May 24, 2023 17:10 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 915. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 44 ya Ad-Dukhan, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 45 ya Al-Jaathiya. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya kwanza hadi ya tatu ya sura hiyo ambazo zinasema:

حم

H'a Mim.

تَنزِيلُ الْكِتَابِ مِنَ اللَّهِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ

Uteremsho wa Kitabu umetoka kwa Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

إِنَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّلْمُؤْمِنِينَ

Hakika katika mbingu na ardhi kuna Ishara kwa Waumini.

Suratul Jaathiya iliteremshwa Makka; na kama zilivyo sura nyingine za Makka, aya zake zimegusia hoja za tauhidi, maonyo kwa watu waliopotoka na hatima yao itakavyokuwa Siku ya Kiyama. Aya ya mwanzo ya sura hii imeanza kwa herufi za mkato za Haa Miim. Kwa kuzingatia aya ya baada yake, ambayo kumezungumziwa ndani yake kuteremshwa kwa Qur’ani na Mwenyezi Mungu Mtukufu, hilo linabainisha muujiza wa Qur’ani ambayo maandiko yake yametokana na herufi hizi hizi zinazojulikana, za alfabeti za Kiarabu; ikimaanisha kwamba, japokuwa watu wote wanazitumia herufi hizo lakini hakuna hata mtu mmoja awezaye kuleta japo sura moja tu iliyo mfano wa Qur’ani. Kuteremshwa kwa Qur’ani kumenasibishwa pia na sifa mbili za Mwenyezi Mungu, za izza na hekima. Kwa kuzingatia sifa hizo, Allah SWT anawataka waumini nao pia wawe daima wanalinda izza na heshima yao na wasikubali madhila kwa hali na namna yoyote ile. Halikadhalika, waendeshe mambo yao kwa akili na hekima na waache kufanya mambo kilegelege na bila umakini na uthabiti. Aya zinazofuatia zinazungumzia ishara za adhama ya Mwenyezi Mungu katika ulimwengu na kutanabahisha juu ya nukta moja muhimu ya kwamba, aliyeiteremsha hii Qur’ani ndiye huyohuyo aliyeumba mbingu na ardhi; na hukumu na maamrisho yake yaliyomo ndani ya Qur’ani yanaendana na kuwiana na mfumo wa uumbaji wa dunia na mwanadamu. Kwa hivyo waumini, si tu wanazingatia aya za kitabu hicho cha mbinguni, lakini wanaziangalia pia kwa makini mbingu na ardhi ili kuona na kubainikiwa na ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu, kunakozifanya imara na thabiti imani zao. Adhama ya mbingu na mfumo wake wa kustaajabisha pamoja na umbo la ardhi na maajabu yake, kila kimoja ni ishara mojawapo za Mwenyezi Mungu. Sayari ya dunia iko kwenye mwendo wenye nidhamu na hisabu maalumu. Sayari hii inajizunguka yenyewe na kulizunguka jua pia kupitia njia makhsusi iliyowekewa. Na kwa kufuatana na maumbo mengine ya mfumo wa jua na sayari zake, sayari hii inaendelea na safari yake isiyo na kikomo kupitia kwenye mzingo ilioainishiwa. Pamoja na hayo, mwenendo huo ni wa taratibu mno, kiasi kwamba hauwanyimi raha na utulivu wanadamu na viumbe hai vingine vyote, wala kuwafanya wakazi wa sayari hii ya dunia wahisi mtikisiko wowote wa mwendo huo. Katika ardhi hii zimejazwa aina kwa aina za maliasili, madini na vitu vingine vya mahitaji ya maisha kwa ajili ya mabilioni ya wanadamu wanaoishi ndani yake. Milima na bahari, nazo pia ni katika ishara za Mwenyezi Mungu. Kwa hakika mbingu na ardhi zina uzuri wa kuvutia unaomteka na kumstaajabisha mwanadamu. Na bila shaka kwa waumini na wapendao kuijua haki, wao hawavipiti vivi hivi tu vitu hivyo, bali wanatafakari katika ishara hizo, adhama na uwezo wa Mola Muumba. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur’ani, ambacho ni kitabu cha sheria za Allah za kumpatia maisha ya saada na fanaka mwanadamu, imeteremshwa kwa msingi wa ujuzi na hekima yake Mola isiyo na ukomo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mifumo ya sharia na uumbaji imetokana na chimbuko na asili moja na kuna mlingano, uratibu na uwiyano kamili baina yao. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kwamba, aya za Kitabu cha Allah na vilevile kurasa za kitabu cha ulimwengu wa maumbile, vyote hivyo ni alama na ishara kwa waumini.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya nne hadi ya sita ambazo zinasema:

وَفِي خَلْقِكُمْ وَمَا يَبُثُّ مِن دَابَّةٍ آيَاتٌ لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ

Na katika kuumbwa kwenu na katika wanyama alio watawanya zimo Ishara kwa watu wenye yakini.

 

Na kupishana usiku na mchana, na riziki anayo iteremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni, na kwayo akaifufua ardhi baada ya kufa kwake, na mabadiliko ya upepo, ni Ishara kwa watu wenye akili.

