Sura ya Az-Zukhruf, aya ya 49-56 (Darsa ya 903)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 903 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 43 ya Az-Zukhruf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 49 na 50 za sura hiyo ambazo zinasema:
وَقَالُوا يَا أَيُّهَ السَّاحِرُ ادْعُ لَنَا رَبَّكَ بِمَا عَهِدَ عِندَكَ إِنَّنَا لَمُهْتَدُونَ
Na wakasema: Ewe mchawi! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa ile ahadi aliyo kuahidi; hakika sisi tutakuwa wenye kuongoka.
فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُمُ الْعَذَابَ إِذَا هُمْ يَنكُثُونَ
Basi tulipo waondolea adhabu hiyo, mara wakaingia kuvunja ahadi.
Katika darsa iliyopita tulizungumzia juhudi alizofanya Nabii Musa (as) za kumfikishia wito wa uongofu Firauni na watu wake pamoja na miujiza tofauti aliyowaonyesha ili kuthibitisha ukweli wa Utume wake. Aya hizi tulizosoma zinasema: Watu hao hawakuujali ujumbe uliokuwemo kwenye wito wa Nabii Musa, aliyewalingania tauhidi na kutii amri za Muumba wa ulimwengu na kujiepusha na makatazo yake. Lakini walipokuja kufikwa na mabalaa, masaibu na misukosuko walimtaka Mtume huyo amwombe Mwenyezi Mungu awaondolee mabalaa na masaibu hayo na kuahidi kwamba, wakiondokwa na masaibu hayo watamwamini Nabii Musa na kuukubali wito wake. La ajabu ni kwamba, licha ya kumwomba Mtume wao huyo msaada, lakini waliendelea kumwita mchawi. Walikuwa wakidhani, Mitume pia, kama walivyo wachawi, hufanya mambo ya ajabuajabu yaliyo nje ya uwezo wa mtu wa kawaida ili kuwateka na kuwavuta watu. Hii yenyewe inaonyesha kuwa ahadi waliyotoa watu hao waliokuwa na kibri na ghururi kwamba wataamini, ilikuwa ya uongo. Ukweli ni kwamba walipokuwa wametanzwa, walitaka wapate njia ya kuwaokoa na mabalaa yaliyowafika; na si kwamba walikuwa na nia ya kweli ya kuufuata uongofu. Na ndiyo maana aya iliyofuatia inasema, wakati tulipowaondolea tabu, misukosuko na mabalaa, walihalifu ahadi waliyotoa na wala hawakuamini. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, aghalabu ya watu, wakati wanapotingwa na mambo huwakimbilia mawalii wa Mwenyezi Mungu ili wawaombee dua Allah awaondolee masaibu hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati wa kufikwa na masaibu na hatari, fitra na maumbile ya kumjua Mwenyezi Mungu huzinduka kutoka kwenye usingizi wa mghafala na mtu humkumbuka Mola; lakini baada ya kuondokewa na misukosuko na masaibu, hughafilika tena na kumsahau Allah.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 51 hadi 53 ambazo zinasema:
وَنَادَىٰ فِرْعَوْنُ فِي قَوْمِهِ قَالَ يَا قَوْمِ أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ۖ أَفَلَا تُبْصِرُونَ
Na Firauni alitangaza kwa watu wake, akisema: Enyi watu wangu! Kwani mimi sinao huu ufalme wa Misri, na hii mito inapita chini yangu? Je! Hamwoni?
أَمْ أَنَا خَيْرٌ مِّنْ هَٰذَا الَّذِي هُوَ مَهِينٌ وَلَا يَكَادُ يُبِينُ
Au mimi si bora kuliko huyu aliye mnyonge, wala hawezi kusema waziwazi?
فَلَوْلَا أُلْقِيَ عَلَيْهِ أَسْوِرَةٌ مِّن ذَهَبٍ أَوْ جَاءَ مَعَهُ الْمَلَائِكَةُ مُقْتَرِنِينَ
Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu, au hawakuja Malaika pamoja naye wakamwandama?
