Akhlaqi Katika Uislamu (12)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 12 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Bila shaka mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tuliendelea kuzungumzia baadhi ya vielezi vya kiakhlaqi, ambavyo vina taathira na mchango muhimu katika maisha yetu. Na kama tulivyotangulia kueleza, katika utamaduni wa kimalezi na kiitikadi wa Uislamu wa asili uliofunzwa na Bwana Mtume SAW kuna mfungamano usiotenganishika baina ya dunia na akhera, kwa maana kwamba misimamo na mitazamo yetu yote ya kifikra na kimatendo ina taathira ya moja kwa moja kwa akhera yetu. Kuhusiana na suala hili, kuna Hadithi fupi lakini wadhiha ya Bwana Mtume SAW inayozungumzia nukta hii muhimu sana na ya msingi isemayo: "Dunia ni shamba la akhera", ikimaanisha kwamba, kama ilivyo kwa mkulima, ambaye hupata mazao na mavuno kulingana na mbegu na mimea anayopanda, kila fikra, imani, amali na tendo la mtu litakalojionyesha na kujidhihirisha katika dunia hii, taathira na matunda yake yatakuja kushuhudiwa katika ulimwengu wa baada ya kifo na kuandamana na mtu mwenyewe. Kanuni hii inajiakisi na kufanya kazi pia katika misingi na thamani za kiakhlaqi.
Na kama mpendwa msikilizaji utakuwa ungali unakumbuka, katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba moja ya thamani muhimu za kiakhlaqi, ambayo ina nafasi kuu na ya msingi katika kuimarisha mahusiano ya kijamii ni "hulka na tabia njema." Kuhusu athari za msingi huu wa kiakhlaqi katika ulimwengu mwingine wa akhera, Bwana Mtume SAW amesema: "Hakuna kitu kitakachokuwa bora na chenye uzito zaidi katika mizani ya amali za mtu Siku ya Kiyama kama tabia njema." (Usulul-Kafi)
Moja ya mambo ambayo kila mtu mwenye imani juu ya ulimwengu wa baada ya kifo analitamani zaidi, si kusalimika tu na adhabu au mateso ya aina yoyote, bali muhimu zaidi, ni kuingizwa peponi na kufaidika na neema zake zisizo na kikomo. Siri mojawapo ya kumuingiza mtu kwenye Pepo ya milele ya Mwenyezi Mungu ni kuwa tabia na akhlaqi njema. Bwana Mtume SAW, ambaye ni dhihirisho la sifa zote njema za kiakhlaqi amesema: "Mtu mwenye akhlaqi njema ataingia peponi bila ya shaka yoyote." (U'yunu Akhbari-Ridha, Juzuu ya 2, Ukurasa wa 31).
Katika Hadithi nyingine, mtukufu huyo amelizungumzia hivi suala la tabia njema: "Amali itakayowaingiza zaidi peponi watu wa umati wangu ni kumcha Mwenyezi Mungu na akhlaqi njema." (Usulul-Kafi)
Kwa hakika siri na sababu itakayowafanya watu wenye akhlaqi na tabia njema waingie peponi ni mtindo wao wa maisha ya kiakhlaqi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema maneno ya hekima kuifafanua nukta hiyo. Ayatullah Khamenei amesema: "Maisha ya tabasamu ni maisha ya peponi; na maisha yasiyo na tabasamu ni maisha ya motoni."
Sifa nyingine kubwa ya watu wa peponi ni taathira kubwa waliyonayo kwa nyoyo za watu na mvuto wao mkubwa kwa wanadamu wenzao. Kwa hakika ni sifa hiyo hiyo ya kuziathiri nyoyo, ndiyo iliyochangia sana kumfanya Bwana Mtume Muhammad SAW apendwe na watu; na ndiyo iliyoufanya Uislamu uzidi kukua na kuenea siku baada ya siku na kuvutia watu wengi zaidi makundi kwa makundi. Mwenyezi Mungu Mtukufu ameitaja kwa wema sifa hiyo ya Bwana Mtume katika aya ya 159 ya Suratu Aal Imran aliposema: "Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia."
Kwa hivyo kama tunataka tuishi maisha ya peponi, na kesho Kiyama tukaingizwe kwenye Pepo ya Allah na sisi pia kuweza kuziathiri nyoyo za watu kama alivyokuwa Bwana Mtume SAW, inatupasa tujipambe kwa sifa ya tabia na akhlaqi njema.
Ni jambo la kujiuliza mpendwa msikilizaji, kwamba inawezekanaje Muislamu wa kweli, ambaye kila siku anaposali na kusoma dhikri na nyuradi huwa anamtaja Mola wake kwa sifa zake mbili tukufu za Rahman na Rahim zinazobainisha rehma, huruma na urehemevu wa Allah usio na kikomo wala kifani, kisha Muislamu huyo akawa na roho isiyo na huruma na khulka na vitendo vya ukatili? Ilhali Bwana Mtume SAW amesema: "Wapendeni wanadamu wote ili na nyinyi Mwenyezi Mungu akupendeni." (Kanzul-U'mmal)
Nukta nyingine muhimu sana, ambayo inausiwa na kutiliwa mkazo katika utamaduni wa kiakhlaqi wa Uislamu, ni kuwataka Waislamu wawe na huruma na urehemevu kwa wanadamu wote na wao wenyewe kuishi maisha ya kuhurumiana. Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye Mwenyezi Mungu Mtukufu amemtaja kuwa ni rehma kwa walimwengu anasema: "Naapa kwa Mwenyezi Mungu ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, hawataingia peponi isipokuwa watu wenye huruma." Waliposikia hayo, kundi moja la masahaba wakasema: Lakini sisi tunahurumiana. Bwana Mtume akawaambia: "Hamuwezi kuambiwa kuwa mna sifa ya huruma, mpaka muwapende na kuwaonea huruma watu wote." (Kanzul-U'mmal)
Chemchemi ya mtazamo huu wa upendo kwa watu, ambao hauna mpaka na wala hauzingatii chengine chochote isipokuwa utu na ubinadamu wao, ni Qur'ani tukufu ambayo inasema katika aya ya 75 ya Suratun-Nisaa ya kwamba: "Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako".
Wakati Muislamu anapojengeka na kuondokea kuwa na mtazamo huu wa kupambika na tabia na akhlaqi njema kwa kupanda mbegu ya upendo, huruma na urafiki ndani ya nyoyo za watu na akawa anawapenda na kuwahurumia wanadamu wote, hataweza katu kupuuza shida, machungu na mateso wayapatayo binadamu wenzake; na hatohisi au kujiona kuwa hana masuulia wala jukumu lolote la kushirikiana nao katika masaibu yawafikayo. Tuombeni dua ifike siku ambayo tutakuja kushuhudia dunia iliyojaa na kutawaliwa na upendo na kuhurumiana baina ya wanadamu wote. Na kwa dua hiyo mpendwa msikilizaji, niseme pia kwamba, sehemu ya 12 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 13 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/