Siku ya Familia ya Kiislamu
(last modified Mon, 17 Sep 2018 07:57:04 GMT )
Sep 17, 2018 07:57 UTC
  • Siku ya Familia ya Kiislamu

Tarehe 25 Dhulhija ndiyo siku ilipoteremshwa sura ya Qur'ani tukufu ya "Insan" kwa Mtume Muhammad (saw).

Kwa kuwa sura hii ya Qur'ani iliteremshwa kuhusu familia tukufu na takatifu zaidi duniani yaani familia ya Mtume Muhammad (saw), siku hiyo ya tarehe 25 Dhulhija katika kalenda ya Iran imepewa jina la "Siku ya Familia". 

Wanazuoni wote wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia na aghlabu ya maulama wa madhehebu za Suni wanaamini kuwa, sura hii ambayo pia ni maarufu kwa majina ya Sura ya "Hal Ataa" na Suratud "Dahr" iliteremshwa kuhusiana na Ahlubaiti wa Mtume Muhammad (saw) yaani Ali, Fatima, Hassan na Hussein kufuatia kitendo chao kilichokuwa kimejaa ikhlasi na uchamungu. 

Imenukuliwa katika vitabu vya historia, tafsiri ya Qur'ani na Hadithi kwamba, siku moja watoto wawili wa nyumba hiyo ya watu waliokuwa na maisha ya chini kimaada lakini adhimu zaidi kimaanawi na kiroho yaani Hassan na Hussein walipatwa na maradhi. Mtume (saw) na masahaba wake wawili walikwenda nyumbani kwa Fatima kuwajulia hali wajukuu wake. Huko, Mtume alimwambia Ali bin Abi Twalib (as) kwamba: "Itakuwa bora uweke nadhiri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ili awape shifaa na kuwaponya watoto wako." Ali alimwambia Mtume (saw) kwamba: Ninaweka nadhiri ya kufunga Swaumu siku tatu iwapo Hassan na Hussein watapata shifaa na kupona. Bibi Fatimatu Zahra (as) pia alisema maneno hayo hayo. Vivyo hivyo waliweka nadhiri Hassan, Hussein na hadimu wao, Fidha. Siku kadhaa baadaye Hassanain walipata shifaa na kupona. Hivyo watu wa nyumba hiyo ya kimaskini walianza kutekeleza nadhiri yao na kufunga Swaumu. Hata hivyo hawakuwa na chakula chochote cha futari. 

Ali bin Abi Twalib (saw) alikwenda kwa bwana mmoja Myahudi ambaye alikuwa mtengeza sufu na kumwambia: Uko tayari binti wa Muhammad akusokotee sufu na mkabala wake utoe kiwango fulani cha shayiri? Myahudi yule ambaye alikuwa amepigwa na butwaa kutokana na maisha ya watu wa chini kabisa kimaada ya Nyumba ya Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu alikubali pendekezo hilo na akampa kiasi fulani cha sufu kwa ajili ya kusokotwa. Bibi Fatima alisokota sufu hiyo kisha Ali (as) akanunua unga na kutayarisha vipande vitano vya mkate wa shayiri kwa ajili ya futari. Baada ya kuswali Swala ya Magharibi na Mtume (saw), Ali bin Abi Twalib alirejea nyumbani na kitanga cha chakula kikatandikwa ambapo watu wote watano wa nyumba hiyo waliketi kwa ajili ya kufuturu. Ghafla alijitokeza maskini na kuomba chakula. Watu wa nyumba hiyo walimpa maskini huyo vipande vyote vitano vya mkate. Walilala njaa na kutosheka kwa kunywa maji matupu.

Siku ya pili yake watukufu hao pia walifunga Swaumu wakitimiza nadhiri yao. Baada ya Swala ya Magharibi walipoteki kupata futari, alikuja nyumbani hapo mtoto yatima na kuomba chakula. Mara hii pia watukufu hao walisabilia chakula chao cha futari na kubakia na njaa usiku kucha. Hali hiyo ilikariri tena siku ya tatu wakati mateka aliyekuwa amezongwa na njaa alipokwenda nyumbani hapo na kuomba chakula. 

