Jul 06, 2024 13:04 UTC
  • Kuomba radhi kwa kuchelewa Kanisa Katoliki

Makala yetu ya juma hili imeangazia kuomba radhi Kanisa Katoliki kutokana na jinai zilizofanywa dhidi ya wakazi asilia wa Marekani.

Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Marekani hivi karibuni waliwaomba radhi wazawa na wakazi asili wa nchi hiyo kwa madhara yaliyosababishwa na kanisa hilo katika kwa jamii ya wakazi asili wa nchi hiyo. 

Kufichuliwa vitendo vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto wa wakazi asili katika shule za bweni za Marekani zinazosimamiwa na Kanisa Katoliki kumegonga vichwa vya habari katika pembe mbalimbali za dunia. Mmoja wa viongozi wa jamii ya watu asilia anayefuatilia kashfa hiyo huko Marekani ameeleza kuwa: Shule za bweni za watoto wa wakazi asilia zinajulikana kama eneo la uhalifu wa kitaifa. 

Serikali ya Shirikisho ya Marekani ilianzisha zaidi ya shule 500 za bweni za watoto wa jamii ya watu asilia kati ya mwaka 1819 na 1969 katika fremu ya juhudi za kuangamiza jamii za wazawa na wakazi asilia wa nchi hiyo na utamaduni wao. Marekani ilifanya hivyo lengo likiwa ni kuteka na kudhibiti ardhi za wazawa na kungamiza vizazi vya asili vya nchi hiyo. Uchunguzi wa gazeti la Washington Post unaonyesha namna shule hizo zilivyofungua njia kwa uhalifu wenye ugonjwa wa ngono.

Hadi sasa kumegunduliwa unyanyasaji wa kustaajabisha wa kingono dhidi ya watoto asilia katika shule za bweni za Marekani. Makumi ya maelfu ya  watoto hao kuanzia mwaka 1819 hadi 1969 walipelekwa katika shule za bweni za Marekani baada ya kutenganishwa kwa lazima na familia zao. 

Idadi kubwa kati ya shule 500 za bweni za watoto asilia ziilikuwa zikifadhiliwa na serikali ya Marekani, na kimsingi, lengo lilikuwa kuangamiza utamaduni wa wazawa na wakazi asili wa Marekani. Mienendo na hatua za shule hizi ziliwatesa na kuwabughudhi sana wenyeji wa Marekani. Hadi kufikia mwaka 1900 mtoto mmoja kati ya kila watoto 5 wa jamii asilia waliokuwa na umri wa kwenda shule huko Marekani alikuwa akisoma katika shule ya bweni za Kanisa Katoliki zilizofanyiliwa na serikali. 

Jinai na uhalifu uliofanywa katika shule za bweni hususan ule uliowalenga watoto wa jamii asilia nchini Marekani unatambuliwa kuwa kashfa ya taifa huko Marekani. Chunguzi nyingi zinaonyesha kuwa, kulikuwa na matatizo makubwa katika shule 80 za bweni zilizokuwa zikisimamiwa na Kanisa Katoliki; ambapo vitendo vya kuogofya vya unyanyasaji wa kingono kwa watoto vilifanyika kwa kiasi kikubwa. 

Utafiti uliofanywa na gazeti la Washington Post unaonyesha kuwa, wawakilishi wa Kanisa Katoliki wasiopungua 122 katika shule 22 za bweni wanatuhumiwa kuhusika moja kwa moja na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto wa wakazi asilia wa Marekani. 

Ilibainika pia kuwa, shule 18 kati ya hizo, kwa miaka mtawalia zilikuwa zimeajiri watu wanaotuhumiwa wenye mafaili ya kuhusika na unyanyasaji wa kingono katiika Kanisa Katoliki. 

Unyanyasaji mwingi wa kingono dhidi ya watoto katika shule za bweni za watoto wa jamii asilia nchini Marekani  ulifanyika katika miaka ya 1950 na 1960, na kuathiri zaidi ya watoto elfu moja waliotenganishwa na familia zao.

