Sep 16, 2018 10:27 UTC
  • Maswali Kuhusu Tukio la Ashura (2)

Je, tukio la Ashuraa na mauaji ya mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika siku ya tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria lina umuhimu katika utamaduni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia peke yao? Au la, madhehebu nyingine za Kiislamu pia kama madhehebu za Ahlusunna, zinajali sana tukio hilo na kuumizwa mno na masaibu ya Hussein bin Ali na dhulma zilizofanywa na madhalimu dhidi ya familia hiyo ya Mtume?

Siku moja wakati Hussein alipokuwa ameketi kwenye mabega ya babu yake, yaani Mtume Muhammad (saw) akicheza, Mtume alimshika na kumbusu kisha akasema: Husseini ni kutokana na mimi, na mimi natokana na Hussein. Mwenyezi Mungu ampende anayempenda Hussein." Mke mwema wa Mtume (saw), Ummu Salama radhi za Allah ziwe juu yake, ananukuu kwamba: Siku moja Hussein alipokuwa kwa Mtume, ghafla nilimuona mtukufu huyo akilia machozi. Nilimuuliza sababu ya kulia kwake. Mtume (saw) alijibu kwa kusema: Ewe Ummu Salama! Malaika Jibrail alikuwa hapa pamoja na mimi na Hussein na akaniuliza je, unampenda Hussein? Nilimwambia ndiyo ewe Jibrail. Alisema: Lakini umma wako utamuua katika ardhi ya Karbala baada yako wewe. Kisha Mtume (saw) alinipa fundo la mchanga wa ardhi ya Karbala."

Hadithi hii imepokewa kwa wingi katika vitabu vya wanazuoni wa madhehebu za Shia na Suni.   

Japokuwa kumuashiki na kumpenda Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) na maumivu ya kukumbuka mauaji ya mjukuu huyo wa Mtume (saw) vimevuka mipaka ya kijiografia na kidini, lakini tukio hilo la tarehe 10 Muharram lina maana nyingine kabisa kwa Shia na wafuasi wa Watu wa Nyumba tukufu ya Mtume wanaomtambua Hussein kuwa ni kiongozi na Imamu wao wa tatu kati ya maimamu 12 waliokuja baada ya Mtume (saw). Imam katika utamaduni wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ndio njia pekee ya kutuelekeza kwa Mwenyezi Mungu SW baada ya Mtume wake na kwa mujibu wa aya ya Tat'hir (aya ya 33 ya Suratul Ahzab), Imam anapaswa kuwa maasumu na mtu asiyetenda dhambi na makosa.

Jina la Shia limefungamana kikamilifu na jina la Hussein na siku ya Ashuraa. Kwa msingi huo yumkini likajitokeza swali kwa baadhi ya watu kwamba, je tukio la Ashuraa yaani siku ya tarehe 10 Muharram mwaka 61 katika ardhi ya Karbala linapewa umuhimu katika utamaduni na madhehebu ya Waislamu wa Shia pekee? Na je madhehebu nyingine za Kiislamu yaani madhehebu za Kisuni hazijali wala kutilia maanani tukio la kuuawa shahidi mjukuu huyo wa Mtume Muhammad (saw) na dhulma walizofanyiwa watu wa familia ya mtukufu huyo?   

Ahlusunna wamenukuu hadithi na riwaya nyingi katika vitabu vyao kuhusu nafasi ya Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein (as) na matukio ya siku ya Ashuraa. Aghlabu ya maulama wakubwa wa Ahlusunna wameeleza mapenzi yao kwa Ahlulbait wa Mtume (saw) na wanamtaja Imam Hussein kuwa Amiin, Siddiq na mtu adhimu na mwenye daraja ya juu. Wasomi hao wanaitaja harakati ya mapambano ya Imam Hussein kuwa ilikuwa harakati ya haki, na wanamtambua Yazid bin Muawiya kuwa alikuwa mtu fasiki, muovu, dhalimu na mal'uni kutokana na aliyofanya kwa familia na wajukuu wa Mtume Muhammad (saw). Miongoni mwa maulamaa wanaomtambua Yazid bin Muawiya kuwa ni dhalimu na mlaaniwa ni Ibn Imad, Taftazani na Ibnul Jawzi. Naam, wako baadhi ya wanazuoni ambao japokuwa wanaamini kuwa Imam Hussein alikuwa kwenye haki lakini hawamuoni Yazid kuwa alikuwa mkosa na wanawabebesha watu wengine dhambi ya maafa yaliyotokea Karbala dhidi ya watu wa Nyumba ya Mtume (saw). Aghlabu ya wanazuoni wenye itikadi hii ni wale wa kundi la kiwahabi wanaojaribu kutetea na kuhalalisha maovu yote yaliyokuwa yakifanywa na watawala wa Bani Umayya.

