoambiwa na Mtume (saw). Al-Khawarazmi anamnukuu Ibn Abbas akisema: "Sisi sote Ahlul Bayt hatukuwa na shaka kwamba al-Hussein bin Ali angeuawa huko Taff!

Kadhalika watu hawakusahau kwamba Mtume alionya na kutahadharisha dhidi ya kumuacha Husein auawe na watu waovu. Huyu hapa Ibn Abbas anasimulia kwamba Mtume Mtukufu (saw) siku moja alisema: "Nina kazi gani na Yazid (ananihusu nini)! Mungu asimbariki Yazid! Hakika atamuua mwanangu na mtoto wa binti yangu, al-Hussein bin Ali." Kisha akasema Mtume: "Naapa kwa jina la yule ambaye nafsi (roho) yangu iko mikononi Mwake, mwanangu asiuawe ila miongoni mwa kaumu ambayo haitamnusuru (kumtetea) na Mwenyezi Mungu aweke hitilafu kwenye nyoyo na ndimi zao." Kisha Ibn Abbas akalia.

Na Waislamu wakalia kwa uchungu baada ya kuuawa shahidi Abi Abdillah al-ussein, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake. Wakamlilia mjukuu wa Mtume al-Hussein, jinsi alivyouawa kinyama! Na wakajililia wenyewe, jinsi walivyomwacha auawe na kutojiunga naye, jinsi walivyomdhalilisha na kutomnusuru na jinsi walivyomwacha peke yake hadi alipozingirwa na maadui ambao walimuua kikatili bila huruma!

Hakika waliofaulu ni wale tu walioitikia wito wa Mtukufu Mtume (saw) ambao aliwaomba wamnusuru mwanawe nao wakawa wameitikia wito huo. Wakawa wamejitolea nafsi zao kupigana bega kwa bega pembeni ya mtukufu huyo hadi walipouawa shahidi kwenye njia hiyo. Waliokuwa katika mstari wa mbele katika jihadi hiyo tukufu ni Abul Fadhl Abbas bin Ali, mashuhuri kwa lakabu ya Qamar Bani Hashim, Ali Akbar ambaye alifanana sana kiumbo na Mtume al-Mustafa (saw), Qassim bin Hassan al-Mujtaba az-Zaki na Maanswar waaminifu wakiwemo Habib bin Madhahir, Burair bin Khudhair, Hurr ar-Riyahi, Muslim bin Aujasa, John, Abbas, Wahab, Hilaal, Junada, watoto wa Muslim bin Aqil, ndugu zake Abbas kutoka kwa mama yake Ammul Baneen na wema wengine kutoka katika ukoo wa Bani Hashim.

Mtu mmoja kwa jina la Anas bin al-Harith alisema siku moja: "Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akisema: "Huyu mwanangu – yaani Hussein – atauawa katika ardhi ya Iraki, basi atakayemkuta na amsaidie." Waandishi wa historia wameandika kwamba mtu huyo alijiunga na msafara wa Imam Abu Abdallah al-Hussein, na akapigana kwenye kundi lake hadi alipopata baraka na utukufu wa kuuawa shahidi.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran, ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi kwa juma hili. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena katika kipindi kijacho, tunakuageni nyote kwa kusema Wassalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.