Akhlaqi Katika Uislamu (21)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 21 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Katika sehemu kadhaa zilizopita za kipindi hiki tumezungumzia misingi na thamani kadhaa muhimu; kama umoja, suluhu na upatanishi pamoja na kutetea na kusimamisha uadilifu; mambo ambayo yana mchango wenye taathira kubwa katika kuimarisha mahusiano ya kijamii. Ili kuhakikisha unapatikana uthabiti na kuendelezwa anga hiyo ya kuleta utulivu, ya kuondoa mivutano na yenye kupendeza, Uislamu umetoa miongozo mingine pia ambayo ndiyo tuliyopanga kuizungumzia katika sehemu hii ya 21 ya kipindi hiki.
Katika sehemu ya aya ya 29 ya Suratul-Fat'h, Qur'ani tukufu inayataja mahusiano ya kijamii ya wafuasi wa kweli wa Uislamu kuwa ni ruhamaau bayanhum, yaani "wenye kuhurumiana wao kwa wao". Imam Jaafar Sadiq (as) ameyafafanua maelezo hayo ya aya hiyo aliposema: "fanyianeni wema kama Mwenyezi Mungu alivyosema." (Usulul-Kafi). Na katika Hadithi nyingine mtukufu huyo amesema: "Muislamu ni ndugu wa Muislamu; hamdhulumu, hamwachi mkono (wakati wa shida), hamsaliti. Inastahiki Waislamu wajitahidi kuimarisha mahusiano yao, wahurumiane na wawe na hima ya kuwasaidia wahitaji; na waamiliane na wenzao kama alivyowataka Mwenyezi Mungu." (Usulul-Kafi).
Kila mtu, mpendwa msikilizaji, hukumbana na mchanganyiko wa matamu na machungu ya maisha, dhiki na faraji, kupata na kukosa na furaha na misiba. Lakini baadhi ya watu huwajali jamaa na marafiki zao, wakawathamini na kujiweka karibu nao pale dunia inapowapa uso na wakawa na uwezo na kipato. Lakini siku dunia inapowapa mgongo, wakapatwa na ufukara na kubaki hohehahe, wale wote waliokuwa wamewazunguka, hutawanyika na kuwaacha peke yao. Ni kama alivyonena mshairi: Jamaa na marafiki walikthiri nilipokuwa tajiri, lakini wote wamenikimbia na kuniacha mkono, kisa ni ufakiri.
Lakini kinyume na kundi hili ambalo ni la watu wa maslahi tu, kuna watu waungwana, waliolelewa wakaleleka, ambao hawawaachi mkono jamaa na marafiki zao katika hali yoyote ile, hasa pale wanapofikwa na shida, mateso na masaibu. Huwakimbilia kuwapa msaada wa hali na mali na kujitahidi kuwafuta machozi ya huzuni na majonzi na kuirejesha furaha na bashasha kwenye nyuso zao. Bwana Mtume Muhammad SAW, ambaye ni dhihirisho la juu kabisa la huruma na upendo katika watu amesema: "Yeyote amfurahishaye muumini, kwa kweli huwa amenifurahisha mimi; na yeyote anayenifurahisha mimi, kwa hakika huwa amemfurahisha Mwenyezi Mungu". (Usulul-Kafi). Nabii huyo wa rehma, ndiye iliyebainishwa shakhsia yake na Mwenyezi Mungu mwenyewe katika aya ya 128 ya Suratu-Tawba aliposema: "Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini, ni mpole na mwenye huruma."