Katika miaka ya karibuni, chunguzi mbalimbali zilifanywa kuhusu vitendo walivyokumbana navyo watoto hao katika shule za bweni za Kanisa Katoliki huko Canada na Marekani baada ya kugunduliwa makaburi ya umati katika maeneo ya shule hizo. Inakadiriwa kuwa, idadi ya watoto wenyeji wa Marekani waliopoteza maisha katika shule za bweni za kanisa ni takriban 4,000. Kiwango cha kunyanyaswa kingono watoto hao katika shule hizo za Marekani kimeendelea kuwa kitendawili katika historia.  

Gazeti la Washington Post limeashiria uchunguzi wake katika uwanja huo na kuandika: "Wahanga wengi bado hawajaweka wazi mateso waliyokumbana nayo au hawajawahi kupewa fursa ya kueleza masaibuu yaliyowapa. Kasisi mmoja wa zamani wa Kikatoliki anakiri kwamba, alipokumbana na madai ya unyanyasaji wa kingono, alitambua kwamba shule hizo zilikuwa ardhi ya maajabu ya watenda jinai. Alisema: Wahanga wa unyanyasaji wa kingono katika shule za bweni za Marekani wanaweza kupiga kelele ya kuomba msaada, hata hivyo hakuna anayewasikiliza wala kuamini maneno yao." 

Kufichuliwa unyanyasaji mkubwa wa kingono dhidi ya watoto katika shule za bweni zinazosimamiwa na Kanisa Katoliki na wakati huohuo kubainika wazi namna kanisa hilo lililivyoficha kesi za wahanga kwa makusudi kumewashajiisha baadhi ya waathiriwa kuhisi kuwa wanaweza kueleza wazi kwa watu wengine masaibu na matatizo yao ya kinafsi.

Mmoja kati ya waathiriwa wa shule hizo za Kanisa Katoliki ambaye sasa ana umri wa miaka 77 anasema: "Nilisubiri kwa muda wa miaka 67 ili nisimulie hadithi yangu. Nilipelekwa shule iliyo umbali wa maili 700 kutoka nyumbani kwetu huko Alaska".

Wakili anayewatetea wahanga wa unyanyasaji wa kingono katika shule za bweni nchini Marekani amesema: Wahanga sasa wanasimulia jinai za Kanisa Katoliki kwa sababu yale yaliyofichuliwa huko nyuma yanaonyonesha kuwa wananchi wanaweza kupata majibu." 

Msemaji wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Marekani amedai kuhusiana na suala hili kwamba: Kanisa Katoliki linatambua suala la unyanyasaji wa kingono kwa watoto asilia na limekiri kwamba historia ya shule za bweni nchini humo inasababisha masikitiko makubwa. Amesema: "Tunatumai kuwa mazungumzo ya kweli na ya uaminifu yatapelekea kupatikana suluhu kati ya Kanisa Katoliki na jamii zilizoathiriwa. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani hivi karibuni liliwaomba radhi wazawa wa nchi hiyo kwa kuhusika  Kanisa Katoliki katika madhara yaliyoipata jamii ya wenyeji asilia. Uombaji radhi huo ni sehemu ya waraka ambao Maaskofu wa Kikatoliki nchini Marekani wameuidhinisha kwa kuupigia kura katika mkutano wao wa karibuni huko Louisville, Kentucky. 

Nukta muhimu ya kuashiria hapa ni kuwa, ubakaji na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto huko Marekani hauhusiani tu na miongo iliyopita, bali uhalifu huu unaendelea hadi sasa katika nchi hiyo. Baadhi ya nyaraka zilizotolewa na mwakilishi wa Kidemokrati wa Baraza la Wawakilishi la Marekani zinaonyesha kuwa, zaidi ya kesi 4,500 za unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto wahamiaji haramu zimesajiliwa katika vituo walikowekwa watoto hao nchini Marekani kati ya 2014 na 2019.

Ted Deutch, aliyekuwa mbunge wa Kidemokrati katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, ambaye alifichua nyaraka hizo mnamo 2019, anasema: Hati hizi zinaonyesha uwepo wa mazingira yaliyojaa unyanyasaji wa kingono wa kupangwa unaofanywa na wafanyikazi wa vituo hivyo dhidi ya watoto wahamiaji.

Tags