Siku iliyofuatia Mtume Muhammad (saw) aliwaona Ahlibaiti wake huku Hassan na Hussein wakitetemeka kutokana na njaa. Binti yake mtukufu, Fatimatu Zahraa ambaye macho yake yalikuwa yametumbukia ndani kutokana na kutokula chakula kwa siku tatu za funga ya nadhiri, alikuwa katika hali ya ibada. Baadaye kidogo Mtume (saw) alimkumbatia kifuani binti yake kipenzi na kusema: Subhanallah! Mumekaa na njaa siku tatu mfululizo?! Wakati huo Malaika Jibrilu aliteremka kwa Mtume (saw) na kusema: "Ewe Muhammad! Mwenyezi Mungu SW anakupongeza kwa kuwa na Ahlubaiti na familia kama hii, na pokea alichokutayarishia Mola kwa ajili yao." Mtume aliuliza: Ni kitu gani ewe Jibrilu? Malaika huyo mwema alianza kusoma aya za mwanzoni mwa Suratul Insan au Hal Ataa hadi alipofika aya inayosema: Hakika haya ni malipo yenu, na juhudi zenu zimekubaliwa.

Kama tulivyosema mwanzoni mwa kipindi hiki, tarehe 25 Mfunguo tatu Dhulhija ni siku ya kuteremshwa Sura ya "Hal Ataa" na siku hii katika kalenda ya Iran imepewa jina la Siku ya Familia ili kupitia njia ya kufuata nyayo za familia hiyo tukufu, tupate baraka za Mwenyezi Mungu katika familia zetu. Familia katika utamaduni wa Kiislamu ni taasisi takatifu na muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa mwanadamu na ni jiwe na msingi la maisha bora ya jamii. Familia iliyojengeka kwa mujibu wa misingi sahihi mbali na kustawisha watoto wema kwa ajili ya jamii, vilevile huwa ngome ya amani na utulivu kwa wazazi wawili na watoto wao. Hali hii huwa na taathira kubwa katika kujenga jamii yenye watu wema, iliyostawi na kustaarabika.

Hii leo taathira nzuri za taasisi muhimu ya familia zimepungua sana katika mtindo wa maisha wa kimagharibi kutokana na kupuuzwa umuhimu wa taasisi hiyo na kusisitizwa zaidi na kupita kiasi juu ya maisha ya mtu binafsi. Tunaona kuwa, mahusiano baina ya wanachama wa familia moja yamekuwa ya kuyumbayumba na yanatawaliwa na mashaka na misukosuko mingi katika baadhi ya jamii za kimagharibi au jamii zinazofuata mtindo wa maisha wa Magharibi. Uhusiano usio na mipaka baina ya mwanamke na mwanaume nje ya misingi ya ndoa na familia na kuzaliwa watoto ambao hawakupata ladha ya maisha yenye utulivu na malezi ya baba na mama, vinaathiri malezi na ustawi wa kimwili, kiakili na kiroho wa watoto na kusababisha matatizo mengi kwa wanawake. Kudurusu na kupitia tena nafasi ya familia katika dini inayomjenga mwanadamu ya Uislamu katika mazingira kama haya kunaweza kuwa mojawapo na njia za kufumbua matatizo ya jamii ya leo ya mwanadamu.

Msingi wa kujenga familia katika Uislamu huanza kwa kufunga ndoa ambayo ni mfungamano mtakatifu sana baina ya mwanaume na mwanamke. Kwa msingi huo Aya za Qur'ani tukufu na Hadithi za Mtume (saw) na Ahlibaiti wake watoharifu zinasisitiza sana suala la kufunga ndoa na kukataza au kukemea ukapera na useja. Imepokewa katika Hadithi kwamba Mtume (saw) amesema:

من سعاده المرء الزوجه الصالحه.

