May 22, 2023 12:02 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 850 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 39 ya Az-Zumar. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 51 ya sura hiyo ambayo inasema:

فَأَصَابَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا ۚ وَالَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْ هَـٰؤُلَاءِ سَيُصِيبُهُمْ سَيِّئَاتُ مَا كَسَبُوا وَمَا هُم بِمُعْجِزِينَ

Basi ukawasibu ubaya wa waliyo yachuma. Na wale walio dhulumu miongoni mwa hawa utawasibu ubaya wa waliyo yachuma. Nao si wenye kushinda.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizowazungumzia watu wasio washukurivu, ambao wanapofikwa na shida humkumbuka Allah, lakini wanapopata neema na raha humsahau na kuitakidi kuwa neema walizonazo zimetokana na juhudi zao wao wenyewe na si Allah SW! Baada ya maelezo ya aya hizo, aya hii ya 51 inasema: Shida na matatizo yaliyokuwa yamewapata watu hao yalikuwa matokeo ya amali na matendo yao, kama ambavyo, katika mustakabali pia, watakuja kuyaona matokeo ya dhulma walizozifanya jana yao na kuendelea kuzifanya hadi hii leo. Bila shaka malipo halisi na kamili ya adhabu kutokana na amali zao watayapata Siku ya Kiyama na wala wasidhani kwamba wataweza kuikwepa adhabu ya malipo ya amali zao, hapa duniani au huko akhera. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kama ilivyo kwa mfumo wa kimaada katika maumbile, ambapo kanuni ya tendo na mjibizo, yaani action and reaction huwa inatawala, hilo pia linathibiti katika utaratibu wa Allah kuhusu amali za mwanadamu. Kwa hiyo amali zake mja zitafuatiwa na radiamali mwafaka ya Mola, ambayo ataishuhudia mtu mwenyewe, iwe leo au kesho, mwaka huu au mwakani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, neema tuzipatazo zinatokana na Allah, lakini akthari ya shida na matatizo yanayotufika ni matokeo ya maamuzi na hatua zisizo sahihi tunazochukua sisi wenyewe.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 52 ambayo inasema:

أَوَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

Kwani wao hawajui kwamba Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye na humkunjia? Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao amini.

Kama tulivyoeleza katika darsa iliyopita, baadhi ya watu huona wamepata neema walizonazo kutokana na elimu na ujuzi wao. Aya hii inaupinga mtazamo huo potofu na kueleza kwamba: Riziki, asili yake inatokana na Mwenyezi Mungu na iko mikononi mwake Yeye Mola; kwa hiyo si kama wanavyodhani watu hao, kwamba kila mwenye elimu na ujuzi ana uhakika wa kujipatia riziki. Bila shaka mwanadamu ana wajibu wa kujifunza elimu na ujuzi na kufanya hima na juhudi za kuhangaikia maisha yake; na kimsingi, Allah SW hawapendi watu wajinga au wavivu wasiojishughulisha. Lakini pamoja na hayo, mtu isimpitikie akadhani kwamba, kila kitu kinafuata irada na matakwa yake au kinategemea jitihada na juhudi zake. Riziki, ni kile kitu ambacho mwishowe huwa kinamfikia mwanadamu na kinategemea mambo na sababu mbali mbali za mtu binafsi na za kijamii; na Yeye Allah anaigawa riziki baina ya waja wake kulingana na hekima Yake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, jukumu letu sisi ni kujituma na kutafuta chumo la halali la maisha, lakini kuhusu kiwango cha fungu la riziki analopata kila mtu, hilo tujue linafuata hekima ya Allah SW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, uadilifu wa Mwenyezi Mungu katika suala la riziki haumaanishi watu wote kupata kiwango sawa cha riziki, bali Yeye Mola, na kwa kuzingatia sababu mbali mbali alizoweka katika mfumo wa ulimwengu na uumbaji, amevitafautisha viwango vya riziki za waja wake. Na tab'an kila mtu atakwenda kusailiwa na kuulizwa kulingana na kiwango cha riziki alichojaaliwa.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 53 ambayo inasema:

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ

Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Aya hii wapenzi wasikilizaji, ni moja ya aya za Qur'ani tukufu zenye kumpa matumaini makubwa zaidi mja. Katika aya hii, Allah SW ametumia lugha yenye upeo wa juu kabisa wa huruma na upendo na kuwafungulia mlango wa rehma zake waja wake wote na kuwa tayari kutoa msamaha kwa wao wote. Aya inawahutubu wafanya madhambi wote na wale waliozidhulumu nafsi zao kwa kuutumia umri na uwezo wao wote katika mambo ya batili na yasiyo na maana yoyote, na kuwatangazia kwamba: Njia ya kujirudi na mlango wa toba uko wazi daima; na kutokana na wema na rehma za Allah zilivyo, haifai kwa mtu yeyote kukata tamaa na rehma zake Mola na kudhani kwamba, Yeye Mola Mrehemevu hawezi kumsamehe makosa aliyofanya. Naam, milango ya maghufira na rehma imefunguliwa kwa waja wote. Muhimu ni mtu mwenyewe tu ajirudi na kufahamu kuwa amekosea. Pale mtu anapojuta majuto ya kweli na akaamua kwa dhati kubadilisha mwenendo wake kwa kuiacha njia ya makosa aliyokuwa akiifuata, hujiandalia mazingira ya kupata maghufira na msamaha wa Allah, na Yeye Mola humsamehe mja wake huyo. Huu ni katika wema na uraufu wa Mwenyezi Mungu kuwahutubu na kuwachukulia wafanya madhambi kuwa ni waja wake; sawa na alivyo baba aliyekerwa na vitendo vibaya vya mtoto wake, ambaye anapomuasa aache vitendo hivyo viovu humwambia: Vyovyote itakavyokuwa, wewe ni mwanangu, na mimi nimekusamehe uliyofanya huko nyuma. Ila jitahidi kuanzia sasa usije ukayarudia tena makosa yale. Kwa hakika ibara isemayo "waliojidhulumu nafsi zao" iliyomo katika aya hii, inamaanisha kwamba, ewe mwanadamu, vitendo viovu unavyofanya, havimdhuru yeyote ghairi ya wewe mwenyewe, basi usijidhulumu, ifikirie nafsi yako. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, rehma za Mwenyezi Mungu hazina mpaka, bali zinawaenea waja wake wote na wala haziwahusu waumini peke yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kughufiriwa madhambi kunahitajia rehma za Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo, haifai kuvunjika moyo na kukata tamaa ya kupata rehma za Mola; na haipasi katika hali yoyote ile wafanya madhambi kukata tamaa ya kupata rehma za Allah SW. Aidha aya hii inatutaka tuelewe kwamba, kufanya dhambi ni aina mojawapo ya kujidhulumu na kukengeuka njia ya kadiri na wastani. Vile vile aya hii inatufunza kuwa, mtu anayeasi amri ya Mwenyezi Mungu kwa kufanya dhambi, huwa kwa hakika hamdhuru Allah, ila anajidhuru yeye mwenyewe. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 850 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe taufiki ya kutubia toba za kweli kwa dhambi zetu kabla ya mauti, atakabali toba zetu na atufishe akiwa radhi nasi. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags