Apr 29, 2017 12:53 UTC
  • Imam Hussein AS, kigezo bora kwa wapigania ukombozi

Tarehe tatu Shaaban ni kumbukumbu ya kuzaliwa shakhsia mkubwa ambaye aliyapa maana kamili maneno ya umaridadi na mapenzi. Ana moyo maridadi, karama, maarifa ya kina na hatimaye yeye ni kielelezo cha maisha ya mwanaadamu aliyekamilika. Leo ni siku ambayo mji wa Madina ulishuhudia kuzaliwa, Hussein, mtoto mwingine katika nyumba ya Bibi Fatimatuz Zahra SA binti mpenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW.

Kila mtu huvutiwa na umaridadi na uzuri. Ukimtazama mwanaadamu, utaona uzuri na umaridadi ambao ni ishara ya Mwenyezi Mungu. Wenye hekima wanasema mwanaadamu ni maridadi zaidi kuliko viumbe wengine. Maumbile yake hayana kifani na ni maridadi.Kant, mwanafalsafa Mjerumani anasema: 'Ili kumpata Mungu nilitazama vitu viwili. Moja ni mbinu ambazo maumbile yake ni adhimu na pili ni ndani ya nafsi yangu. Vitu hivi viwili ni vya ajabu na vinaweka wazi pazia la ubora.'

Haram ya Imam Husaain AS nchini Iraq

 

Mjukuu wa Mtume SAWImam Hussein AS ni nembo ya wazi ya mwanaadamu mwenye sifa za juu na mwenendo bora. Yeye ni mjukuu wa Mtume SAW, mwana wa Ali AS na Fatima Zahra SA. Aliinukia na kulelewa katika nyumba ya Wahyi na mazingira ya kimaanawi ya mafundisho ya Ahul Bayt (AS). Hizi ni sifa kubwa kwa mwanaadamu.Pamoja na hayo, Imam Hussein AS hakutosheka na sifa hizo. Tokea utotoni wake, alipata mafunzo na malezi ya hali ya juu kupitia tadbiri na hekima ya baba yake. Hussein AS daima alikumbuka maneno haya ya baba yake aliposema: "Umaridadi wa mwanaadamu uko katika akili na fikra zake." Kwa hivyo kwa kufuata mkondo huo aliweza kufika katika daraja ya juu kabisa ya izza na heshima.Aziz ni moja ya majina ya Mwenyezi Mungu SWT na neno hili linamaanisha mwenye uwezo, nguvu , sharafa na heshima.Watu wenye shani na heshima kubwa miongoni mwa wengine na ambao hawanyooshi mkono wa msaada kwa yeyote huitwa Aziz. Mwenyezi Mungu huitwa Aziz kutokana na kuwa hahitajii chochote na ni mkwasi ilihali viumbe na vyote vilivyo mbinguni na ardhini vinamhitaji Yeye.Mawalii wakubwa wa Mwenyezi Mungu wanataka mwanaadamu awe na izza na kuwataka watu wajipambe kwa sifa nzuri.Kwa mtazamo wa Imam Hussein AS, mtu ambaye maisha yake yana izza, ni mtu aliye imara na asiyeweza kusambaratika. Mwanaadamu mwenye izza huwa amechagua maisha yenye uhuru, heshima na nguvu na huwa katika mkondo wa kukamilika na kustawi.Kwa mujibu wa fikra za Imam Hussein AS, moja ya vigezo vingine vya umaridadi katika mwanaadamu ni kutozingatia masuala ya kujirundikia mali ya kidunia. Aliukumbusha umma kuhusu suala hili muhimu kwa kusema: 'Kile ambacho kinaangaziwa na jua katika ardhi, kutoka Mashariki hadi Magharibi, bahari hadi jangwani, kutoka milima hadi maeneo tambarare, ni mtu mwenye maarifa ya Mwenyezi Mungu.....' Katika sehemu nyingine anaendelea kwa kusema: ‘Enyi watu msijiuze kwa dunia hii inayopita. Jueni kuwa chochote isipokuwa Janna hakiwezi kuwa malipo yenu na kila ambaye anafungamanisha roho yake na dunia hii, badala ya Mola wake atakuwa ameridhika na kitu kisicho na maana.'Kila mwaka tunapomkumbuka Imam Hussein AS, tunashuhudia kuongozeka watu ambao wameathiriwa na moyo wake mtakatifu na hivyo kufuata njia nyoofu.

