Oct 04, 2022 16:40 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (52)

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu, ili tuweze kufungua ukurasa mwingine katika kurasa za historia ya Maulamaa na wanazuoni wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 52 kitamzungumzia Sayyid Muhammad Baqir Gilani Shafti, mmoja wa wasomi na wanazuoni watajika aliyeishi katika karne ya 13 Hijria ambaye anajulikana katika jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa lakabu ya Hujjatul Islam Mutlaq. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Karibu.

 

Sayyid Muhammad Baqir Gilani Shafti alizaliwa katika kijiji cha Chirza katika mkoa wa Zanjan nchini Iran. Baba yake alikuwa msomi na mwanazuoni wa kuchanganyika na watu na ni miongoni mwa wajukuu wa Imam wa saba wa Waislamu wa madhehebu ya Shia. Baada ya Muhammad Baqir Gilani Shafti kumalizika masomo ya msingi kwa baba yake, alifunga safari akiwa na umri wa miaka 16 na kuelekea Karbala Iraq kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Alibakia Karbala kwa muda wa mwaka mmoja akishiriki darsa na masomo ya walimu wakubwa na mahiri wa zama hizo kama Wahid Bahbahai na Allama Bahr al-Ulum. Kisha akaelekea katika mji wa Najaf huko huko Iraq na kusoma katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha mji huo kwa muda wa miaka 6. Alishiriki masomo ya walimu katika mji huo kama Sheikh Ja’afar Kashif al-Ghitaa na baada ya hapo akaelekea katika Chuo cha Kidini (Hawza) katika mji wa Kadhmein Iraq na huko alisoma kwa wanazuoni wengine watajika katika zama hizo kama Sayyid Muhsin A’raji. Baadaye kipindi fulani alikuwa katika miji ya Qum na Kashan Iran na kuhudhuria darsa na masomo ya Mirza Qumi na Mullah Mahdi Naraqi na hivyo kupanua wigo wa ufahamu wake kielimu na kimaarifa. Mwaka 1216 alielekea katika mji wa Isfahan.

Msomi huyu aliishi maisha ya kawaida na ya kimasikini mno. Alikuwa na shauku na hamu kubwa ya elimu ambapo alikipitisha kipindi cha ujana wake nyakati za usiku akisoma kwa bidii. Baada ya kuishi kwa miaka kadhaa katika mji wa Isafahan Iran akisoma na kufanya utafiti wa kielimu, aliamua kufunga safari na kuelekea katika jiji la Tehran. Alianza maisha yake yaliyojaa zuhdi na kuipa mgongo dunia katika Madrasa ya Choharbagh mjini Tehran. Upana wa elimu na maarifa yake ya kielimu siku baada ya siku yalikuwa yakidhihiri kwa wanafuzni waliokuwa wakishiriki darsa na masomo aliyokuwa akiyafundisha. Hatua kwa hatua kutokana na ushujaa na tabia njema aliyokuwa amejipamba nayo alianza kupata nafasi maalumu miongoni mwa watu. Kutokana na Sayyid Muhammad Baqir Gilani Shafti kubobea katika elimu ya fikihi, usuli, Qur’ani na hadithi, hatua kwa hatua mazingira ya kuwa Marjaa yakawa yamejitokeza.

 

Mwanazuoni huyo alikuwa na mapenzi na akizingatia sana mambo ya wajibu katika dini. Ibada zake zilikuwa ibra na funzo kubwa kwa wafuasi na watu wake wa karibu. Mmoja wa watu wa karibu na mwanazuoni huyu anasimulia kwa kusema:

“Wakati wa Swala, mwili wake ulikuwa ukitetemeka sana kwa hofu ya Mwenyezi Mungu. Alikuwa akifanya ibada, kunong’ona na Allah na kumtaaradhia Mola Muumba kuanzia nusu ya usiku mpaka wakati wa asubuhi. Wakati wa kusoma dua na kunong’ona na Allah alimu huyu alikuwa na hali maalumu na alikuwa akilia kwa sauti kubwa bila ya hiari yake. Mwishoni mwa umri wake, madaktari walimwambia kwamba, aache kulia kwani kufanya hivyo ni hatari mno kwa afya yake. Lakini pamoja na katazo hilo, bado machozi ya Sayyid Gilani Shafti yalikuwa yakitiririka bila ya hiari yake wakati anapokuwa katika dua na kuongea na Mwenyezi Mungu”.

 

Huba na mapenzi yake kwa Ahlul-Beiti na maktaba ya haki ya Ushia ni kitu ambacho hakikujificha kwa watu. Alimu huyu alikuwa akibadilika mno wakati anaposikia visa na simulizi za misiba na masaibu ya Ahlul-Beiti (as) kiasi kwamba, anapokuwa katika majlisi fulani ya maombolezo, msomaji wa masaibu alikuwa akisoma na kusimulia kwa mukhtasari misiba na masaibu hayo ya watu wa nyumba ya Bwana Mtume (saw).

