Mwaka 2019 na kujiondoka Marekani na Israel katika shirika la UNESCO
Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe Mosi mwezi huu wa Januari 2019 zilijiondoa rasmi katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) zikilalamikia kile kilichotajwa ni mwelekeo wa jumuiya hiyo dhidi ya Israel.
Kujiondoa kwa Marekani na Israel katika shirika hilo kuliwekwa katika ajenda ya pande hizo mbili yapata mwaka mmoja uliopita na tawala hizo mbili zilitangaza uamuzi huo mwaka 2017. Hata hivyo kwa mujibu wa hati ya UNESCO uamuzi huo ulipaswa kutekelezwa kivitendo mwishoni mwa mwaka uliofuata yaani mwaka jana.
Kufuatia hatua ya Marekani na Israel ya kujiondoa katika Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran Muhammad Javad Zarif ameandika katika mtandao wa Twittwer kwamba: Baada ya kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, makubaliano ya biashara huru kaskazini mwa America (NAFTA), Mkataba wa Biashara ya Pacific na makubaliano ya hali ya hewa ya Paris.. sasa je, kuna kitu kingine kilichobakia ambacho serikali ya Donald Trump na utawala kibaraka wake (Israel) zinataka zijiondoe ndani yake? Labda sasa wote wawili wajiondoe katika sayari ya dunia!!
Marekani ilishurutisha kufanyika marekebisho ya kimsingi katika UNESCO ili ibakie katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa hususan marekebisho katika turathi za kimataifa za shirika hilo ambazo zinayatambua maeneo matakatifu ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu kuwa ni turathi za Kiislamu na Kipalestina, tofauti na matakwa ya Wazayuni wa Israel. Kepewa uanachama Palestina katika shirika la UNESCO pia ni miongoni mwa sababu kuu za kujiondoa Marekani katika shirika hilo. Marekani na Israel zinapinga vikali suala la Palestina kupewa uanachama katika Umoja wa Mataifa na zinawataka viongozi wa Palestina waketi kwenye meza ya mazungumzo na Israel kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa hitilafu zao badala ya kutumia ukumbi wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo na licha ya upinzani mkubwa wa Marekani na Israel, Wapalestina wamefanikiwa kupata uanachama kamili katika shirika la UNESCO na hivyo kupiga hatua muhimu katika njia ya kutambuliwa rasmi katika Umoja wa Mataifa.
Hitilafu baina ya Marekani na Israel kwa upande mmoja na shirika la UNESCO katika upande mwingine zilianza mwaka 2011 wakati shirika hilo lenye makao yake makuu mjini Paris, Ufaransa lilipokubali uanachama wa Palestina katika jumuiya hiyo.
UNESCO pia ilipasisha maazimio kadhaa yanayotambua haki za kihistoria za Palestina na kuilaani Israel kutokana na kupotosha uhakika wa kihistoria. Kwa mfano tu mwaka 2016 UNESCO ilikanusha madai ya kuwepo uhusiano wa aina yoyote baina ya Uyahudi na Msikiti wa al Aqsa na vilevile baina na Uyahudi na Ukuta wa Buraq (Western Wall), na mwaka 2017 iliutambua mji wa Quds (Jerusalem) kuwa ni mji mkuu wa Palestina.
Sambamba na hayo shirika hilo la Umoja wa Mataifa pia limechukua hatua kadhaa za kutaka kuiridhisha Marekani na Israel ili zisijiondoe katika shirika hilo. Miongoni mwa hatua hizo ni kuanzisha kituo cha utamaduni cha kufafanua tukio la Holocaust na mradi wa kukabiliana na eti chuki dhidi ya Wayahudi (Antisemitism). Hata hivyo inaonekana kuwa, hatua hizo hazikuweza kuzishawishi Marekani na Israel na kuzizuia kujiondoa katika shirika la UNESCO.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema amesikitishwa sana na uamuzi wa Marekani kwa kujiondoa katika shirika la UNESCO. Taarifa ya Guterres imesema: Uamuzi wa Donald Trump wa kuiondoa Marekani katika UNESCO unasikitisha sana kwa kutilia maanani mchango muhimu wa nchi hiyo katika shirika hilo tangu lilipoasisiwa.
Hali ya mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) na Haram ya Msikiti wa al Aqsa imekuwa ikizusha hitilafu kwa miaka mingi. Umoja wa Mataifa unatambua maeneo hayo kuwa yanakaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel na imeutaka utawala huo urejee katika mipaka ya kabla ya vita vya siku sita baina ya Waarabu na Israel mwaka 1967. Mkabala wake, utawala ghasibu wa Israel unataka Baitul Muqaddas (Jerusalem) itambuliwe kuwa ni mji mkuu wa dola la Kiyahudi.
