Sura ya Qaaf, aya ya 31-37 (Darsa ya 952)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 952 na sura tunayoizungumzia kwa sasa ni ya 50 ya Qaaf. Tunaianza darsa yetu ya leo kwa aya yake ya 31 na 32 ambazo zinasema:
وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ غَيْرَ بَعِيدٍ
Na Pepo italetwa karibu kwa ajili ya wachamngu, haitakuwa mbali (nao).
هَٰذَا مَا تُوعَدُونَ لِكُلِّ أَوَّابٍ حَفِيظٍ
Haya ndiyo mnayo ahidiwa kwa kila aelekeaye (kwa Mwenyezi Mungu na) ajilindaye.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizoelezea hatima ya watu ambao hawakuiamini na wakaikataa haki kutokana na inadi na ukaidi. Mkabala na watu hao, aya tulizosoma zinaashiria mwisho mwema wa walioamini na kueleza kwamba: Siku ya Kiyama, Pepo itaandaliwa na kuwekwa tayari kwa ajili ya waja wema waliomcha Mwenyezi Mungu ili waweze kuneemeka na kustareheshwa kwa neema zisizo na ukomo za Mola Karima. Malipo hayo adhimu na makubwa kabisa ni matunda ya namna walivyojichunga katika kutekeleza maamrisho ya Allah SWT hapa duniani, wakajihadhari na kumuasi Yeye Mola. Na hata ilipowatokezea kuteleza na kufanya makosa kwa sababu ya ujinga na mghafala, walizinduka na kutubia haraka kwa makosa yao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, muumini, kama alivyo kafiri, hakingiki wala hatakasiki na madhambi; lakini kinyume na alivyo kafiri, yeye huwa hakazanii wala hashupalii kufanya madhambi; na pale anapoteleza kwa kufanya kosa au dhambi hujuta haraka na kuifidia kwa toba. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kama tuna imani ya kweli juu ya ahadi za Mwenyezi Mungu, basi tuwe na uhakika kwamba taqwa, toba na kujitakasa na maasi vitatufikisha kwenye Pepo ya milele ya Mola.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 33, 34 na 35 ambazo zinasema:
مَّنْ خَشِيَ الرَّحْمَٰنَ بِالْغَيْبِ وَجَاءَ بِقَلْبٍ مُّنِيبٍ
Mwenye kumwogopa Mwingi wa Rehema katika faragha, na akaja kwa moyo ulio elekea.
ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ ۖ ذَٰلِكَ يَوْمُ الْخُلُودِ
(Wataambiwa) ingieni (Peponi) kwa salama. Hiyo ndiyo siku ya daima dawamu.
لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ
Humo watapata wakitakacho, na kwetu yako ya ziada.
Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa na aya zilizotangulia na kueleza kwamba: alama ya imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu, ni mtu kumkhofu na kumcha Yeye Mola kwa kutofanya dhambi hadharani na faraghani pale anapokuwa haonekani na yeyote ghairi ya Yeye Allah SWT; na kama atateleza na kufanya maasi, akatubia na kuomba maghufira haraka. Kuwa na moyo na nafsi kama hiyo ndiko kunakomuepusha mtu na adhabu ya Moto na kumuingiza kwenye Pepo ambayo ataishi ndani yake milele. Wale ambao hapa duniani walijikhini na vile zilivyotamani nafsi zao kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu, Mola Mwenyezi atawafidia kwa kuwalipa Pepo huko Akhera na wataambiwa: Sasa hivi mumeshaandaliwa kila mtakacho, kinachozipendeza na kuzifurahisha nafsi zenu. Lakini mbali ya hayo, Allah TWT atakupeni pia kwa fadhila na ukarimu wake neema ambazo hata nyinyi wenyewe hamzijui na hamjafikiria kuziomba. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, nyoyo za waumini zina sifa ya kutubia na kumrejea Allah kumuomba maghufira; na hilo ndilo litakalowafanya wapate nusra na uokovu. Lakini nyoyo za makafiri na wanafiki zina maradhi ya kutetea na kuhalalisha maovu na madhambi wanayofanya; na kwa hivyo hazitaokoka. