Trump na kupamba moto tena ubaguzi nchini Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani siku chache zilizopita aliendeleza siasa za kuwapiga vita wahajiri na wageni nchini humo kwa kutoa matamshi machafu yaliyowakasirisha walimwengu na kuonesha tena dhati ya kibaguzi ya kiongozi huyo.
Alkhamisi iliyopita ya tarehe 11 Januari alipokuwa akihutubia kikao cha wawakishi wa chama cha Democratic na Republican, Trump aliashiria wahajiri kutoka El Salvador, Haiti na nchi za Kiafrika na kusema: Kwa nini mnawaruhusu watu kutoka nchi ambazo ni shimo la kinyesi kuingia Marekani? Trump alisema anafadhilisha kuona wahajiri kutoka nchi kama Norway wakiingia Marekani.

Pasi na kukanusha matamshi hayo, Ikulu ya Rais wa Marekani, White imetangaza kuwa: "Baadhi ya wanasiasa mjini Washington wanatetea maslahi ya nchi za kigeni lakini Trump siku zote anapigana vita kwa ajili ya watu wa Marekani." Taarifa hiyo imedai Trump anataka kurekebisha sheria za uhamiaji za Marekani ili nchi hiyo ipokee wahajiri watakaosadia kustawisha uchumi wa Marekani.
Matamshi ya Trump na majibu la White House kwa malalamiko ya walimwengu dhidi ya matamshi hayo yamezusha wimbi la hasira ya wanasiasa na taasisi za kimataifa ikiwemo Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa. Mkuu wa kamisheni hiyo Zeid Ra'ad al Hussein amesema: Neno bora zaidi linaloweza kutumiwa kwa ajili ya kuarifisha matamshi ya Trump ni kwamba ni ya "kibaguzi". Haiwezekani kuzitaja nchi na mabara ambayo hutaki kuwapokea wakazi wake kwa sababu ya rangi ya ngozi yao kuwa ni kinyesi na uchafu", mwisho wa kunukuu.
Hapana shaka yoyote kwamba, matamshi kama haya ya Trump yanatokana na fikra na mitazamo ya kibaguzi iliyokuwepo na iliyopo hivi sasa nchini Marekani. Historia ya ubaguzi nchini Marekani inarejea katika zama za kuundwa nchi hiyo na kuhamia wazungu kutoka Ulaya. Wazungu wa Uingereza, Wafaransa na Wahispania waliohamia nchini humo ndio walioanza kutoa fikra kuwa wao ndio watu bora zaidi na kuwaita wenyeji na wakazi asilia wa eneo hilo kuwa ni wanyama na washenzi, na huu ulikuwa mwanzo wa kujitokeza ubaguzi katika eneo hilo. Hata hivyo dhulma hiyo ya ubaguzi haikuwapata Wahindi Wekundu wa Amerika pekee. Wakati wazungu wa Ulaya walipoanza kuzikoloni nchi za bara la Afrika katika kipindi cha mwaka 1500 na 1800 wafanyabiashara ya utumwa miongoni mwao waliwachukua karibu Waafrika milioni 15 na kuwapeleka huko Amerika na kuwatumikisha katika mashamba na migodi ya madini. Utumwa huko Amerika haukukomeshwa hata baada ya kutangazwa uhuru wa Marekani na kuwepo serikali inayojitegemea, bali uliendelezwa katika sura mpya. Japokuwa kukoma kwa vita baina ya wakazi wa kaskazini na kusini mwa Marekani kulipelekea kuachiwa huru mamilioni ya watumwa, lakini ubaguzi katu haukukomeshwa katika jamii ya Marekani na watu weusi waliendelea kunyimwa haki zao nyingi za kiraia ikiwemo haki ya kumiliki na haki ya kushika nafasi yoyote muhimu ya kisiasa.

Kutokea kwa Vita vya Pili vya Dunia na kushiriki kwa wingi Wamarekani weusi katika vita hivyo kuliwapa matumaini kwamba, yumkini suala hilo likawafanya wapate nafasi sawa na za wazungu. Hata hivyo matumaini hayo hayakuwa ila sarabi na mazigazi matupu. Kwani upinzani dhidi ya utangamano na usawa wa mbari na watu wa rangi tofauti uliendelea kushuhudiwa katika majimbo yaliyokuwa mstari wa mbele katika utumwa. Kwa msingi huo harakati za kupigania uhuru wa watu weusi ziliendeleza mapambano kwa nguvu kubwa zaidi hadi kulipopasishwa sheria ya kufuta utumwa mwaka 1964. Pamoja na hayo ushahidi unaonesha kuwa, Marekani licha ya madai yake ya kuwa kirana wa kutetea haki na utukufu wa mwanadamu, bado inaongoza katika ubaguzi na ukiukaji wa haki za binadamu. Dr. Joseph Errington ambaye ni profesa wa Anthropolojia katika Chuo Kikuu cha Yale ameashiria uhakika huo na kusema: Hapana shaka kuwa, ubaguzi ungali unaendelea kwa kiwango kikubwa nchini Marekani hususan katika majimbo ya kati na kusini mwa nchi na kuna safari ndefu sana hadi kuweza kung'oa kikamilifu mizizi ya mielekeo na fikra za kibaguzi katika jamii ya Marekani.