Imam Hussein AS awavutia hata wasiokuwa WaislamuTakwimu zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya watu wanaosilimu huwa wamevutiwa na shakhsia wakubwa kama vile Mtume SAW, Imam Ali AS na hamasa ya kudumu ya Imam Hussein AS. Leo wanaadamu wengi wanakidhi kiu ya umaanawi kwa kufuata kigezo ambacho ni mfano wa kivitendo na wa kweli wa mwanaadamu aliyetakasika.Wengi waliosimama kidete mbele ya hujuma na uporaji wa madola makubwa yanayotumia mabavu wamepata ilhamu kutoka mapambano ya kutetea haki na izza ya Imam Hussein AS. Itikadi hii ya kihistoria inapatikana katika fasihi ya kisasa ya Wakristo wa Lebanon.Mashairi na maandishi ya baadhi ya malenga wa Kikristo Lebanon yameangazia kwa kiasi kikubwa shakhsia ya kihamasa ya Imam Hussein AS na harakati yake adhimu. Paul Salameh malenga na mwanafasihi mashuhuri Mkristo wa Lebanon ni kati ya watu ambao wameandika mashairi yenye kudhihirisha mapenzi ya kina kwa Imam Hussein AS. Salameh anaandika hivi: ‘Malenga Mwarabu awe Mwislamu au Mkristo ana deni kubwa kwa Uislamu. Hii ni kwa sababu haiyamkiniki kuandika kwa ufasaha bila kufaidika na yaliyomo katika Qur'ani Tukufu.....pengine mtu anaweza kulalamika na kuhoji ni kwa nini Mkristo anafafanua kuhusu historia ya Uislamu...Ndio mimi ni Mkristo; lakini Mkristo mwenye uono mpana.....Kila wakati ninapotizama maisha ya Ali AS na mwanae Hussein AS nakumbuka nara za kuunga mkono haki na kupinga dhulma.'

 

