Hikma za Nahjul Balagha (23)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 23 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 23.
مَنْ أَبْطَأَ بِهِ عَمَلُهُ لَمْ یُسْرِعْ بِهِ [حَسَبُهُ] نَسَبُهُ
Mtu ambaye matendo yake hayamfikishi popote, asitarajie heshima ya familia yake itamfikisha popote.
Inapendeza mtu kuwa na familia, na kuwa mtoto wa mtu mwenye ustaarabu au shujaa wa mashujaa, au mwanasayansi bora na watu wenye sifa aali na nzuri. Historia imejaa watoto ambao walichukua sifa nzuri za baba na wazazi wao kwa ustahiki mkubwa na kuziendeleza. Lakini ni hivyo hivyo, historia imejaa watoto ambao wameshindwa kurithi sifa nzuri za wazazi wao. Wako watoto ambao licha ya kuwa na wazazi mashuhuri, wanaoheshimika na wastaarabu, lakini hufuata njia mbaya na hawajidhuru wao wenyewe tu, bali pia huwaletea madhara wazazi wao. Watoto kama hao huweka chini ya alama ya kuuliza si itibari yao binafsi tu, bali pia itibari ya wazazi wao. Kwa sababu mara nyingi, watu wa kawaida huwa hawana uchanganuzi sahihi wa mambo na husema vipi mwanachuoni mkubwa kama huyo na umaarufu wake wote, ameshindwa kumlea vizuri mwanawe na amemwacha amekuwa hivi? Watu hao huwa hawazingatii ukweli kwamba Qur'ani Tukufu inataja kisa cha Mtume mtukufu na mkubwa sana kama Nabii Nuh AS lakini ona mtoto wake alikuwa miongoni mwa makafiri na aliangamia kwenye ile gharika kubwa.
Imam Ali AS katika hikma ya ishirini na tatu, anaashiria umuhimu wa matendo mema ya mtu mwenyewe katika kuainisha hatima yake na anasema kwamba, wale watu ambao wanasubiri nasaba zao ziwaainishie mustakbali wao, wanafanya kosa. Anasema wazi kuwa, mtu ambaye matendo yake hayakumsaidia, asitarajie heshima na itibari ya familia yake kuwa itamsaidia.
Kwa hakika, maneno ya Imam Ali AS katika hikma hii ya 23 ni muhimu na ni ya kuzingatiwa sana. Ni hikma inayotushajiisha na kutuhamasisha kujipinda kutenda mambo mema na inatuamsha ili tuwe makini sana katika matendo yetu kwenye maisha yetu ya kila siku. Ni sawa kabisa na wakati Bwana Mtume SAW alipowakusanya jamaa zake na kuwaambia: Enyi watoto wa Abdul Muttalib, Enyi watoto wa Hashim, Enyi watoto wa Abdul Manaf, na wewe, binti yangu; Fatimah, ingawa mimi ni Mtume wa Allah, lakini kuwa kwangu hivyo hakuwezi kukusaidia chochote kama mwenyewe hukujipinda kwa ibada. Kuwepo kwangu hakuwezi kukufanya usimuhitajie Mwenyezi Mungu. Kitu kinachomfurahisha Mwenyezi Mungu ni matendo na amali njema.
Mwanadamu katika dunia hii ni msafiri anayetoka katika ulimwengu wa kimaada kuelekea ulimwengu wa Akhera. Masurufu, chombo na njia za harakati na safari yake hiyo si chochote ila ni matendo mema. Katika safari yake hiyo, mwanadamu lazima awe na mbawa mbili, moja ya ilmu na nyingine ya matendo. Moja ya mbawa hizo inapokatika, hupelekea kufeli kupaa mwanadamu katika safari yake hiyo. Au tuseme kwa maneno ya wazi zaidi kwamba, mtu anaposhindwa kuwa na matendo mazuri, si tu hawezi kufikia anakokwenda, lakini huporomoka kwenye udhalili wa chini kabisa wa mambo ya kimaada na kidunia. Kwa kuzingatia hayo tutaona kuwa nasaba ya mtu bila ya matendo mazuri haiwezi kumpandisha kwenye daraja za juu za mja mwema. Ni kwa sababu hiyo ndio maana aya ya 13 ya Surat al Hujurat ikasema: Hakika mbora wenu mbele ya Allah ni yule anayemcha zaidi Mwenyezi Mungu. Naam, nasaba na umashuhuri wa familia hauwezi kumfikisha popote bali matendo yake mazuri ndiyo yanayoweza kumnyanyua.