Ripoti iliyopewa jina la Boston Review inaunga mkono waziwazi kuwepo kwa ubaguzi nchini Marekani. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa zaidi ya Wamarekani milioni mbili wenye asili ya Afrika wanasumbuliwa na vizuizi vya aina mbalimbali katika kupiga kura. Vilevile Wamarekani weusi daima hukabiliwa na vikwazo na matatizo mengi wakati wa kutafuta ajira na kazi, na ubaguzi katika sekta ya ajira nchini Marekani unatajwa kuwa jambo la kawaida. Uchunguzi uliofanyika nchini Marekani pia unaonesha kuwa, kumeibuka tena harakati ya ubaguzi wa rangi na mbari (apartheid) katika maeneo ya kazi nchini humo. Takwimu zinaonesha kuwa, baadhi ya Wamarekani wanataka kutenganishwa baina ya wazungu na watu weusi katika kazi 19 kati ya kazi 58 zilizofanyiwa uchunguzi.

Wataalamu wengi wanaamini kuwa, harakati hiyo ya kibaguzi inayomtambua mtu mweupe kuwa ni bora zaidi kuliko mweusi imeshika kasi zaidi baada ya ushindi wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani. Vilevile wanasema kuwa mapigano yaliyoambatana na umwagaji damu yaliyotokea katika mji wa Charlottesville kwenye jimbo la Virginia huko Marekani baina ya waungaji mkono wa ubaguzi na wapinzani wao yanashabihiana sana na mapigano kama hayo yaliyokuwa yakishuhudiwa nchini humo katika nusu ya kwanza ya karne iliyopita. Katika mapigano hayo makundi yenye misimamo mikali ya wabaguzi wa rangi, manazi mamboleo na waungaji mkono wa Donald Trump walitoa nara na kaulimbiu kali za kibaguzi zinazowatambua wazungu kuwa ndio watu bora na kizazi cha juu zaidi na kuwalaani wahamiaji na wahajiri. Vilevile mzungu mmoja kati ya wabaguzi hao walichukua gari lake na kuwagonga watu waliokuwa wakiandamana kupinga ubaguzi, na ripoti ya vyombo vya dola inasema, mwanamke mmoja aliyekuwa na umri wa miaka 32 aliuawa na wengine 19 walijeruhiwa katika hujuma hiyo.
Wamarekani wanaamini kuwa Trump ndiyo sababu kuu ya matukio hayo yote na wanasema kuwa, kiongozi huyo wa Marekani na washauri wake wanaunga mkono moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja harakati za makundi ya kibaguzi. Wamarekani wanasisitiza kuwa, kasi ya vitendo vya kibaguzi vinavyoshuhudiwa sasa nchini humo ni matokeo ya matamshi ya kibaguzi yanayotolewa na Donald Trump. Hasira za Wamarekani dhidi ya Trump katika machafuko ya mji wa Charlottesville ilishadidi zaidi baada ya kujulikana kwamba, idadi kubwa ya wabaguzi wa rangi na mbari waliokuwa katika machafuko hayo ni wafuasi wa Trump na kwamba kiongozi huyo hakuwataka wafuasi wake wasishiriki katika ghasia hizo au kwa uchache wasifanye fujo na ukatili licha ya kwamba alikuwa na habari ya mipango ya maandamano ya kundi hilo. Hata katika ujumbe wake alioutoa baada ya ghasia hizo, Trump hakuwa tayari kuwataja wabaguzi hao kuwa ndio waliosababisha machafuko bali alizilaumu pande zote mbili za watetezi na wapinzani wa ubaguzi!

Matusi na matamshi ya kibaguzi ya Donald Trump dhidi ya Waafrika na nchi zao ni mwendelezo wa fikra na mitazamo hiyo ya kibaguzi. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana baadhi ya wabunge wa Marekani wakayataja matamshi hayo kuwa ni kielelezo kwamba kiongozi huyo ni mbaguzi. Mbunge wa jimbo la Florida katika Kongresi ya Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic, Ileana Ros-Lehtinen ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: "Kuiita nchi ya Haiti kuwa ni shimo la choo ni sawa na kupuuza huduma zilizotolewa na wahajiri wa nchi hiyo nchini Marekani. Maneno kama haya hayapaswi kutoka White House."
Seneta wa chama cha Republican, Orrin Hatch yeye ametaka maelezo zaidi kuhusu matamshi hayo ya kibaguzi ya Trump. Hatch amesisitiza kuwa, kuhamia Marekani watu wenye vipaji kutoka maeneo mbalimbali ya dunia ni miongoni mwa mambo yanayoifanya nchi hiyo kuwa maalumu.
Mbunge Luis Gutiérrez anayewakilisha jimbo la Illinois katika Kongresi ya Marekani anasema: "Sasa imebainika kwa asilimia mia moja kwamba Donald Trump ni mbaguzi na kwamba hakubali thamani zinazodhaminiwa na katiba ya Marekani."

Siku moja baada ya matamshi ya kibaguzi ya Trump, Umoja wa Afrika ulitoa taarifa ukipinga vikali matamshi hayo ya Rais wa Marekani na kusisitizia kuwa: Kwa kutilia maanani ukweli wa kihistoria kwamba idadi kubwa ya Waafrika walipelekwa Marekani kama watumwa, matamshi ya Trump ni kinyume kabisa na kaida na hayawezi kuvumiliwa. Sehemu moja ya taarifa ya Umoja wa Afrika imesema: Matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu bara Afrika yanaonyesha ubaguzi wa wazi wa kiongozi huyo.
Ukweli ni kwamba Rais wa Marekani ambaye kila siku anaishambulia nchi huru kwa madai ya kutoheshimu haki za binadamu yeye mwenyewe ni miongoni mwa wakiukaji wakubwa zaidi wa haki za binadamu duniani. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa sheria zote za kimataifa, ubaguzi na ubaguzi wa rangi ni miongoni mwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na inaonekana kwamba, Trump anajisahaulisha suala hilo.