تِلْكَ آيَاتُ اللَّهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ ۖ فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَ اللَّهِ وَآيَاتِهِ يُؤْمِنُونَ

Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki; basi hadithi gani watakayo iamini baada ya Mwenyezi Mungu na Aya zake?

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia ishara za Mwenyezi Mungu katika ulimwengu, aya hizi, kwanza zinawatanabahisha watu kwa kuwauliza: kwa nini hamutafakari juu ya kuumbwa kwenu ili muweze kubaini adhama ya aliyofanya Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mwanadamu? Kwa nini hamutafakari juu ya uumbaji wa anuai za wanyama mnaoishi pamoja nao katika sayari hii ya dunia? Hali ya kuwa kuyazingatia na kuyatafakari mambo hayo ni chanzo cha kupata yakini ya kuwepo kwa Mungu mmoja tu na wa pekee. Ni kama ilivyo pia kwa vitu vingine vya kimaumbile, kama upepo, mvua na kuchomoza na kuzama kwa jua, ambavyo kama mtavitafakari, mtabaini kuwa Muumba wa ulimwengu ameyapanga na kuyaendesha mambo yote hayo ili yakidhi mahitaji ya kimaumbile ya wakazi wa sayari ya dunia na kuwafanya waweze kuendelea kuishi katika sayari hiyo. Kama kuna watu ambao hawakai wakatafakari juu ya ishara zote hizi zisizoweza kuhesabika na hawako tayari kuzingatia na kuyaamini aliyoteremshiwa Mtume, tatizo litakuwa ni wao wenyewe; ama kwa upande wa ishara na aya za Mwenyezi Mungu katika kitabu cha ulimwengu wa maumbile na ndani ya Qur’ani, hizo ziko wazi kabisa na wadhiha, kiasi kwamba, kama mtu atazitafakari kidogo tu zitamfikisha kwenye imani na yakini juu ya Mola Muumba. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wahyi wa Mwenyezi Mungu unatutaka tutafakari na kutumia akili zetu, ili imani zetu kwa Yeye Mola zitokane na maarifa na utambuzi; na kwa njia hiyo kuifikia yakini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, tusivitazame kama mambo yatokeayo kwa sadfa tu vitu vya kimaumbile, kama mawingu, upepo, mvua na theluji. Ikiwa vitu hivyo vya kimaumbile havitatokea kwa kufuata nidhamu na utaratibu maalumu viliowekewa, wanadamu na viumbe vingine hai wataangamia na kutoweka kwa njaa na ukame katika sayari hii ya dunia. Halikadhalika, aya hizi zinatuelimisha kwamba, Mwenyezi Mungu ametimiza dhima yake kwa watu kwa kuwateremshia Vitabu vya mbinguni; kwa hivyo wale wasioamini, hawatakuwa na udhuru wala kisingizio chochote cha kutoa.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya saba na ya nane ya sura yetu ya Al-Jaathiya ambazo zinasema:

وَيْلٌ لِّكُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ

Ole wake kila mtunga uongo mwenye dhambi!

يَسْمَعُ آيَاتِ اللَّهِ تُتْلَىٰ عَلَيْهِ ثُمَّ يُصِرُّ مُسْتَكْبِرًا كَأَن لَّمْ يَسْمَعْهَا ۖ فَبَشِّرْهُ بِعَذَابٍ أَلِيمٍ

Anaye sikia Aya za Mwenyezi Mungu akisomewa, kisha anashikilia (aliyo katazwa), na anajivuna, kama kwamba hakuzisikia. Basi mbashirie adhabu iumizayo!

Katika aya zilizotangulia zimegusiwa baadhi ya ishara za Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ulimwengu wa uumbaji na pia kuteremshwa Qur’ani na Yeye Mola aliyetukuka. Aya tulizosoma zinasema: watu wasiomwamini Mwenyezi Mungu, Mtume wake na Vitabu vyake vya mbinguni ni wale wafanyao madhambi na ufisadi kutokana na hawaa na matamanio ya nafsi zao; na nyoyo zao haziko tayari kuikubali haki. Kwa hiyo vyovyote vile watakavyosomewa aya za Mwenyezi Mungu, hawako tayari kuzisikiliza na kuzitafakari. Ni sawa kabisa na mtu aliyejifanya amelala, ambaye hata tukimwita mara ngapi, huwa kama hatusikii. Ni wazi kwamba mtu kama huyo anastahiki adhabu kutokana na kutakabari kwake mbele ya haki na kufanya aina kwa aina za maovu na maasi. Na atayaona hapa duniani na huko akhera malipo ya mabaya aliyofanya. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tunatakiwa tuyafikishe maneno ya Mwenyezi Mungu kwa watu wote, hata wale walioghariki kwenye dimbwi la madhambi na ufisadi ili kuondoa dhima juu yao. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kiburi ni kitu kibaya, lakini ni kibaya na kiovu zaidi kumfanyia Mwenyezi Mungu, Mola Muumba; na lililo baya na ovu zaidi ya hilo ni mtu kushupalia na kuendeleza kiburi chake hicho. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 915 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuzidishie utambuzi juu ya ishara na adhama yake utakaozipa uthabiti imani zetu; na azitakase na kila maradhi machafu ya kiroho yakiwemo ya kiburi, nyoyo na nafsi zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/