Dec 26, 2022 08:08 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (49)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 49 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki.

Kama tujuavyo, kupambana na madhalimu na kuwatetea wanaodhulumiwa na wanaonyongeshwa duniani ni miongoni mwa maudhui za akhlaqi za kisiasa katika Uislamu; na hiyo mpendwa msikilizaji ndio mada tutakayoizungumzia katika kipindi chetu cha leo. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Katika vipindi vyetu kadhaa vilivyopita tulichambua baadhi ya sifa za kipekee za utamaduni wa kisiasa wa Uislamu. Kuhusiana na maudhui hii tunaweza kusema kuwa, sifa na kielezi kingine muhimu cha mfumo wa kisiasa wa Uislamu halisi na wa asili, alioulingania Bwana Mtume SAW, ambao ni tofauti kabisa na Uislamu wa Kimarekani, ni kupambana na madhalimu na kuwatetea wanyonge na wanaodhulumiwa duniani. Kuna msemo na kaida maarufu isemayo: "Dunia inaweza kusimama juu ya misingi ya ukafiri, lakini haiwezi kudumu katu juu ya mihimili ya dhulma na uonevu".

Wakati Imam Ali (AS) alipokuwa katika lahadha za mwisho za uhai wake, baada ya kuhujumiwa kwa upanga katika mihrabu ya ibada na mtu mwenye fikra mgando na ufahamu potofu wa dini, aliwaachia wasia mzito, wa kihistoria na wa kudumu milele wanawe wapendwa Imam Hassan na Imam Hussein (AS). Katika sehemu moja ya wasia wake huo, mtukufu huyo alisema: "kuweni adui kwa madhalimu, na wasaidizi na watetezi kwa wanaodhulumiwa".

Kwa sababu hii, Uislamu, sio tu unakataza na kukemea vikali kushirikiana kwa namna yoyote ile na viongozi madhalimu, lakini umetilia mkazo pia suala la kupambana nao na kusimama imara kukabiliana nao; na unawataka Waislamu wenye imani ya kweli, walio tayari kujitolea nafsi zao na kutekeleza wajibu wao wa kidini, wachukue hatua za kivitendo kwa namna yoyote ile iwezekanayo, ili kuzuia upotoshaji, dhulma na upigaji vita dini unaofanywa na madhalimu hao.

Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein Ibn Ali (AS), alisimama kukabiliana na utawala wa kidhalimu wa Yazid Ibn Muawiya Ibn Abi Sufyan na jinai za Bani Umayyah, ili kwa kufanya hivyo, awaachie mfano wa milele wa kuiga, watetezi wote wa uhuru na ukombozi duniani. Katika hotuba aliyotoa kubainisha falsafa ya kuhuisha utamaduni huo wa kupiga vita dhulma wa Uislamu wa asili, Imam Hussein (AS) aliwaambia watu: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: Yeyote anayemwona mtawala dhalimu, anayehalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu, anayevunja ahadi ya Mwenyezi Mungu, anayepinga suna na sharia ya Mtume, anayefanya madhambi na maasi mbele ya waja wa Mwenyezi Mungu na anayepanda mbegu za uadui, kisha mtu huyo akaacha kupambana na dhalimu huyo wala kumpinga kwa kauli na matendo yake, basi (kwa sababu ya kimya anachoonyesha), itastahiki Mwenyezi Mungu amtupe kwenye Moto uleule atakaomvurumizia ndani yake huyo dhalimu". (Tabari, Juzuu ya Saba, Ukurasa wa 300).

