Jumanne, tarehe 18 Aprili, 2023
leo ni Jumanne tarehe 27 Ramadhani 1444 Hijria sawa na 18 Aprili 2023.
Miaka 884 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu alizaliwa huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".
Siku kama ya leo miaka 334 iliyopita aliaga dunia Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Allamah Majlisi aliandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu. Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa sala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza hadithi za Mtume wa Uislamu na Ahlul Bait zake watoharifu. Idadi ya vitabu vilivyoandika na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na umashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayat na Zadul Maad.
Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, alizaliwa Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika mji wa Mash'had huko kaskazini mashariki mwa Iran. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alikuwa mwana wa marhoum Hujjatul Islam wal Muslimin Hajj Sayyid Javad Husseini Khamenei na alikuwa mtoto wa pili katika familia. Maisha ya Sayyid Javad Khamanei, sawa na ya wanazuoni wengi yalikuwa sahali na ya kawaida kabisa. Ayatullah Khamenei alipata malezi bora katika familia ya kidini na kuanza kusoma akiwa na umri wa miaka minne. Akiwa na umri wa miaka 18, Ayatullah Khamenei alianza masomo chini ya usimamizi wa mwanazuoni na marjaa maarufu Ayatullahil Udhma Milani. Sayyid Ali Khamenei alianza masomo ya dini chini ya usimamizi wa baba yake na kupiga hatua zaidi za maendeleo katika uwanja huo. Hatimaye alielekea katika mji mtakatifu wa Qum na kuendelea na masomo ya juu kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kwa muda wa miaka saba. Wanazuoni kama Imam Khomein MA, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai ni miongoni mwa wasomi ambao Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alipata elimu kutoka kwao. Katika kipindi cha ujana wake Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei alijiunga na harakati za Imam Khomein MA za kuupinga utawala wa kidikteta wa Shah. Alieneza fikra za Imam Khomein na kufichua ufisadi wa viongozi waliokuwa katika utawala wa wakati huo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikamatwa na kutiwa gerezani mara kadhaa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa mwanachama wa Baraza la Mapinduzi na kisha baada ya hapo, aliwahi pia kuchaguliwa kuwa mbunge na pia mwanachama wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu. Aidha alikuwa Rais wa Iran katika duru mbili mfululizo na hatimaya mwaka 1989, baada ya kuaga dunia Imam Khomeini MA, alichaguliwa na Baraza la Wataalamu kuwa Kiongozi wa pili wa Iran.
Miaka 69 iliyopita katika siku kama ya leo, Gamal Abdel Nasser alifanya mapinduzi dhidi ya Muhammad Nagib na kuwa Rais wa nchi hiyo. Gamal Abdel Nasser ndiye aliyetaifisha na kuitangaza kuwa mali ya taifa Kanali ya Suez na alikuwa na nafasi muhimu katika juhudi za kukabiliana na ubeberu katika ulimwengu wa Kiarabu na barani Afrika. Aidha rais huyo wa zamani wa Misri alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM.
Katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, mkutano wa kwanza wa wawakilishi wa nchi za Asia na Afrika uliojulikana kwa jina la Mkutano wa Bandung ulifanyika katika mji wenye jina hilo nchini Indonesia. Mkutano huo uliowashirikisha wajumbe kutoka zaidi ya nchi 29 za Asia na Afrika, ulikuwa na lengo la kujenga umoja wa nchi hizo za ulimwengu wa tatu katika kukabiliana na kambi kubwa mbili duniani za Mashariki na Magharibi. Mkutano wa Bandung ndio ulioandaa mazingira ya kuundwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).
Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 18 Aprili 1980, Zimbabwe ambayo wakati ule ilikuwa ikijulikana kwa jina la Rhodesia, ilipata uhuru. Zimbabwe ilikoloniwa na Uingereza mwishoni mwa karne ya 19. Mara baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kufuatia kudhoofika Uingereza, zilianza harakati za wananchi za kupigania uhuru na hatimaye harakati hizo zilipelekea kuundwa makundi ya mapambano ya silaha. Zimbabwe ina ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 390,000 na inapakana na nchi za Msumbiji, Zambia, Botswana na Afrika Kusini.
Miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 18 Aprili 1996, jeshi la anga la utawala wa Kizayuni wa Israel lilishambulia makao ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika kijiji cha Qana, kusini mwa Lebanon. Katika shambulizi hilo la kinyama la Wazayuni, takribani raia 110 wa Lebanon waliuawa shahidi wakiwemo wanawake na watoto. Licha ya hayo, Marekani ilizuia kupasishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa azimio la kulaani mauaji ya kijiji cha Qana yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Na miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 29 Farvardin mwaka 1358 Hijria Shamsiya, Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilitangaza utiifu kwa Imam Khomeini (MA) Hayati Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Siku hiyo Jeshi lilitangaza utiifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mnasaba huo likaandaa gwaride zisizo na kifani kote Iran.
Gwaride hizo zilipokelewa kwa vuraha na wananchi Waislamu wa Iran kwani zilikuwa ni dhihirisho la mshikamano wa wananchi na jeshi katika njia ya kulinda Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu na taifa la Kiislamu. Kwa msingi huyo katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku hiyo hutambuliwa kama 'Siku ya Jeshi' na kila mwaka huandaliwa gwaride maalumu kwa mnasaba huo.