Sep 11, 2018 07:49 UTC
  • Maswahaba wa Imam Hussein AS-01

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachozungumzia matukufu na ubora wa masahaba wa Imam Hussein bin Ali (as) na imani yao thabiti, kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika jangwa la Karbala, wafuasi wa Imam Hussein (as) walikuwa wa kila aina, wenye umri tofauti na rangi mbalimbali. Mzee, kijana, mwanamke na mtoto, mweusi kwa mweupe, wote walikuwa katika jangwa hilo kwa ajili ya kumnusuru Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). Baadhi ya masahaba kama vile Habib Bin Madhahir na Muslim bin Ausajah walikuwa miongoni mwa wafuasi wenye ikhlasi na masahaba wa zamani wa Mtume (saw) na baadhi yao kama vile Zuhair bin Qain Bajala alikuwa mtu wa mrengo wa Othmani. Wengine ni kama Wahab bin Abdullah Kalbi, walikuwa Wakristo ambao ndio kwanza walikuwa wamesilimu na kuingia katika dini ya Uislamu na aliendelea kushikamana na mjukuu huyo wa Mtume (as) na kuuawa shahidi.

******

Mwanzoni mwa kudhihiri dini ya Uislamu kulijiri vita na mapigano mengi dhidi ya ukafiri na udhalimu. Hata hivyo hakuna mapigano yaliyokuwa na sifa ikhlasi kubwa na kumsafishia nia Allah SW kikamilifu kama yale ya Karbala. Katika vita hivyo vya awali kulishuhudiwa baadhi ya kesi za kutokuwa na ikhlasi kwa baadhi ya  watu na wakati mwingine unafiki na kufia dunia. Baadhi ya askari ambao walikuwa wakipigana vita ama hawakuwa na ari, au walikuwa na woga na tamaa ya kupata ngawira na mali na wakati mwingine walimuacha Mtume Muhammad (saw) peke yake akiwa na masahaba wachache tu waaminifu. Kama ilivyotokea katika vita ya Uhud ambapo wapenda dunia miongoni mwa askari walimuacha Mtume (saw) akiwa peke yake na masahaba wachache waliosabilia nafsi zao kumnusuru mtukufu huyo. Vilevile katika vita vya Khandaq (vita vya Ahzab) baadhi ya masahaba wa Mtume (saw) walikumbwa na woga wa kukabiliana na wapiganaji wa Kikuraishi na walishindwa hata kuinuka katika maeneo yao kwa ajili ya kupambana na washirikina.

Katika tukio la Karbala, Imam Hussein (as) kwanza aliondoa baia (kiapo) kutoka kwa masahaba wake wote na alimtaka kila mmoja wao kuondoka uwanja wa Karbala kwa sababu yoyote ile. Katika njia yao kuelekea Karbala na kwa mara kadhaa, wafuasi wa Imam Hussein walikuwa wakisafisha nia na kuamua kumfuata mjukuu huyo wa Mtume (saw). Hii ni kwa kuwa walimtambua Imam kuwa mtu bora wa zama zao ambaye mapinduzi yake yalipasa kuendelea ili yawe fundisho kwa zama na vizazi vijavyo. Kila mtu aliyebakia pamoja na Imam Hussein alijitenga kabisa na wasiwasi, woga na udhaifu. Suala hilo ndilo lililoifanya siku ya Ashura kuwa kigezo chema na kamilifu. Wakati habari ya kuuawa shahidi Muslim Bin Aqil ilipowafikia watukufu hao, Imam aliwakusanya masahaba wake na kusema: Mtu anayetaka kuondoka, basi na aondoke bila ya tatizo na mimi ninamruhusu..." Hata hivyo masahaba hao wa mjukuu wa Mtume ambao walifadhilisha kifo cha kuuliwa shahidi kuliko maisha ya udhalili, waliendelea kuwa pamoja na Imam Hussein hadi mwisho wa uhai wao.

Wakati Imam Hussein (as) alipowasili jangwa la Karbala tarehe pili mwezi wa Muharram mwaka 61 Hijiria akiwa na masahaba wake aliomba dua akisema: "Ewe Mola wangu Mlezi! Ninajikinga kwako kutokana na shida na balaa…Mola wangu! Ninajikinga kwako kutokana na huzuni na tabu. Haya ndiyo mashukio yetu. Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba eneo hili ndipo tutafufuliwa Siku ya Kiama. Nilisikia kauli hii kutoka kwa babu yangu, Mtume wa Mwenyezi Mungu na hakuna shaka yoyote katika kauli yake", mwisho wa kunukuu.

Baada ya wafuasi wa Imam kusikia maneno ya mtukufu huyo hawakuondoka mahala hapo na kumuacha peke yake. Katika kitabu cha Injili imepokewa kuwa Nabii Isa Masih (as) alikuwa na masahaba 12 waaminifu na waliotambulika kwa jina la 'Hawariyyuna.' Hata hivyo katika usiku ambao Nabii huyo wa Mungu alitabiri kuwa atapatwa na shida, masahaba hao si tu kwamba walipatwa na wasiwasi mkubwa kwa kuwaogopa askari wa adui na kujitenga naye, wengine walikaribia kumkana Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu na wako miongoni mwao waliomkana kabisa kama Yuda. Hali hii ni tofauti kabisa na ile wa masahaba wa kweli wa Imam Hussein (as) ambao waliyapokea mauti na kuuliwa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mikono miwili.  

