May 24, 2023 11:29 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 896. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 42 ya Ash-Shuura, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya kwanza hadi ya nne ya sura hiyo ambazo zinasema:

حم

H'a Mim

وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ

Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha.

إِنَّا جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ

Hakika Sisi tumeifanya Qur'ani kwa Kiarabu ili mfahamu.

 وَإِنَّهُ فِي أُمِّ الْكِتَابِ لَدَيْنَا لَعَلِيٌّ حَكِيمٌ

Na hakika hiyo imo katika mama wa Kitabu kilichoko Kwetu, ni tukufu na yenye hikima.

Kama tulivyoeleza, Suratuz-Zukhruf ni sura ya 43 ya Qur'ani na ina aya 89. Sura hii, kama zilivyo sura nyingine zilizoteremshwa Makka, inazungumzia masuala ya imani na itikadi kama asili ya uumbaji, maadi, yaani kufufuliwa viumbe na utume. Kuna sura saba za Qur'ani, ambazo zimeanza kwa herufi za mkato za "Haamiim". Suratuz-Zukhruf ni moja kati ya sura hizo; na kama zilivyo sura nyingine zinazofanana nayo, baada ya herufi hizo yamefuatia maelezo kuhusu Qur'ani na kuteremshwa kwake kwa ajili ya kuwaelekeza watu kwenye uongofu. Kwa hiyo katika sura hii pia, na kama tulivyotangulia kueleza, baada ya herufi hizo za mkato, Allah SWT ameapa kuiapia Qur'ani na kueleza kwamba, hakika na ukweli wa kitabu hicho uko wazi; ni kibainisho cha kuonyesha kwa uwazi kabisa njia ya saada na uongofu. Wahutubiwa wa mwanzo wa kitabu hicho walikuwa wazungumzaji wa lugha ya Kiarabu; na kitabu chenyewe cha Qur'ani kimeteremshwa kwa lugha ya Kiarabu. Lakini pamoja na hayo, haikukusudiwa kaumu ya Waarabu peke yao au watu wenye asili ya lugha hiyo tu, bali yaliyomo ndani yake wanaweza kuyafahamu na kuyaelewa watu wa kila mahala na zama. Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye aliyeteremsha Qura'ni, amewataka wanadamu wote watumie akili zao kuzitafakari aya zake, wazingatie mafundisho yake matukufu na waiamini kwa basira, maarifa na uelewa kamili. Ni wazi kuwa, baada ya kukiamini kitabu hiki, inatakiwa mtu ayafuate na kuyatekeleza mafundisho yake yanayomjenga mtu na kumtatulia yote yanayomtatiza. Kinyume na wanavyodai baadhi ya watu kwamba Qur'ani ni maneno ya mtu aitwaye Muhammad, ukweli ni kwamba Qur'ani tukufu ni maneno ya Mwenyezi Mungu na asili na hakika yake iko kwake Yeye Mola, imehifadhiwa na kutunzwa kwenye Ummul-Kitaab, yaani Kitabu Mama au Lawhul-Mahfuudh. Ni kitabu ambacho kutokana na ujuzi na hikma ya Allah, ndilo chimbuko la vitabu vyote vya mbinguni. Ukweli na hakika kuhusu ulimwengu, sababu za kupatia saada na fanaka na chanzo cha kuharibikiwa na kuhasirika mwanadamu pamoja na yale yanayohitajika kumjenga kihikma na kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiutu yamebainishwa ndani ya kitabu hicho chenye daraja ya juu ya utukufu na kilichotukuka na kutakasika na utiaji mkono wa kupotosha na kubadilisha yaliyomo ndani yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur'ani ina daraja ya utakatifu mpaka Allah SWT ameipa hadhi ya kuiapia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuchagua kufuata njia ya Mwenyezi Mungu inatakiwa kufanyike kwa tafakuri na kutumia akili, si kufuata kwa kuiga na kwa mazoea tu. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, ujumbe waliokuja nao Mitume wote na yaliyomo ndani ya vitabu vyote vya mbinguni ni mamoja; kwa sababu yameteremshwa kutoka kwenye chemchemi na chimbuko moja.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya tano hadi ya nane ambazo zinasema:

أَفَنَضْرِبُ عَنكُمُ الذِّكْرَ صَفْحًا أَن كُنتُمْ قَوْمًا مُّسْرِفِينَ

Je! Tuache kukukumbusheni kabisa kwa kuwa nyinyi ni watu mlio pita mipaka?

وَكَمْ أَرْسَلْنَا مِن نَّبِيٍّ فِي الْأَوَّلِينَ

Na Manabii wangapi tuliwatuma kwa watu wa zamani!

وَمَا يَأْتِيهِم مِّن نَّبِيٍّ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ

Na hakuwajia Nabii yeyote ila walikuwa wakimkejeli.

فَأَهْلَكْنَا أَشَدَّ مِنْهُم بَطْشًا وَمَضَىٰ مَثَلُ الْأَوَّلِينَ

Na tuliwaangamiza walio kuwa na nguvu kushinda wao. Na mfano wa watu wa zamani umekwisha pita.