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuacha na kujizuia kufanya dhambi hadharani na mbele ya macho ya watu si alama ya kuamini kikweli, kwa sababu yumkini mtu akafanya hivyo kwa kuhofu kuchukuliwa hatua za kisheria, kulaumiwa na wenzake au kuadhirika na kupoteza heshima yake. Lakini kama tutamkhofu Mwenyezi Mungu faraghani na kuchunga heshima na mipaka yake Mola, hiyo itakuwa alama ya kuwa na imani ya kweli ya kumwamini Yeye Mola. Aidha, aya hizi zinatutaka tufahamu kwamba, wakati waja wema watakapoingizwa Peponi, watalakiwa na kukaribishwa kwa mapokezi na maamkizi maalumu. Vilevile aya hizi zinatuonyesha kuwa, huko Peponi hakutakuwako na mipaka na ukomo au tabu na usumbufu wa kuzipata neema za Allah SWT; na katika bishara bora zaidi wanayopewa watu wa Peponi ni kustareheshwa na kuneemeshwa kwa neema za milele na zisizomalizika. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujue kwamba, mwanadamu ni kiumbe chenye sifa ya kupenda mambo bila ya kikomo. Kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu atawapa waja wake wema wa Peponi, zaidi ya yale watakayotaka na watakayoyatarajia.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 36 na 37 za sura yetu ya Qaaf ambazo zinasema:
وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هُمْ أَشَدُّ مِنْهُم بَطْشًا فَنَقَّبُوا فِي الْبِلَادِ هَلْ مِن مَّحِيصٍ
Na uma ngapi tuliziangamiza kabla yao walio kuwa na nguvu zaidi kuliko wao! Nao walikuwa na satua katika miji. Je! Walipata pa kukimbilia?
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ
Hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au ategaye sikio, naye mwenyewe awe hadhiri.
Aya hizi ni onyo na indhari kwa madhalimu wote kwamba wasidhani kama nguvu, uwezo na mamlaka waliyonayo yanaweza kuzuia kuthibiti lile alitakalo Allah Jalla Jalaaluh na kwamba wataweza kuiepuka adhabu na ikabu ya Mola. Kwani katika historia, walikuwepo watawala majabari chungu nzima waliokuwa na satua, na ambao walitawala na kuyahodhi maeneo ya kila pembe ya dunia, lakini mwishowe walitiwa mkononi na Allah wakahilikishwa na kuangamizwa. Ni wazi kwamba watu wanaopata mafunzo, ibra na mazingatio kutokana na yaliyozisibu kaumu zilizopita ni wale ambao, kwa kuitalii na kuisoma historia ya watu wa kaumu hizo huuhakiki na kuuchambua mwenendo, matendo na yaliyowafika watu hao, na kwa njia hiyo kubaini sababu za kuporomoka na kuangamizwa kwao. Au kama si kufanya hivyo, basi angalau kuwasikiliza walio wajuzi wa kuchambua matukio ya kihistoria; na kutokana na mafunzo watakayopata, wakaacha ukafiri, dhulma na uchupaji mipaka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuzifahamu sababu za kuporomoka na kutoweka staarabu kubwa kubwa zilizokuwepo duniani, inapasa kutumiwe kama mwenge wa kuangazia na kuongozea njia kwa vizazi vya sasa na vya baadaye. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mojawapo ya kanuni za kudumu za Allah ni kuziangamiza umma na watawala majabari na madhalimu. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, utawala na madaraka ni kichocheo cha dhulma na ufisadi na chachu ya kuasi, kuchupa mipaka na kuwaonea watu, isipokuwa tu kama kutakuwepo na nguvu ya imani itakayomdhibiti na kumzuia mtu asiwafanyie dhulma na uonevu wanadamu wenzake. Vilevile aya hizi zinatuonyesha kuwa, kusoma na kutalii tu historia za waliotangulia, hakutoshi kwa ajili ya kufuzu na kuokoka; bali inapasa tuwe na utambuzi pia wa matukio na mabadiliko ya kihistoria na kanuni zilizopelekea kujiri matukio na mabadiliko hayo. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 952 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamuomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake watakaorithishwa Pepo ya milele kwa fadhila zake na kuepushwa na hilaki ya Moto wa Jahannamu kwa rehma zake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/