Siasa na sera mojawapo ya watawala madhalimu ni kuzusha hofu na vitisho na kuzikandamiza na kuzidhoofisha jamii za watu waliochini ya tawala zao za kidhalimu. Katika hali na mazingira hayo, watu wanaoishi katika jamii hizo hugawika katika makundi mawili. Kundi moja, ni la wa watu wanaopata ilhamu ya utamaduni wa Uislamu, wa kupambana na dhulma, wakaamua kusimama kwa azma na irada thabiti kupinga na kuikabili dhulma na uonevu, hata kama kufanya hivyo kutahatarisha maisha na roho zao. Lakini kundi la pili, la watu wasiopenda tabu na dhiki huamua kuridhia na kuvumilia dhulma zozote wanazotendewa. Watu wa aina hii, ambao hawachukui hatua yoyote dhidi ya tawala za kidhalimu mpaka mwisho wa maisha yao, hukabiliwa na masuali yafuatayo ya malaika wakati wa kutolewa roho, kama aya ya 97 ya Suratu-Nisaa inavyosema: "Hakika wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao, wataambiwa: Mlikuwa katika hali gani? Watasema: Tulikuwa wanyonge katika ardhi. Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa pana mkahamia humo? Basi hao makaazi yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa".

Kwa mtazamo na uchambuzi wa kimantiki tunaweza kusema kwamba, ikiwa watu wa mataifa watakataa kunyongeshwa na kutonyamaza kimya mbele ya dhulma, wakasimama bila hofu wala woga na kupambana ili kuwang'oa watawala madhalimu na madikteta, hapana shaka tawala za kidhalimu za watenda jinai hao hazitaweza kubaki na kudumu. Kwa kweli sababu hasa ya kuendelea kubaki tawala za madhalimu, ni watu wanaoridhia kufanyiwa dhulma yoyote ile kwa kuhofia roho na mali zao. Na ni kwa sababu hii ndipo Qur'ani ikasema, makazi ya wale ambao ni washirika wa madhalimu katika dhulma zao zote wanazofanya zikiwemo za uporaji haki za watu na mauaji ya halaiki, ni katika moto wa Jahanamu. Na katika Hadithi imeelezwa kuwa: "dhalimu na anayeridhia kudhulumiwa, makazi yao wote wawili ni katika Moto wa Jahanamu".

Lakini ukiachilia mbali watu wanaoridhia dhulma na kunyongeshwa, kuna watu wa mataifa ambao husimama kidete kupambana na tawala za madhalimu na hawasiti kufanya lolote wawezalo ili kuziporomosha tawala hizo na kung'oa na kuitokomeza mizizi ya dhulma, lakini uwezo wao ni mdogo; na kwa hivyo huelekeza matumaini yao kwa msaada wa mataifa mengine ili yawaokoe na kutowaacha mkono katika kupambana na mateso na madhila yanayowakabili. Katika hali kama hii, ndipo unapodhihirika msingi mwingine muhimu wa utamaduni wa kisiasa wa Uislamu, mbali na ule wa kupiga vita dhulma. Msingi huo ni kusimama kuwasaidia na kuwakomboa wanaodhulumiwa. Aya ya 75 ya Suratu-Nisaa inaubainisha usuli huo kwa kusema: "Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako".

Kinyume na watu wenye mtazamo finyu, ambao wanaliweka suala la kuwasaidia wanyonge na wanaodhulumiwa kwenye mizani na mipaka ya kidini, kisiasa, kimbari na kijiografia, Qur'ani tukufu, na kama aya tuliyosoma inavyosema, inabainisha wazi kwamba, suala la kuwatetea wanaodhulumiwa halifungamanishwi na kitu chochote kile.

Bwana Mtume Muhammad SAW ameyafafanua maneno hayo ya wahyi kuhusiana na kuwasaidia na kuwakomboa wanaodhulumiwa bila kulifungamanisha suala hilo na kitu chochote aliposema: "Yeyote atakayesikia wito wa anayedhulumiwa akiita kwa kusema, enyi Waislamu nipateni, na yeye asimuitike, basi si Muislamu". (Usulul-Kafi, Juzuu ya 3).

Huku tukimwomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kuishuhudia siku ambayo, wale wote wanaodhulumiwa duniani watakomboka na mateso ya madhalimu, niseme pia kwamba, sehemu ya 49 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga mpendwa msikilizaji hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 50 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/