Kuwa na mke mwema ni sehemu ya ufanisi na saada ya mwanaume. Vilevile amesema katika Hadithi nyingine kwamba:

مَنْ سَرَّهُ أنْ‌ یَلْقَی اللهَ طاهِراً مُطَهَّراً فَلْیَلْقَهُ بِزَوْجَةٍ.

Mtu anayetaka kukutana na Mwenyezi Mungu akiwa msafi na aliyetwahirishwa basi akutane naye akiwa na mke.

Ili kulinda familia ambayo ndiyo msingi wa malezi bora na ustawi wa mwanadamu, Uislamu umekuja na mafundisho muhimu kwa wanandoa wawili na watoto wao na kuainisha majukumu na haki za kila mmoja wao.

Kwa mfano tu, kuhusu umuhimu wa kuenzi familia, Mtume Muhammad (saw) anasema: Mwanaume kukaa pamoja na mke na mtoto wake ni bora zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kufanya itikafu msikitini. Vilevile anasema katika Hadithi nyingine kwamba: Mtu anayefanya jitihada kutafuta rizki ya halali kwa ajili ya familia yake ni sawa na mtu anayepigana vita vya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.     

Katika mafundisho ya Uislamu kumetajwa majukumu na haki za mke na mume lakini muhimu zaidi ni kuheshimiana, kuwa na insafu na uadilifu, kusameheana na kuvumiliana. Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 19 ya Suratu Nisaa kwamba: Na kaeni nao (wake zenu) kwa wema, na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu na Mwenyezi Mungu ametia kheri nyingi ndani yake... Vilevile Mwenyezi Mungu anawauasia wanawake kulinda mali na hadhi ya waume zao, kuwa na upendo na usahemevu na kusisitiza kuwa, mashaka anayopata mume na mke kwa jaili ya kumfurahisha, kumridha na kuhakikisha mwenzi wake anapata hali bora yana ujira na malipo huko Akhera na yana taathira katika ukamilifu wa kiroho.

Katika upande mwingine watoto wanaozaliwa katika familia yenye misingi sahihi wamepewa mazingatio maalumu na wana haki kwa wazazi wao wawili. Kwa mfano tu Mtume (saw) anasema: Waheshimuni watoto wenu na amilianeni hao kwa adabu na mwenendo mzuri. Vilevile watoto wana majukumu mbele ya wazazi wao na wanawajibika kuwatendea wema na kuamiliana nao kwa upole na unyenyekevu. Aya ya 23 ya Suratu Israa inasema: Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima.

Mtazamo kama huu kwa familia katika utamaduni wa Kiislamu unaifanya taasisi hiyo muhimu zaidi ya kulea mtu na jamii iimarike zaidi na kuwa thabiti hata katika vipindi vigumu na vyenye misukosuko mingi. Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa Hadithi ya Mtume Muhammad (saw) inayosema:

اِذا اَرادَ الله‏ُ بِاَهْلِ بَیتٍ خَیرا فَقَّهَهُمْ فِى الدّینِ وَ وَقَّرَ صَغیرُهُمْ کَبیرَهُمْوَ رَزَقَهُمُ الرِّفْقَ فى مَعیشَتِهِمْ وَ الْقَصْدَ فى نَفَقاتِهِم وَ بَصَّرَهُمْ عُیوبَهُمْ فَیتُوبُوا مِنْها وَاِذا اَرادَ بِهِمْ غَیرَ ذلِکَ تَرَکَهُمْ هَمَلاً؛

Mwenyezi Mungu anapoitakia kheri familia yoyote ile huipa elimu na maarifa ya dini, mdogo wao humuheshimu mkubwa miongoni mwao, huwapa rizki katika maisha yao, na mwenendo wa wastani na kutochupa mipaka katika matumizi yao na huwaonesha aibu na nakisi zao ili waondokane nazo...