Moja ya kaida na utaratibu aliouweka Allah SWT katika zama zote za historia ni kutuma Mitume na kuteremsha vitabu vya mbinguni kwa ajili ya kuwaongoza na kuwaelekeza watu kwenye uongofu. Lakini kila mara yametokea makundi ya watu na watawala waliosimama kuupinga wito wa mbinguni na wakatumia mbinu mbalimbali ikiwemo ya kutusi, kukejeli na kufanya shere na stihzai ili kuzidunisha shakhsia za Mitume hao wa Allah. Wakati mwingine, upinzani huo ulifikia kiwango cha juu, kwa watu hao kutumia wenzo wowote ule ili kuzuia mafundisho ya Mitume yasienee. Na ili kufikia lengo hilo, waliweza hata kuanzisha vita na mapigano, bali hata kuwaua Mitume na wafuasi wao. Lakini pamoja na hayo, Mwenyezi Mungu hakusitisha kutuma Mitume, na wala hakuwaacha kama walivyo watu waliofanya maovu hayo dhidi ya Mitume wake na wafuasi wao. Na bila shaka mwisho wa ubaya wa wapinzani wa haki ulikuwa ni kuangamizwa, na hatima yao ikawa funzo la ibra na mazingatio kwa wengine. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, vikwazo na vizuizi visiwafanye viongozi na wafanya tablighi ya dini warudi nyuma katika kutekeleza jukumu lao la kufikisha wito wa haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, waumini wasiyumbe na kulegalega kwa sababu ya kejeli na stihzai za wapinzani. Kwa sababu Mitume wa Allah walikuwa wakifanyiwa shere na stihzai kila mara na makafiri, lakini viongozi na waja hao wateule walisimama imara na wala hawakutetereka katika kuendeleza kazi ya kulingania wito wa haki. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, adhabu ya Mwenyezi Mungu haihusiani na akhera pekee, bali baadhi ya kaumu zilizokuwa na nguvu na zikakithiri katika kuchupa mipaka na kufanya israfu, zilihilikishwa na kuangamizwa papa hapa duniani.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya tisa na ya 10 ambazo zinasema:

وَلَئِن سَأَلْتَهُم مَّنْ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ لَيَقُولُنَّ خَلَقَهُنَّ الْعَزِيزُ الْعَلِيمُ

Na ukiwauliza: Nani aliye ziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Kaziumba Mwenye nguvu, Mjuzi, 

الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ مَهْدًا وَجَعَلَ لَكُمْ فِيهَا سُبُلًا لَّعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ

Ambaye amekufanyieni ardhi kama tandiko, na akakufanyieni ndani yake njia mpate kuongoka. 

Aya hizi zinaashiria risala na ujumbe wa Mitume katika kuamsha fitra na maumbile yaliyolala ya watu ili yazingatie na kumuelekea Muumba wao na kueleza kwamba: kama washirikina waliokuwa wakiabudu masanamu wangeulizwa Muumba wa ulimwengu ni nani, basi wangekiri kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba mbingu na ardhi. Kutokana na kushughulishwa zaidi na pirika za kila siku za maisha, watu wengi hujisahau, wakaghafilika na suala la asili au mwanzo wa ulimwengu na mwisho wake. Hushughulishwa na kula na kulala na raha na starehe za maisha huku wakifanya kila wawezalo ili kufanikisha malengo hayo kwa kujichumia na kujilimbikizia mali ili kuendesha maisha yao kwa raha. Wanashughulishwa na mambo hayo wakati hilo silo lengo halisi la maisha; na hata kama mtu atafikia malengo ya kukidhi matashi yake kwa vitu hivyo vya kimaada, hatajihisi amepata fanaka na saada ya kuiridhisha nafsi na batini yake. Mitume wa Mwenyezi Mungu wamekuja ili kuwapa watu maonyo na indhari, kwamba wasighafilike na umuhimu wa kufikiria hatima ya amali na matendo yao; na wala mashughuliko ya kimaisha yasiwasahaulishe Mola wao. Mola ambaye ndiye aliyewaumba na akawajaalia neema mbalimbali. Ni Yeye Mwenyezi Mungu aliyeifanya ardhi kuwa tandiko na mahali pa kumpa utulivu mwanadamu. Nukta moja ambayo inapasa tuizingatie ni kwamba, ijapokuwa ardhi ina harakati za aina kadhaa, lakini kutokana na kanuni ya mvutano na sababu zinginezo, inabaki kuwa tulivu kiasi cha kuwafanya wakazi wake wasihisi adha yoyote. Neema nyingine ni kwamba Yeye Allah SWT amekuwekeeni njia mbalimbali katika ardhi za kukuongozeni na kukufikisheni mnakokusudia kwenda. Inafaa tuashirie hapa kuwa, karibu sehemu zote za nchi kavu katika ardhi zina sura ya nyufa na mipasuko iliyojazwa juu yake milima mikubwa na midogo pamoja na mabonde. Lakini kitu chenye kutoa mguso ni kwamba baina ya vigingi vya milima hiyo mirefu iliyokwenda juu katika pembe mbalimbali za dunia kuna mianya na nafasi za wazi ambazo mwanadamu huzitumia kupata njia ya kumpitisha na kumfikisha anakoelekea. Hii yenyewe ni katika rehma za Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Na kama ni hivyo, ni Mola huyo tu aliyemjaalia mwanadamu neema zote hizo na ambaye ndiye Muumba na Mwendeshaji wa ulimwengu, ndiye anayestahiki kuabudiwa. Na ni kwa kumwabudu na kumtii Yeye, ndipo mwanadamu ataweza kunufaika na neema zake za duniani; na huko akhera pia kuingizwa kwenye Pepo ya milele. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kumjua Mwenyezi Mungu ni jambo la kimaumbile, lakini pamoja na hayo mtu anahitaji kukumbushwa na kutanabahishwa ili asije akamsahau Mola wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuzitafakari neema za Mwenyezi Mungu katika maisha ni njia bora ya kujivua na mghafala na kukwangua kutu za usahaulifu ndani ya moyo na roho ya mtu. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, Mungu aliyeumba mbingu na ardhi na akaweka ardhini nyenzo na suhula zote anazohitaji mwanadamu, amempangia pia kiumbe huyo sababu na njia ya kumfikisha kwenye uongofu ili aweze kupata neema na saada ya duniani na akhera. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 896 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/