Imam Hussein (as) katika usiku wa Ashura na baada ya kuwaomba maadui muhula wa usiku mmoja kwa ajili ya kunong'ona na Mola Muumba, alitoa hotuba nyingine kwa masahaba wake akisema: "Mola wangu! Ninakutukuza sana na ninakushukuru kwa raha na shida, magumu na raha. Mola wangu nakushukuru kwa kuwa wewe ni Mwenyezi Mungu ambaye ulimtuma kwetu Mtume aliyetufundisha elimu ya Qur'ani na elimu ya dini. Umetupa masikio yenye kusikia, macho yenye kuona na mioyo inayoelewa. Ewe Mola Mlezi! tujaalie tuwe kati ya watu wanaokushukuru. Amma baad! Mimi sijui wafuasi bora na waaminifu zaidi kuliko masahaba zangu, wala familia ya watu watiifu na wakweli zaidi kama familia yangu. Mwenyezi Mungu akupeni malipo mema kwa kunisaidia." Akiendelea na hotuba yake mjukuu huyo wa Mtume aliwaruhusu tena masahaba wake waondoke na kunusuru maisha yao kwa kusema: "Ninajua kwamba kesho tutakuwa na vita na wao. Hivyo ninaondoa baia (kiapo) chenu kwangu. Tumieni giza hili la usiku kwa ajili ya kuondoka na kuepukana na eneo hili la hatari. Hao watu wananitaka mimi tu na watakaponipata mimi, hawatokuwa na shida na nyinyi", mwisho wa kunukuuu.

Baada ya Imam Hussein kutoa hotuba hiyo kila sahaba alitoa maelezo yenye kusisimua na yenye kuonyesha upendo wake wa hali ya juu kwa mjukuu huyo wa Nabii wa Allah na kuahidi kuendelea kuwa pamoja na Imam hadi mwisho wa uhai wake. Kwanza kabisa alianza Abbas bin Ali, (ndugu yake Imam Hussein) kwa kusema; "Kwa nini tukuache peke yako? Ili tuweze kuishi baada yako? Mwenyezi Mungu asitujaalie kuiona siku kama hiyo." Baada ya Abbas vijana wengine katika familia ya Bani Hashim mmoja baada ya mwingine walitoa maneno kama hayo na kuahidi kuendelea kuwa pamoja na Imam Hussein (as).

Makaburi ya mashahidi wa Karbala

Baada ya watu wa familia ya Mtume kutoa baia na kiapo cha utiifu na kuendelea kumnusuru mjukuu huyo wa Mtume, Muslim bin Ausajah Asadi, alikuwa mtu wa kwanza kusimama na kutoa maneno yenye msisimko na upendo kwa kusema: "Ewe Abu Abdillah! Hivi kweli tunaweza kukuacha peke yako? Wakati huo tutatoa udhuru gani mbele ya Mwenyezi Mungu? Hapana, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba kamwe hatutokuacha peke yako. Sitaondoa mkono wangu kwako hadi nitakapotoa pigo kwa maadui na mshale na upanga wangu hautoanguka chini ila baada kuwapiga nayo maadui. Na baada ya hapo kama sitakuwa na silaha, basi nitawapiga maadui kwa mawe. Ninaapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba kamwe sitotengana na wewe ili Mwenyezi Mungu ajue kwamba, tumelinda hadhi na heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Wallahi nikijua kuwa nitauawa, kisha nifufuliwa, kisha nikachomwa moto na kuwa majivu na kwa mara nyingine nikafufuliwa na nikafanyiwa hivyo mara 70, kamwe sitotengana na wewe hadi pale nitakapoungana na msafara wako wa kuuliwa shahidi. Na ni kwa nini nisifanye hivyo ilhali nitauawa mara moja tu na kisha kupata utukufu na saada ya milele?".

Muslim Bin Ausajah Asadi, alikuwa mmoja wa masahaba wakubwa wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na pia sahaba wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Alikuwa mtu mwema sana na mcha-Mungu aliyesifa kwa zuhudi kubwa na kuipa mgongo dunia. Muslim alikuwa mpiganaji hodari na mpanda farasi shujaa ambaye alikuwa akizungumziwa sana katika vita mbalimbali vya Kiislamu. Sahaba huyo alitoka kabila la Bani Asadi ambalo lilikuwa likiishi Kufa nchini Iraq. Alikuwa miongoni mwa watu waliomuandikia barua Imam Hussein kutoka Kufa na baada ya Muslim Bin Aqil kuwasili mji huo aliendelea kuchukua baia  na viapo vya utiifu kutoka kwa wakazi wa Kufa. Baada ya Muslim Bin Aqil na Hani Bin Urwa kukamatwa na kuuawa shahidi, Muslim bin Ausajah alielekea kwa Imam Hussein pamoja na familia yake na kusabilia roho yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Tags