Nov 06, 2022 14:58 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (17)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 17 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Kwa kila msikilizaji wetu anayefuatilia kwa karibu kipindi hiki bila shaka angali anakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tulibainisha kwa kiwango fulani misingi mikuu ya akhlaqi za Kiislamu na tofauti za msingi zilizopo kati yake na vyuo vingine vya fikra za kiakhlaqi. Kisha tukazungumzia baadhi ya maudhui zinazohusu akhlaqi za mtu binafsi kama kuijenga mtu nafsi yake, hulka njema, kuwa na bashasha, kusamehe, ukweli na kutunza amana na uaminifu.

Kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, kuanzia mfululizo huu wa 17 tutazungumzia akhalqi za kijamii. Kama tujuavyo, msingi wa kwamba mtu binafsi na jamii wana kipaumbele cha pamoja na chenye uzito sawa, ndio nukta kuu inayoupambanua na kuutafautisha mtazamo wa Uislamu na nadharia ya Ubepari wa Magharibi na Usoshalisti wa Mashariki; kwa sababu jamii, muundo wake unatokana na watu wake; na kwa hivyo kama tuna matarajio ya kuwa na jamii safi iliyojengeka kiakhlaqi, inatakiwa watu wenyewe wa jamii hiyo wapambike na thamani aali na tukufu za kiakhlaqi.

Moja ya misingi muhimu na yenye taathira kubwa sana ya akhlaqi za kijamii ni msingi wa umoja, mshikamano na kuwa na muelekeo mmoja; jambo ambalo limezingatiwa na kupewa umuhimu mkubwa katika aya za Qur'ani, Hadithi na mafundisho yanayoshajiisha umoja, ya dini tukufu ya Uislamu. Lakini kabla ya kuingia kwenye maudhui kuu ya mazungumzo yetu, ingefaa tuashirie machache kwanza kuhusu udharura na umuhimu wa umoja wa Waislamu katika kipindi hiki hasasi na chenye unyeti mkubwa cha zama zetu hizi.

Tunapoitupia jicho historia ya Uislamu tutabainikiwa na ukweli mchungu wa kwamba, tokea mwanzoni mwa kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad SAW, vinara wa shirki na ukafiri, kwa mashauriano na mashirikiano na Ahlul-Kitab, hususan Mayahudi na wanafiki, walitumia mbinu na hila tofauti ili kupanda mbegu za sumu ya mpasuko na mfarakano kwenye kitovu cha jamii ya Kiislamu kwa madhumuni ya kuivunja mihimili ya nguvu za utawala, umoja na mshikamano wa Waislamu; na siasa hizo chafu zimekuwepo katika zama zote za historia ya Uislamu na zingali zinaendelea kushuhudiwa katika kipindi hiki cha sasa. Hata hivyo licha ya njama zote hizo zilizofanywa na tawala za kishetani, kwa irada ya Mwenyezi Mungu na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyosambaratisha mahesabu yote ya maadui, Uislamu ulifufuka upya. Nguvu mpya uliyopata Ulimwengu wa Kiislamu na kambi madhubuti ya muqawama iliyoundwa vimeweza kwa nguvu na uwezo kamili kutoa vipigo vikali na kuwashinda mara kadhaa maadui zao wa kambi ya madola yenye nguvu za kimaonyesho tu.

Hapana shaka, njia pekee ya kuendeleza ushindi huu, ni kulindwa na kudumishwa umoja na mshikamano wa wananchi wa mataifa ya Waislamu waliopata mwamko wa kukabiliana na kambi iliyoungana ya ubeberu na uistikbari wa dunia.

Kwa mtazamo wa kitauhidi kuhusu ulimwengu, mhimili madhubuti zaidi na wa uhakika zaidi wa kuleta umoja katika dini ya Uislamu ni mbiu kuu ya wito unaolinganiwa na aya ya 103 ya Suratu Aal Imran usemao: "Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane." 

Ili kuufahamu uzito na taathira ya mtazamo huu, inatosha kufahamu kwamba kila pale umoja wa watu unapokuwa umejengwa juu ya misingi ya sababu za utaifa, rangi, ukabila, asili, jiografia, siasa, jeshi n.k baada ya kupita muda huvunjika na kusambaratika; na mara nyingi hupelekea kuwaka moto wa vita na uadui baina ya watu. Lakini Qur'ani, na ili kuwapa hakikisho waumini pale wanaposhikamana kwa msingi wa imani yao, inawaeleza katika aya ya 256 ya Suratul-Baqarah ya kwamba:  "Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua." 

Kwa hiyo umoja na makubaliano yoyote yanayofanyika katika Ulimwengu wa Kiislamu inapasa yafanyike kwa nia ya kidini ili yaweze kudumu na kuwa na hakikisho la utekelezaji. Tamaa na utegemezi wa aina yoyote ile kwa maajinabi na wasio Waislamu, ambao hawana lengo jengine ghairi ya kulinda manufaa na maslahi yao, hutuweka mbali na njia iliyonyooka ya Mwenyezi Mungu; njia ambayo ni kwa irada yake Yeye tu Mola huotesha ndani ya nyoyo mbegu za upendo; na kutokana na kufuta kila aina ya uadui, huwezesha umoja, mshikamano na urafiki kutanda kwenye anga ya mahusiano ya pande zote, ya Ulimwengu wa Kiislamu.

Mwenyezi Mungu, Mola Mrehemevu na Mwenye huruma anatupa taswira ya ukweli huo katika aya ya 63 ya Suratul-Anfal kwa kusema: "Na akaziunga nyoyo zao. Na lau wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima."

Ikiwa Waislamu wataunganisha safu na nguvu zao wakiwa na mtazamo huu, wakatumia uwezo na suhula zao zote adhimu za kimaada na kimaanawi walizonazo na wakasimama bega kwa bega kukabiliana na tawala za kishetani, bila ya shaka wataweza kuisambaratisha haiba bandia ya madola hayo na kuifanya bendera ya izza, heshima na ushindi ya Uislamu ipepee duniani; na kambi hiyo yenye nguvu ya Ulimwengu wa Kiislamu, mbali na kupata auni na msaada wa Mwenyezi Mungu, itakuwa pia kipenzi cha Yeye Mola. Ni kama wanavyoelezewa na aya ya nne ya Suratu-S'af ya kwamba: "Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigana katika Njia yake kwa safu kama jengo lilio kamatana."

Kama kuundwa kambi imara kama hiyo iliyoungana na kushikamana pamoja, inayorehemewa kwa kupata msaada wa Mwenyezi Mungu kutaandamana na subira na uendelevu katika kukabiliana na madhara, kutakuwa na mchango mkuu katika kufanikisha ushindi wa wapambanaji wake wanaomwepekesha na kumwabudu Mola pekee wa haki. Na kwa maelezo hayo basi, niseme pia mpendwa msikilizaji kwamba sehemu ya 17 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 18 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/

 

 

Tags