‘Hussein ni johari ya kudumu ya dini mbali mbali'Antoine Bara mwandishi habari Mkristo kutoka Syria anasema Imam Hussein ni wa wanaadamu wote na anamuarifisha kwa kusema, ‘Hussein ni johari ya kudumu ya dini mbali mbali.' Mwandishi huyo anamaliza ibara hiyo kwa kusema, ‘Hussein AS yuko katika moyo wangu.' Anaendelea kusema: ‘Sisi tumechunguza kile ambacho ni maridadi na kufikia natija hii kuwa, umaridadi wote uko katika shakhsia ya Mtume Muhammad SAW, Imam Ali AS na Imam Hussein AS. Siku moja mjini Damascus katika kongamano, Mohammad Rafaie, malenga wa Syria alisema hivi kunihusu. Dini ya Antoine ni Ukristo, utambulisho wake ni wa Mwislamu, mapenzi yake ni Ushia na lugha yake ni Kiarabu.' Antoine Bara anaendelea kusema: ‘Ukweli ni kuwa mimi ninampenda Hussein. Mimi ni mfuasi wa roho ya kimapinduzi ya Hussein AS. Khushuu yake sambamba na roho yake ya kimapinduzi ni moja ya nukta za shakhsia ya Hussein iliyonipelekea nivutiwe naye. Sambamba na izza, uhuru na ushujaa mbele ya maadui, alikuwa na roho ya khushuu. Ni vigumu sifa hizi kujikusanya katika mtu mmoja.'Antoine Bara anamtaja Imam Hussein kuwa ‘Taa ya Uislamu' kwa maana ya mwokozi na anayeweka wazi njia. Aidha anamtaja Imam Hussein kuwa ‘Silaha ya Uislamu' kwa maana ya anayeikinga dini kutokana na uharibifu au madhara.Mkristo mwingine wa Lebanon Joseph al Hashim vile vile katika moja ya kasida zake anasema: ‘Kutokana na kuwa ulimwengu ulikuwa umetawaliwa na shirki na ufisadi, Mwenyezi Mungu aliwatuma Ahlul Bayt, ili wawe kama mwenge wa kuwaokoa waja wa Mungu na hivyo haki ienee katika mataifa....Ewe mwana wa Fatima na Ali! Je, kuna adhama kubwa zaidi kuliko hii? Ewe ambaye amerithi ukubwa na heshima! Ewe ambaye hukudanganyika kwa vishawishi vya dunia! Ewe ambaye umeitoa muhanga roho yako! Kama hungekuwepo, hakuna bendera yoyote ya Mwenyezi Mungu ambayo ingeweza kupepea. Wewe si Imam wa Mashia wako tu, bali ni kiongozi wa wanaadamu wote. Umepeleka nafasi ya imani katika kilele na kudhihirisha umaridadi wa mwanaadamu.....'Tuiangazie pia kauli ya Nasri Salhab mwandishi wa Lebanon ambaye katika utangulizi wa kitabu chake, baada ya kuashiria shakhsia adhimu na ya kijihadi ya Amirul Muminin Ali AS na hitajio la zama hizi kwa shakhsia kama huyu anaandika hivi: Ewe bwana wa Mashahidi! Mimi natoka katika ardhi ya kengele zenye majonzi na minara iliyotulia.....acha nije kwa maneno ya wazi kutoka kwa moyo ulioumia, nisema nimekuja ili nipige hatua katika njia yako na nichukue cheche kutoka kwako ili ziwashe adhama katika nafsi yangu, ili kwanza kuniwezesha nimshinde adui wa ndani ya nafasi yangu na baada ya hapo adui wa nje ambaye amechafua nchi yangu na kuvunja heshima. Hussein AS kwa maisha yake maridadi na kifo cha heshima, daima atabakia katika dhamiri za wanaadamu. Kwa nini sisi tusichukue hatua ya Jihadi kwa njia ya nchi yetu (Lebanon) iliyoporwa, umma uliojeruhiwa, heshima ya damu yetu? Kwa nini kama Hussein, shujaa wa Karbala bali hata shujaa wa nyakati zote, hatupazi sauti kwa mdomo na vitendo.'Maandishi ya Edmond Rizk mwanasheria na malenga maarufu wa Lebanon pia ni ya kuvutia. Anasema hivi katika makala: ‘Siujui msafara wowote katika historia ambao ninatamani ningekuwa nao kama msafara ambao ulitoka Hijaz kwa uongozi wa mwana wa Ali na Zahra na kueleka Iraq ili kwa kujitolea muhanga wahuishe haki.

Imam Hussein AS alitawakal kwa AllahHakuna wakati wowote moyo wangu ulitaka kurusha mkuki au kulengwa kwa mshale ila ile siku ambayo nikiwa kijana nilisikia simulizi za hamasa kumhusu Hussein ambaye kwa kutawakali kwa Allah pekee, alichukua upanga.' Anaongeza kwa kusema: ‘Miongoni mwa watu na maamuzi yao kuna uhusiano mkabala. Watu huchukua maamuzi na maamuzi hayo kuwapeleka hadi kileleni. Ewe Hussein kile ambacho kinaonekana katika uso wako ni mafanikio yako katika njia ya wakati maalumu, maamuzi yako ya juu yalikuwa ya kujitoa muhanga, nguvu iko hapo ingawa kidhahiri hilo linaonekana kama udhaifu'.Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa kheri na fanaka kwa Waislamu wote duniani na hasa wapenda amani na haki na wafuasi wa Watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume (SAW) kwa munasaba huu adhimu wa kukumbuka kuzaliwa Imam Hussein AS, kiongozi wa wapenda uhuru duniani.

Tags