May 24, 2023 17:15 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 916 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 45 ya Al-Jaathiya. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 9 hadi 11 ya sura hiyo ambazo zinasema:

وَإِذَا عَلِمَ مِنْ آيَاتِنَا شَيْئًا اتَّخَذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ

Na anapo kijua kitu kidogo katika Aya zetu hukifanyia mzaha. Hao ndio watakao kuwa na adhabu idhalilishayo.

مِّن وَرَائِهِمْ جَهَنَّمُ ۖ وَلَا يُغْنِي عَنْهُم مَّا كَسَبُوا شَيْئًا وَلَا مَا اتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّهِ أَوْلِيَاءَ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ

Nyuma yao ipo Jahannamu. Na waliyo yachuma hayatawafaa kitu, wala walinzi walio washika badala ya Mwenyezi Mungu. Na watapata adhabu kubwa.

هَٰذَا هُدًى ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ لَهُمْ عَذَابٌ مِّن رِّجْزٍ أَلِيمٌ

Huu ni uwongofu. Na wale walio zikataa Ishara za Mola wao Mlezi watapata adhabu yenye maumivu iumizayo.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia watu ambao wamezisikia na kuzielewa aya za Mwenyezi Mungu lakini hawako tayari kuzikubali kutokana na kiburi na ukaidi na wanaendelea kuzipinga na kuzikadhibisha. Aya tulizosoma zinasema: watu hao si tu wamezisikia na wakazifahamu lakini hawakuwa tayari kuzikubali aya za Mwenyezi Mungu, lakini wanazifanyia istihzai pia na vilevile wanamfanyia dharau Mtume na waumini. Kwa sababu hiyo, Allah atawadhalilisha na kuwadunisha watu hao duniani na akhera. Siku ya Kiyama, mali na utajiri wa wale waliokuwa wakiwaendea na kuwategemea badala ya Mwenyezi Mungu hazitawafalia kitu. Hapo ndipo wataelewa uduni na udhalili wao na watapatwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu wakibaki peke yao bila ya kuwa na pa kukimbilia. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, hii Qur'ani ni chemchem ya uongofu, kipambanuzi cha baina ya haki na batili, inamtandikia mwanadamu njia safi na sahihi ya maisha na inawafikisha wafuataji wa njia ya haki kule walikokusudiwa kufika. Lakini kwa wale walioamua kukadhibisha aya na ishara za Mola wao, hatima na mwisho wao ni kufikwa na adhabu kali na yenye kuumiza. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, adhabu za Siku ya Kiyama zitalingana na aina ya dhambi aliyofanya mtu. Na ndio maana malipo ya wafanyao shere na stihzai yatakuwa pia ya kuwadunisha na kuwadhalilisha wao pia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hapa duniani makafiri wanajivunia na kutegemea utajiri, nguvu na madaraka ya marafiki na washirika wao, lakini Siku ya Kiyama, hakuna lolote kati ya hayo litakalowafaa na kuwasaidia. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, yeyote aamuaye kuupa mgongo uongofu wa Mwenyezi Mungu atajichafua kwa maovu na machafu, yatakayomfanya afikwe na adhabu na mateso Siku ya Kiyama.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 12 na 13 za sura yetu ya Al-Jaathiya ambazo zinasema:

اللَّهُ الَّذِي سَخَّرَ لَكُمُ الْبَحْرَ لِتَجْرِيَ الْفُلْكُ فِيهِ بِأَمْرِهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

Mwenyezi Mungu ndiye aliyekutiishieni bahari, ili humo zipite marikebu kwa amri yake, na ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru. 

وَسَخَّرَ لَكُم مَّا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مِّنْهُ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

Na amekutiishieni vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, vyote vimetoka kwake. Bila shaka katika hayo zimo Ishara kwa watu wanao tafakari.

