Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (9) + Sauti
Maombolezo ya Muharram katika kila jamii huambatana na tamaduni, mila na taratibu za jamii hiyo. Lakini jambo la msingi na muhimu hapa ni kwamba utamaduni na mila hizo za maombolezo hazipasi kwenda kinyume na mafundisho ya Kiislamu na wala hazipasi kuruhusiwa kuvunjia heshima dini wala kupotosha ujumbe wa Ashura.
Baada ya tukio la kuhuzunisha la Ashura na kuuawa shahidi wajukuu wa Mtume (saw) katika jangwa la Karbala, Mashia, yaani wafuasi wao walianza kufanya vikao vya maombolezo kwa ajili ya kudhihirisha mapenzi yao kwa Ahlu Beit hao wa Mtume (as) na wakati huohuo kulalamika na kuonyesha kuchukizwa kwao na dhulma waliyofanyiwa watukufu hao wa Nyumba ya Mtume (saw). Vikao hivyo vilifanyika kwa ajili ya kueneza maarifa na mafundisho ya Ahlul Beit (as) na kufikia sasa vimefanikiwa kuhuisha Ushia katika mazingira magumu zaidi ya kisiasa na kijamii katika kipindi cha karne 14 zilizopita. Masisitizo mengi ya Maimamu maasumu (as) juu ya kufanyika vikao hivyo vya maombolezo ya Imam Hussein (as) na Hadithi nyingi ambazo zimepokelewa katika vitabu vya Hadithi ambazo zinazungumzia fadhila za kufanyika vikao hivyo vimepelekea maombolezo ya Imam Hussein kuwa sehemu isiyotenganishika ya utamaduni wa Shia. Lakini kwa masikitiko makubwa baadhi ya marafiki wasio na uelewa wa kutosha na maadui wameingiza baadhi ya tamaduni na mila potovu katika maombolezo hayo ya Muharram, jambo ambalo bila shaka limezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wanazuoni na kuwafanya watoe tahadhari za lazima katika uwanja huo. Kuhusu suala hilo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapiduzi ya Kiislamu anasema: "Leo Hussein bin Ali (as) anaweza kuiokoa dunia kwa sharti kwamba upotovu usitumike kuharibu sura yake. Msiruhusu fikra na mambo potovu na ghalati yazuie macho na nyoyo kuona uso mtukufu na unaong'ara wa Bwana wa Mashahidi (as). Kabilianeni na upotoshaji.''
Moja ya mambo yanayodhuru maombolezo ya Imam Hussein (as) ni kuwa na fikra finyu. Wanazuoni na wanafikra wa Kiislamu wanasisitiza kwamba katika maombolezo hayo, ni fikra na falsafa muhimu ya mapambano ya Ashura dhidi ya dhulma na uonevu pamoja na thamani za kidini na kiutu tu ndizo zinapaswa kufafanuliwa na kuwekwa wazi. Mara nyingine mambo yasiyo na msingi wala umuhimu wowote kama vile kuzungumziwa uzuri wa sura ya watukufu wa Mwenyezi Mungu hubainishwa katika vikao vya maombolezo hayo, suala ambalo kwa hakika hushukisha hadhi yao na vilevile maarifa ya kidini katika jamii. Mfano mwingine ni kwamba katika kumuomboleza Hadhrat Abbas (as) baadhi ya waombolezaji huzungumzia tu macho yake mazuri na ya kuvutia, urefu na umbo kubwa la mwili wake, jambo ambalo kwa hakika ni dhulma kubwa kwa mtukufu huyo. Hii ni kwa sababu thamani muhimu ya mtukufu huyo (as) ilikuwa ni Jihadi na kujitolea kwake, maadili aali, maarifa, subira na mapambano yake ambapo ni kwa kujadili na kufafanua thamazi hizo ndipo jamii inaweza kumtambua vyema na hivyo kushawishika kufuata mfano wake wa ushujaa.
'Kuvuka mpaka katika kupenda' au kwa ibara nyingine, 'kupenda kupita kiasi' ni tatizo jingine linaloonekana likifanywa na baadhi ya watu wanaoongoza maombolezo ya Imam Hussein (as). Watu hao hutoa baadhi ya matamshi na maneno ambayo hukaribia shirki au 'ghuluw' yaani kumsifu mtu kwa sifa asizostahiki na ambazo ametengewa Mwenyezi Mungu tu. Qur'ani Tukufu inakemea na kuwatahadharisha watu na tatizo hilo na Maimamu (as) pia walikuwa wakikabiliana vikali na watu waliojihusisha na suala hilo. Kuhusu hilo, Imam Swadiq (as) anasema: "Watahadharisheni vijana wenu na ghuluw ili wasipate kuharibika. Hii ni kwa kuwa watapuuza na kuukosesha thamani utukufu wa Mwenyezi Mungu na kuwapa umola waja Wake." Hivyo maulamaa na mamar'ja' wanapinga vikali maombolezo ya aina hiyo na kuonya katika fatwa zao, dhidi ya kutumika ibara za aina hiyo zinazokaribia ghuluw na shirki.