Alipokuwa katika mji wa Isafahan aliondokea kuwa na nafasi na ushawishi mkubwa mno miongoni mwa wananchi. Uaminifu na utunzaji wa amana aliokuwa nao ni mambo ambayo yaliwafanya matajiri na wafanyabiashara wampatie mwanazoni huyo mali nyingi. Kwa upande wake Sayyid ambaye alikuwa msimamizi wa Beitul-Mal (hazina ya dola) alikuwa na tadibiri na mipango sahihi na ya hali ya juu ambapo alikuwa akitumia mali hizo kwa ajili ya wahitaji katika masuala ya kimaada na kimaanawi kwa Waislamu wa Kishia. Inaelezwa kwamba, hakuna mhitaji ambaye alikuwa akimuendea alimu huyo na kurejea mikono mitupu. Aidha mwanazuoni huyo alifungua maduka mawili moja likiwa bucha la nyama na jingine sehemu ya kuoka mikate na kuwapatia hawala wahitaji zaidi ya elfu moja ambao kwa kutumia hundi hizo walikuwa wakienda na kuchukua nyama na mikate.

Hatua kwa hatua, mwanazuoni huyo akaondokea kuwa tajiri kiasi kwamba, baadhi wanaamini kuwa, alikuwa ndiye alimu tajiri zaidi miongoni mwa wanazuoni wa Kishia. Hata hivyo inapasa kufahamu kwamba, utajiri huu haukuwa ni utajiri wake binafsi, bali ulikuwa ni amana alizokuwa akipatiwa na watu waliomuamini ili atumie kwa ajili ya masikini na wahitaji miongoni mwa Waislamu.

 

Hujatul Islam Shafti hakuwa akichoka kushughulikia masuala ya Waislamu. Historia inaonyesha kuwa, alikuwa akitumia sehemu kubwa ya muda wake kwa ajili ya kutatua matatizo ya kijamii na kiuchumi ya Waislamu na alikuja na mipango na mikakati makini katika uwanja huo. Ni kutokana na sababu hiyo, ndio maana daima Mashia walikuwa wakimrejea kwa ajili ya kutatuliwa matatizo yao ya kijamii, kiuchumi na hata kisiasa sambamba na kutoa hukumu kuhusiana na masuala mbalimbali na walikuwa wakimtambua kama ni kadhi na hakimu wa Kiislamu. Ingawa baadhi ya wakati kulikuwa na changamoto hasa kutokana na ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na utawala wa wakati huo wa Iran hususan katika mji wa Isfahan. Hata hivyo, mtawala wa wakati huo hakuwa na la kufanya dhidi ya alimu huyu na alishindwa kumzuia waziwazi kufanya harakati zake kutokana na himaya na uungaji mkono mkubwa wa wananchi aliokuwa nao bila kusahau ushujaa wake ambao haukuwa na mithili. Kwa msingi huo, Sayyid Muhammad Baqir Shafti akaitumia fursa hiyo kwa kadiri alivyoweza kutekeleza majukumu yake ya kijamii likiwemo suala la kutoa hukumu miongoni mwa watu. Alikuwa akitilia mkazo mno juu ya kutekelezwa hukumu za Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu.

Msikitii wa Sayyid katika mji wa Isfahan

 

Moja ya hatua nyingine muhimu za msomi huyu ni kujenga msikiti mkubwa katika mji wa Isafahan ambao baadaye uliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Msikiti wa Sayyid. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1240 Hijria na kutokana na usanifu mkubwa wa majengo ulitotumika kujenga msikiti huo, unahesabiwa kuwa moja ya misikiti nadra sana nchini Iran.

Siku moja Fat’h Ali Shah mtawala wa wakati huo wa Iran aliuona msikiti huo mkubwa ukiwa bado haujakamilika na kusema: Nyinyi hamna uwezo wa kukamilisha ujenzi wa msikiti huu, hivyo nishirikisheni mimi katika kukamilisha kwake. Sayyid Shafti alikataa takwa la mfalme huyo na kumjibu akimwambia: Uwezo wetu upo katika hazina ya Mwenyezi Mungu. Hatimaye msikiti huo ulikamilika, na Sayyid aliendelea kuswali ndani yake hadi mwisho wa umri wake na kutokana na mapenzi ya watu kwake, maelfu kwa maelfu ya waumini walikuwa wakishiriki ibada ya Swala katika msikiti huo. Sayyid Muhammad Baqir Gilani Shafti aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 85 na kuzikwa katika eneo la msikiti huo alilokuwa ameliainisha.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu cha leo cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu umefikia tamati, tukutane juma lijalo katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.