Aya hizi zinagusia ishara nyingine ya tauhidi katika ulimwengu wa maumbile kwa kueleza kwamba: nyinyi huwa mnapanda marikebu na majahazi na kutumia njia ya bahari ili kusafiri kwenda pande mbalimbali za dunia kwa ajili ya biashara. Hali ya kuwa kinachokurahisishieni safari zenu hizo ni mazingira na hali maalumu ya maumbile ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia kuwa nayo maji, ili pale marikebu na mameli makubwa makubwa yaliyosheheni mizigo na abiria yanapokata mawimbi, yasizame na kughariki; na nyinyi muweze kufika salama usalimini huko mnakoelekea. Mnadhani ni nani aliyeyafanya maji yawe mithili ya tandiko laini na barabara tambarare ya kuzifanya meli zikate masafa juu yake bila tabu kuelekea upande huu na ule ziutakao? Au ni nani aliyejaalia pepo kuvuma baharini kutoka upande mmoja kuelekea upande mwingine na kuwezesha marikebu na majahazi kukata masafa majini? Ajabu ni kwamba licha ya maendeleo yote aliyofikia mwanadamu wa leo ya kuweza kuunda na kutengeza vyombo mbalimbali vya kisasa vya uchukuzi na usafirishaji kama gari, ndege na treni, sehemu kubwa ya kazi ya usafirishaji mizigo na bidhaa duniani inaendelea kufanywa na meli na kwa kutumia njia za baharini. Njia ambazo hazihitaji kujengwa, kutunzwa wala kufanyiwa ukarabati, bali huweza kutumiwa muda wote na kwa urahisi. Na si bahari peke yake, bali vitu vingine vyote vya maumbile vilivyoko angani na ardhini, kama jua na mwezi, mvua na upepo, madini na anuai za maliasili za ardhini, misitu na majangwa pamoja na milima na mabonde, vyote hivyo ameviumba Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wanadamu na kwa manufaa yao. Neema na atiya zote hizo zinatoka kwake Yeye Allah SWT na ametuandalia mazingira ya namna ya kufaidika na kunufaika na kila aina ya neema alizotujaalia. Hapana shaka kutiishiwa mwanadamu ulimwengu huu ni mojawapo ya ishara na alama za Mwenyezi Mungu kwa watu wenye kufikiri na kutafakari. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Mwenyezi Mungu ameuumba ulimwengu wote kwa ajili ya mwanadamu ili avitumie vilivyomo ndani yake kwa manufaa yake, lakini kiumbe huyo hayuko tayari hata kuonyesha ushukurivu kwa Mola wake kwa neema zote hizo alizopewa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kujituma na kufanya juhudi za kutafuta riziki ili kujikimu kimahitaji ni jambo linalohimizwa na dini tukufu ya Uislamu; na wala hakuna mgongano wa kuishi maisha mazuri duniani na kuweza kushika dini pia kama inavyotakiwa. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kutafakari katika uumbwaji wa vitu mbalimbali vya maumbile kunatufikisha kwa Mwenyezi Mungu na kutufanya tuwe na imani ya tauhidi itokanayo na elimu na uelewa.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 14 ambayo inasema:

قُل لِّلَّذِينَ آمَنُوا يَغْفِرُوا لِلَّذِينَ لَا يَرْجُونَ أَيَّامَ اللَّهِ لِيَجْزِيَ قَوْمًا بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ

Waambie walio amini wawasamehe wale wasio zitaraji siku za Mwenyezi Mungu, ili awalipe watu kwa waliyo kuwa wakiyachuma.

Kuhusu kutakabari makafiri mbele ya aya za Mwenyezi Mungu na kukazania kufuata itikadi batili na imani zao potofu, aya hii inawahutubu waumini ya kwamba: msibishane na kujibizana na watu wasioamini Siku ya Kiyama. Mwachieni Mwenyezi Mungu watu hao, Yeye Mola atajua vya kuamiliana nao na kuwapa adhabu ya kutakabari kwao. Ama kuhusu watu ambao ukafiri wao unatokana na ujinga na kutojua, wanaofanya shirki na kumkufuru Allah kwa sababu ya ujahili, hao inapasa muamiliane nao kiuungwana na kwa uvumilivu ili kuamiliana nao kwa vishindo na ukali kusije kukawafanya wazidi kuwa mbali na haki. Inawezekana mlahaka wa kuamiliana nao kwa wema na uchukulivu ukawa sababu ya wao kuzinduka, wakatoka kwenye mghafala wa ujinga walionao na kuamua hatimaye kuikubali dini ya haki. Lakini kwa upande wa makafiri ambao wanaamua kwa makusudi na kwa inadi na ukaidi kuikataa haki, kuacha kubishana na kujadiliana nao ni aina mojawapo ya njia ya kuwapuuza na kuwaacha kama walivyo. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mbinu ya kuamiliana na kukabiliana na wapinzani hutofautiana kwa kuzingatia hali na mazingira yao na pia hali ya waumini. Kuna wakati huwa inapasa kusimama imara na kukabiliana nao; na wakati mwingine inatakiwa tuwaache kama walivyo na kumwachia Allah mwenyewe. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, adhabu ya Mwenyezi Mungu inalingana na amali zetu. Na amali zenyewe ni zile zilizokuwa ndio njia na mwenendo wetu na ambazo ndizo tunazoshikilia kuzifanya kila mara na kila siku katika maisha yetu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 916 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuwezeshe kuwa wafanya tablighi na wafikishaji wazuri wa ujumbe wa dini yake tukufu kwa watu, tutakaowavutia wengi kuufahamu na kuufuata Uislamu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/