Hata kama Mshia anakuchukulia kunyenyekea na kudhihirisha mapenzi kwa Ahlul Beit (as) kuwa fahari kwake na kujivunia jambo hilo lakini suala hilo linatofautiana sana na kujidhalilisha. Ahlul Beit wa Mtume (as) kamwe hawaruhusu wafuasi wao kujidhalilisha kwa namna yoyote ile. Lakini kwa masikitiko makubwa baadhi ya wasomaji wa mashairi ya maombolezo hutumia baadhi ya maneno na ibara ambazo huashiria moja kwa moja kujidhalilisha huko. Kwa mfano matumizi ya maneno kama vile 'mbwa wa Hussein' na 'mbwa wa Ruqiyya' pamoja na kujifunga mikanda ya mbwa shingoni wakati wa kufanyika maombolezo ya Imam Hussein ni jambo lililo mbali na heshima ya Mwislamu yoyote yule. Qur'ani Tukufu na Riwaya za Mtume (saw) na Maimamu wotoharifu (as) zinasisitiza sana juu ya kulindwa utukufu na heshima ya mwanadamu na hasa ya waumini. Watukufu hao kamwe hawaruhusu wafuasi wao kujidhalilisha kwa kisingizio cha kuwaheshimu wao. Ni kutokana na ukweli huo ndipo maulamaa, mamarja' na wanazuoni wote wenye ikhlasi wakapinga aina hiyo ya maombolezo. Baadhi ya mila zinazofanyika katika baadhi ya maeneo kwa anwani ya maombolezo hazikubaliki kabisa katika mtazamo wa Uislamu na madhehebu ya Shia. Kwa mfano kufunga mwili kwa kufuli, kujipiga kwa minyororo iliyo na nyembe na vitendo vingine vinavyodhuru mwili wa mwanadamu ni mambo yanayopingana na mafundisho sahihi ya dini. Vitendo vya aina hiyo vinahesabiwa kuwa bida' na bila shaka ni haramu kutokana na kuwa vinajeruhi na kuudhuru mwili wa mwanadamu. Nukta muhimu hapa ni kwamba vitendo hivi vya kutisha ambavyo huandamana na umwagaji damu, kuzua hofu na kuchukizwa watu, bila shaka huharibu jina la Ushia na kuwa kizuizi kikubwa katika kufikishwa ujumbe halisi wa Ashura, ujumbe ambao Imam Hussein (as) na wafuasi wake waaminifu waliuawa shahidi kwa ajili ya kuwafikishia walimwengu. Kwa mujibu wa fatwa za maulama na maraaji' wa Kishia katika pembe tofauti za dunia vitendo hivyo vinavyokwenda kinyume na mafundisho ya dini ni haramu.
Mila nyingine ya maombolezo ambayo imekuwa ikienezwa sana katika miaka ya hivi karibuni ni kujikata kwa visu au mapanga kichwani hadi damu atiririke. Kitendo hiki cha kuchukiza pia hufanyiwa watoto eti kwa nia ya kutabaruku. Hata kama kitendo hicho kitafanyika kwa nia ya kuomboleza na kushikamana na waliofiwa, lakini bado kitakuwa ni makosa makubwa na haramu kwa dalili tofauti za kidini, kiakili, kisaikolojia na kiafya. Kuhusu hilo, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema kwamba kutokana na ukweli kuwa kitendo hicho si katika maombolezo kwa mtazamo wa kijamii na hakikufanywa katika zama za Maimamu (as) wala baada yao na wala kukijathibitishwa a madhehebu yoyote ya Kiislamu, katika zama hizi kitendo hicho hakiruhusiwi kwa hali yoyote ile kwa sababu hupelekea kuchukiwa na kuharibiwa jina la Ushia. Kitendo hicho vilevile kimeharamishwa na maulama wengi akiwemo Ayatullah Ali Sistani wa Iraq.
Kuna sababu nyingi mno za kuharamisha kitendo hicho cha kujikata kichwani kwa visi au mapanga mojawapo ikiwa ni kwamba kinadhuru mwili na kuhatrarisha usalama wa mtu, na fiqhi ya Kishia inaharamisha kitendo chochote kinachodhuru afya ya mtu. Mbali na hayo kitendo hicho kinapingana na mienendo ya maisha ya Ahlul Beit (as). Suna ya kuomboleza ni urithi tulioachiwa na Imam Baqir na Imam Swadiq (as), na kabla ya Maimamu wengine wote, walikuwa wakisisitiza sana juu ya kufanyika vikao na mikusanyiko ya maombolezo. Watukufu hao wenyewe walikuwa wakihimiza na kushiriki moja kwa moja katika vikao hivyo na wala hawakushuhudiwa wakifanya vitendo hivyo vya kuchukiza. Sababu nyingine ya kuharamishwa kitendo hicho cha kujikata kichwani kwa visu kama tulivyotangulia kusema, ni kuwa huharibu jina la Ushia, kuchukiza na kuwatia hofu na woga wale wanaokishuhudia. Inatosha tuzitembelee baadhi ya kurasa za mitandao ya kijamii ili tupate kujua ni kwa kiwango gani maadui wa Uislamu wamewekeza katika njama chafu za kuwachochea baadhi ya hawa ndugu zetu wasiotambua ukweli wa mambo, ili waendelee kuuharibia jina Ushia kupitia kitendo hicho cha kuchukiza. Maadui hao hufanya juhudi zao zote kwa ajili ya kuakisi kitendo hicho kinachokwenda kinyume na mafundisho ya dini kwenye vyombo vya habari, ili kudhihirisha kinyume na ukweli wa mambo, kwamba Mashia ni watu wanaopenda unyama na ukatili ulio mbali na maadili na mantiki, ili hatimaye wapate kuficha ujumbe muhimu wa Ashura chini ya kitendo hicho kisichokuwa na msingi wowowte katika mafundisho ya Ushia.
Hivyo tunapasa kufanya juhudi za kubainisha na kuweka wazi misingi ya maombolezo ya Imam Hussein (as) na wafuasi wake waaminifu katika mipaka inayokubalika ya maamrisho na makatazo ya Mweyezi Mungu. Tunatakiwa kuomboleza kwa njia sahihi inayokwenda sambamba na malengo ya mapambano ya Imam Hussein (as), ambayo hayakuwa mengine bali kuhuisha na kueneza mafundisho sahihi ya Ahlul Beit wa Mtume (saw) na Ushia.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.