Shirila la UNESCO kwa kutegemea nyaraka za historia na rai za aghlabu ya wanachama wake, ilitangaza kuwa, Msikiti wa al Aqsa sio wa Wayahudi. Nchi 58 wanachama wa UNESCO isipokuwa Marekani zilipigia kura na kupasisha uamuzi huo. Wakati huo televisheni ya Israel ilidai kuwa, kupasishwa uamuzi huo wa UNESCO kutakwamisha mwenendo wa kurejesha amani baina ya Wapalestina na Israel. Baada ya hapo UNESCO ilitangaza kuwa, Israel haina haki yoyote katika mji wa Baitul Muqaddas. Taarifa ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa ilisisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unakiuka sheria za kimataifa huko Baitul Muqaddas na Ukanda wa Gaza na kuitaja Israel kuwa ni dola ghasibu.
Azimio hilo pia liliitaka Israel irejeshe udhibiti wa Msikiti wa al Aqsa katika hali ya kabla ya mwaka 2000 wakati eneo hilo takatifu lilipokuwa chini ya usimamizi wa Idara ya Waqfu ya Jordan. Azimio hilo pia lililaani vikali ujenzi wa nyumba, barabara makhsusi za Wayahudi na ujenzi wa ukuta wa kutenganisha eneo la kale la mji wa al Khalil (Hebron). Vilevile UNESCO imesisitiza udharura wa kukomeshwa ukatili wa kupanga na uchochezi unaofanywa na walowezi wa Kiyahudi dhidi ya Wapalestina hususan watoto na wanafunzi. Vilevile iliitaka Israel itekeleze maamuzi na maamizio yake ya awali.
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa katika miaka ya hivi karibuni pia limekuwa likilaani mara kwa mara uchimbaji wa mashimo unaofanywa na Israel katika eneo la Mashariki mwa mji wa Baitul Muqaddas na kutangaza kuwa, mienendo ya Israel kuhusu eneo la Gaza, makaburi ya kale ya mji wa al Khalil na huko Bait Lahm (Bethlehem) inakiuka sheria za kimataifa.
Mkutano wa 41 wa Kamati ya Turathi za Kimataifa ya UNESCO uliofanyika mwezi Julai mwaka 2017 katika mji wa Kraków nchini Poland uliutambua mji wa al Khalil (Hebron) huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu kuwa ni turathi ya kimataifa na kulaani hatua zinazochukuliwa na Israel katika mji huo. Israel ilivamia na kukalia kwa mabavu mji wa al Khalil na maeneo ya kandokando ya Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan, mashariki mwa Baitul Muqaddas na Ukanda wa Gaza katika vita vya mwaka 1967.
Mji wa al Khalil ambao ndio mkubwa zaidi wa Ukingo wa Magharibi uko umbali wa kilomita 30 kusini mwa Baitul Muqaddas. Mji huo wenye historia kongwe una jamii ya Waislamu karibu laki mbili. Katika miaka ya hivi karibuni utawala wa Kizayuni wa Israel umejenga vitongoji vya Wayahudi karibu na mji huo wa kihistoria, suala linalozidisha hatari ya kuharibiwa turathi zake za kale. Azimio la UNESCO limesisitiza tena utambulisho wa Kiislamu wa eneo la kale la mji wa al Khalil (Hebron).
Mji huu wenye umri wa miaka elfu 6 ndio wa kale zaidi kati ya maeneo yote ya Palestina na unaheshimiwa na dini zote za mbinguni. Eneo takatifu zaidi na turathi muhimu kuliko zote za mji huo ni Haram ya Nabii Ibrahim al Khalil (as). Mji huo una majengo mengi ya kale yakiwemo makaburi ya Nabii Ibrahim, Is'haq, Yaaqub na wake zao. Kwa msingi huo unatambuliwa kuwa ni mji mtakatifu kwa wafuasi wa dini zote za mbinguni.
Pamoja na hayo na licha ya ushahidi na yaraka zote hizo za kihistoria na kisheria, mwaka 2017 serikali ya Marekani iliitambua rasmi Quds kuwa ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel licha ya sheria za kimataifa kuutambua mji huo kuwa ni eneo linalokaliwa kwa mabavu. Kwa miaka mingi jumuiya mbalimbali za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa zimekanusha madai ya Israel na kutangaza waziwazi kwamba, eneo la mashariki la Quds ni ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Tangazo la serikali ya Donald Trump la kuutambua mji wa Quds kuwa eti ni mji mkuu wa Israel limepingwa na jamii ya kimataifa. Hivyo tunaweza kusema kuwa, kujiondoa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika shirika la UNESCO ni maonyesho tu ya kisiasa yanayoambatana na makelele ya baadhi vyombo vya habari.