Firauni na kaumu yake, kwa upande mmoja, walijionea kwa macho yao miujiza aliyowapelekea Nabii Musa (as); na kwa upande mwingine, kutokana na dua aliyowaombea Mtume huyo, waliondolewa mabalaa na misukosuko iliyowafika. Lakini pamoja na hayo, taghuti huyo na watu wake hawakuwa tayari kuukubali wito wa haki wa Musa (as). Na ili kuwafanya washauri wake na kaumu yake wasiathirike na kuvutiwa na maneno ya mantiki na miujiza ya Mtume huyo wa haki, akaamua atumie mbinu ya ubabaishaji ili kuzuia mvuto wa Nabii Musa ndani ya nyoyo za watu. Kwa hivyo akajaribu kufanya hila ya eti kumdunisha Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu na kujikweza yeye mwenyewe. Akiwa mbele ya kaumu yake, Firauni alitamba na kusema: Kwani utawala wa ardhi hii kubwa ya Misri si wangu mimi? Na hii mito nayo, kwani haiko chini ya amri na mamlaka yangu na haipiti kando ya kasri langu na kwenye konde na bustani zangu? Lakini yeye Musa ana nini alichonacho? Si ufasaha wa kuzungumza, si malaika yoyote anayeandamana naye na wala hayuko kama walivyo wakubwa wa jamii yoyote ile, wenye kila aina ya mapambo, mavazi ya kujivunia na makasri ya kujifakharisha. Chochote kile mkitakacho mimi ninacho, lakini yeye hana kitu chochote. Kama ni hivyo, kwa nini tumwamini na kumfuata yeye. Mto Nile ulikuwa chemchemi na chanzo cha mito yote midogomidogo ya Misri na ulikuwa na taathira kubwa katika kustawisha maeneo mbalimbali ya ardhi hiyo. Mto huo ambao ulikuwa ukikidhi mahitaji ya maji ya kunywa na ya kilimo ya watu wa Misri, mgao wa matumizi yake ulikuwa ukifanyika kwa amri ya Firauni. Na kwa maana hiyo, maisha ya watu yalikuwa kwenye mamlaka yake yeye na hilo likamfanya ajihisi kuwa yeye ndiye 'mungu' halisi wa Wamisri na hakuna maana yoyote ya kuwepo aliye juu zaidi yake yeye. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mataghuti na madola ya kiistikbari hayatumii akili na mantiki, bali yanajivunia nguvu, utajiri na hadhi yao ya kidhahiri; na kuvitumia hivyo kama hoja ya kuonyesha kuwa wao ndio walio katika haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kujivuna na kujifakharisha; na kuwadunisha watu kwa sababu ya aina ya mavazi na wanavyoonekana dhahiri yao au kwa sababu ya lahaja na uzungumzaji wao ni kuwa na hulka ya kifirauni. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, yeyote anayejiona bora kuliko wenzake kwa sababu yoyote ile, ajijue kuwa ana hulka na silika ya ufirauni, hata kama hatokuwa na mali wala madaraka.
Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 54 hadi 56 ambazo zinasema:
فَاسْتَخَفَّ قَوْمَهُ فَأَطَاعُوهُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ
Basi aliwachezea watu wake, na wakamt'ii. Kwa hakika hao walikuwa watu mafasiki.
فَلَمَّا آسَفُونَا انتَقَمْنَا مِنْهُمْ فَأَغْرَقْنَاهُمْ أَجْمَعِينَ
Walipo tukasirisha tuliwapatiliza tukawagharikisha wote!
فَجَعَلْنَاهُمْ سَلَفًا وَمَثَلًا لِّلْآخِرِينَ
Kisha tukawafanya kuwa watangulizi na mfano kwa wa baadaye.
Kwa hakika, kwa kitendo chake Firauni cha kujitukuza yeye mwenyewe na mamlaka aliyokuwa nayo na kujaribu kumdunisha Nabii Musa (as), aliipoteza kaumu yake kwa kutowapa fursa watu wake watumie akili zao ili kuweza kuifahamu haki na ukweli. Aliitia ujingani kaumu yake na kuipumbaza kwa mapambo na marembo, kiasi cha kuwafanya watu wake wote duni na dhalili mbele yake. Na kwa hivyo wakawa wanamtii na kumfuata bila kuuliza wala kuhoji chochote. Na hii, bila shaka, ndio njia na mbinu inayotumiwa na tawala zote ovu na za kijabari; yaani, ili kuweza kuendeleza utaghuti wao, huwatia uzuzu na upofu watu wao, wakawa hawajui kinachoendelea; na hivyo badala ya thamani za kweli na mambo ya maana, wakaamini na kuyakubali mambo ya kipuuzi na yasiyo na maana yoyote. Na sababu ni kwamba, kuzinduka wananchi na kupevuka kwao kiutambuzi na kifikra, ndio hatari kubwa zaidi kwa tawala za kiimla na kidikteta. Katika zama zetu hizi pia, madola ya kiistikbari, hutumia kanali za satalaiti, redio, televisheni, intaneti na vyombo vingine vya mawasiliano ili kuziteka akili na fikra za watu wa mataifa ya dunia na kuzijaza kasumba kuhusiana na ukweli wa mambo ili watu wabaki ujingani na kuendelea kuyatii madola hayo. Hawatoi mwanya kwa watu watambue na kubaini ukweli wa mambo, ili waweze kuendelea kuwatawala bila tabu wala shida yoyote. Lakini tueleze pia kwamba, katika zama za Firauni, watu wenyewe pia walikuwa wakosa. Kwa sababu, kwa jinsi maovu na ufuska ulivyokuwa umezagaa baina yao, ilikuwa rahisi kwao kumtii na kufuata mambo aliyowapumbazia; na kimsingi walijichimbia wenyewe kisima cha upotofu. Na ndiyo sababu iliyowafanya wasiwe na utayari wa kuyakubali maneno ya haki ya Nabii Musa (as). Ilivyo ni kwamba, watu wanaoamua kumfuata Firauni na tawala za Kifirauni, nao pia hupatwa na hatima sawa na ya mafirauni ya kufikwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na hakuna shaka pia kwamba, yaliyojiri katika maisha ya Firauni na wafuasi wa Firauni na hatima ya kutisha iliyowafika, ni somo la kutoa ibra na mazingatio kwa watu wa baada yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tawala mbovu na ovu, huwadunisha watu wao na kuwafanya dhaifu. Katika tawala hizo za kidhalimu, kutojithamini watu wenyewe na kupoteza utambulisho wao huwafanya wasalimu amri mbele ya watawala wao na kuwatii. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, jamii isiyomtii Mwenyezi Mungu, mwisho wake huishia kuwatii na kuwafuata watawala madhalimu na wenye kutakabari. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, baadhi ya wakati, ghadhabu na adhabu ya Allah huishukia kaumu ya watu wakaangamizwa papa hapa duniani ili wawe somo la kutoa ibra na mazingitio kwa wengine. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 903 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/