Hapana shaka kuwa, kuwafurahisha watu walioghariki kwenye dimbwi la majonzi na huzuni huweza kuwa na taathira zaidi, pale mtu anapowaondolea majonzi na huzuni watu hao kwa hatua za kivitendo. Na ndipo Bwana Mtume SAW akasema: "Amali inayoependeza zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni ile ya kumuondolea huzuni na kumletea furaha mtu muumini, kumuondolea njaa aliyonayo na au kumtatulia matatizo yake." (Usulul-Kafi)
Kwa mtazamo wa kiujumla, muumini huwa ni mtu mwajibikaji na anayefikiria shida za watu; na hawezi kukaa vivi hivi tu anapowaona watu wanataabika na kuteseka. Bali hujaribu kufanya kila awezalo, ili kuwatua mzigo huo wa shida na matatizo uliowaelemea. Na sababu ni kwamba, yeye ameufahamu vizuri wito wa Bwana Mtume SAW ambaye amesema: "Mtu anayepambazukiwa na asubuhi bila kulipa umuhimu suala la kuchukua hatua ya kutatua matatizo ya Waislamu, si Muislamu wa kweli." (Usulul-Kafi).
Ni muhimu kutanabahisha pia kwamba, hisia hiyo ya uwajibikaji katika utamaduni unaojali utu, -wa dini ya Kiislamu- haijifungi na kuishia kwa Waislamu pekee, bali unajumuisha wanadamu wote, yaani kama ambavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu, Aliye Mwingi wa rehma na Mwenye kurehemu, alivyomtambulisha Mtume wake Muhammad SAW kuwa ni rehma kwa walimwengu wote, mtazamo wa nabii huyo mteule pia ni wa kujali na kuwazingatia wanadamu wote; na ndipo pale aliposema: "Yeyote atakayesikia kilio cha mtu aombaye msaada, apazaye sauti akisema, enyi Waislamu nipateni, na asimuitike, huyo si Muislamu". (Usulul-Kafi).
Imam Ali (as), ambaye alikulia kwenye chuo cha Unabii na nyumba ya Wahyi, wakati alipomteua Malik Ashtar kwenda kushika wadhifa wa Uliwali wa Misri alimkumbusha kupitia hati yake ya mwongozo wa utawala kwa kumwambia: watu waliochini ya uongozi wako hawatoki kwenye moja kati ya hali mbili; ama ni wenzako katika dini, (yaani ni Waislamu wenzako) au wenzako katika utu, (yaani wanadamu wenzio). Kwa hivyo katika hali zote hizo mbili, ni jukumu lako kuchunga haki zao za kidini na kiutu. Ni kama alivyonena malenga mashuhuri wa Uajemi Sa'adi ya kwamba: Wanadamu wote, wao kwa wao ni wamoja, kwani katika uumbwaji, wanatokana na asili moja. Kwa hivyo kama wewe hayakutii huzuni masaibu yawapatayo watu, haikustahiki wewe mwenyewe pia, kujiita mtu.
Kwa hivyo katika utamaduni wa Uislamu halisi, unaomjenga mwanadamu na ulio na upendo na watu, hawezi mtu kupuuza, akakaa bila kujali wala kushughulishwa na machungu na mateso wanayopata wanadamu wenzake. Bali atajihisi ana jukumu na masuulia kwao, bila kujali rangi na asili zao, eneo la kijiografia walipo, utaifa wao au hata dini zao. Na kwa msingi huo, ikiwa popote pale duniani, atatokea mtu aliyefikwa na shida akapiga mayowe ya kuomba msaada, itampasa Muislamu akimbilie kumsaidia kulingana na wajibu wake wa kidini na kiutu.
Bwana Mtume SAW, ambaye wito na ujumbe wake uliuhusu ulimwengu mzima, ameifananisha na kuichukulia jamii ya wanadamu kama familia moja iliyo chini ya ulezi wa Mwenyezi Mungu, Mola mwenye rehema na huruma, pale aliposema: "Wanadamu wote walivyo ni kama familia moja ya Mwenyezi Mungu; na apendezaye zaidi mbele ya Mola, ni yule mwenye faida kwao (ambaye kwa misaada yake ya kimaada na kimaanawi) huwafurahisha na kuwafariji. (Usulul-Kafi). Na kwa maneno hayo yenye maana kubwa yaliyosemwa na Nabii huyo wa rehma, niseme pia kwamba sehemu ya 21 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga mpendwa msikilizaji hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 22 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/