Jan 13, 2023 02:35 UTC
  • Alkhamisi tarehe 12 Januari 2023

Leo ni Alkhamisi tarehe 19 Jumadithani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Januari 2023.

Siku kama ya leo miaka 358 iliyopita, aliaga dunia Pierre de Fermat mwanahisabati wa Kifaransa na muasisi wa nadharia ya leo ya namba yaani Modern Theory of Numbers na ile ya uwelekeo inayojulikana kama Theory of Probability. Pierre de Fermat alizaliwa mwaka 1601 Miladia na alianza kujifunza hesabu tangu akiwa mdogo. Mwanahisabati huyo wa Kifaransa aligundua pia kanuni msingi ya jiometri changanuzi, yaani Analytic Geometry. Aidha Fermat ameacha athari ya kitabu cha 'Njia Tofauti za Hisabati' ambacho kilichapishwa mwaka 1679 Miladia.

Pierre de Fermat

Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, alizaliwa Jack London mwandishi mashuhuri wa nchini Marekani. Kwa miaka kadhaa Jack alifanya safari katika eneo la ncha ya Kaskazini na maeneo mengine na kupata bahati ya kufahamiana na koo na kaumu mbalimbali katika maeneo hayo sambamba na kubainisha taswira ya masuala hayo katika vitabu vyake.  Jack London aliishi kwa muda wa miaka 40 huku akijihusisha na kazi ya uandishi kwa muda wa miaka 18.

Jack London

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita, sawa na tarehe 22 Dei 1313 Hijiria Shamsia, alifariki duania akiwa na umri wa miaka 79 Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani mmoja wa maulama wakubwa. Awali alianza kusoma mjini Isfahani kwa wasomi wakubwa kama vile Ayatullah Mirza Abul-Maali Kalbasi na Ayatullah Muhammad Baqer Masjid Shahi na baadaye akaelekea mjini Najaf, Iraq kwa ajili ya kukukamilisha masomo yake ya Kiislamu. Baadaye Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani alirejea mjini Isfahan na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji, uandishi na kufanya tablighi ambapo maulama wakubwa zaidi ya 300 walikuwa wakisoma kwake. Mbali na uga wa elimu, msomi huyo alikuwa hodari katika kutoa hotuba ambapo alikuwa akiwalingania watu wa matabaka tofauti. Miongoni mwa athari za Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani ni kitabu cha 'Sharhu Sharaai' chenye juzuu mbili, 'Jannatul-Ma'waa' kinachohusu Akhlaaq, 'ufafanuzi wa tafsiri ya Swaafi' na 'Wasiilatun-Najaat.'

Ayatullah Sayyid Abulqasim Dehkordi Esfahani

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita yaani tarehe 12 Januari mwaka 1964 kulitokea mapinduzi visiwani Zanzibar na Sheikh Abeid Amani Karume aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Afro Shiraz kwa kifupi ASP, akawa rais wa kwanza wa visiwa hivyo. Mapinduzi hayo yaliuondoa utawala wa Kisultani. Si vibaya kuashiria kuwa, Zanzibar na Tanganyika ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 26 Aprili mwaka 1964. Uhuru wa Zanzibar ulipatikana tarehe 10 Desemba mwaka 1963. Zanzibar inaundwa na visiwa viwili vya Unguja na Pemba  huku zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wake wakiwa ni Waislamu.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, Imam Khomeini Mwenyezi Mungu Amrehemu Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran aliagiza kuundwa Baraza la Mapinduzi katika kipindi hicho muhimu cha harakati za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Imam aliagiza baraza hilo liundwe wakati Marekani ilipokuwa ikifanya njama za kuulinda utawala wa kifalme wa Pahlavi. Jukumu kubwa la baraza hilo lilikuwa ni kuratibu mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, kupeleka mbele malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na pia kuandaa uwanja mzuri wa kuundwa serikali ya muda nchini Iran. Katika ujumbe wake Imam Khomeini alisema: "Takwa la wananchi Waislamu wa Iran si tu ni kuondoka Shah na kuung'oa madarakani mfumo wa kifalme, bali ni kuendeleza mapambano ya taifa la Iran na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu ambayo itaambatana na uhuru wa kitaifa na kujitegemea nchi hii na pia kudhamini uadilifu wa kijamii."

Wanachama wa Baraza la Mapinduzi

Siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, mhadhiri wa nyuklia wa Chuo Kikuu cha Tehran, Dokta Massoud Ali-Mohammadi aliuawa kigaidi. Massoud Ali-Mohammadi aliyekuwa na umri wa miaka 50 aliuawa kwa mlipuko wa bomu la kuongozwa kutoka mbali wakati alipokuwa akitoka nyumbani kwake. Alipata shahada ya uzamivu ya taaluma ya fizikia katika Chuo Kikuu cha Sharif mjini Tehran mwaka 1371 na alikuwa miongoni mwa wanachuo wa kwanza wa Iran kupata shahada ya uzamivu ya somo la fizikia ndani ya Iran. Alitunukiwa tuzo ya Tamasha ya Kimataifa ya Kharazmi mwaka 1386 na kushika nafasi ya pili katika utafiti wa masuala ya kimsingi. Wapinzani wa miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran baada ya kushindwa kusimamisha miradi hiyo kwa hatua za kisiasa na vikwazo vya kiuchumi walikhitari kutumia njia za kigaidi na kuwaua wasomi wa nyuklia wa Iran. Magaidi waliomuua msomi huyo wa Iran walitiwa nguvuni na kukiri kwamba walikuwa wakishirikiana na utawala haramu wa Israel.

Dokta Massoud Ali-Mohammadi

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi wenye ukubwa wa 7 kwa kipimo cha Rishta ulitokea huko Haiti katika bahari ya Caribbean. Zilzala hiyo ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea duniani katika miongo kadhaa iliyopita na iliua watu karibu laki tatu na kujeruhi wengine wengi. Mtetemeko huo wa ardhi ulioikumba Haiti uliharibu kabisa miundo mbinu na nyumba nyingi za nchi hiyo. Aidha ulipelekea mamia ya maelfu ya raia kuwa wakimbizi.