Wanahistoria wakubwa wa Ahlusunna kama Tabari, Bukhari na Dhahabi wanasema katika vitabu vyao kwamba, harakati ya Imam Hussein ilikuwa harakati ya kupigania uhuru, uadilifu na hadhi ya mwanadamu na wanaamini kwamba, Hussein aliwafunza wanadamu somo la kuwa huru na kusabilia nafsi kwa ajili ya Allah na dini yake. Taftazani ambaye ni miongoni mwa magwiji wa elimu ya teolojia wa Ahlusunna anasema: "Haiwezekani kuficha dhulma iliyofanyika kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (saw), kwa sababu viumbe na wanyama wasioweza kusema ni mashahidi wa dhulma hiyo iliyofikia kilele cha ukatili na hata ardhi na mbingu zilikaribia kutoa machozi kutokana na dhulma hiyo, milima ilikaribia kung'oka mahala pale na miamba kukatika vipande vipande. Hivyo, laana za Mwenyezi Mungu zimshukie aliyetenda dhulma na jinai hiyo, aliyeiridhia na kusaidia kutokea kwake. Na adhabu kali ya Akhera iwapate waliofanya uovu huo", mwisho wa kunukuu.  

Sibt Ibnul Jawzi ambaye ni mwanahistoria wa Kisuni wa karne ya 7 Hijria aliulizwa kuhusu suala la kumlaani Yazid bin Muawiya, akajibu kwa kusema: Ahmad bin Hanbal (kiongozi wa madhehebu ya Hanbali) alijuzisha na kuhalalisha kumlaani Yazid; mimi pia simpendi Yazid kutokana na jinai alizomfanyia mwana wa binti wa Mtume Muhammad (saw) (Hussein bin Ali)...

Katika kitabu chake cha Nurul Absar Fii Manaqibi Aalin Nabiyyil Mukhtar «نورالابصار فی مناقب آل النبی المختار(ص, Muumin bin Hassan Shablanji Shaafi'i ambaye ni miongoni mwa maulamaa wakubwa wa madhehebu ya Shafi'i amezungumzia matukio na yaliyojiri siku ya Ashuraa, dhulma alizotendewa Imam Hussein na wajukuu wengine wa Mtume (saw), matukufu yake na kadhalika. Vilevile amezungumzia karama zilizotokea kuhusu kichwa kilichokuwa kimekatwa na kuchinjwa cha Imam Hussein (as). Kitabu hicho miaka ya huko nyuma kilikuwa kikipatikana kwa wingi na kuwekwa kandokando ya Qur'ani kwenye misikiti mingi ya Ahlusunna lakini kiliondolewa misikitini na kwenye vituo vingi baada ya mawahabi kudhibiti maeneo mengi ya kidini ya Waislamu.

Ibnul Imad Hanbali ameenda mbali zaidi na kuwatambua watu waliomuua kinyama mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein bin Ali kuwa ni makafiri wanaostahiki kulaaniwa. Ameandika katika kitabu cha Shadharatun Min Dhahab kwamba: Mtu aliyeamuru kuuawa Imam Hussein (ra), aliyemuua, aliyehalalisha mauaji hayo na kutayarisha njia na mazingira ya kuuawa kwake, wote ni makafiri wanaostahiki kulaaniwa".

شذرات من ذهب / ابن العماد الحنبلی: ۱ / ۶۸."

Ibnu Kathir anasema katika kitabu cha al Bidaya Wannihaya juzuu ya 8 ukurasa wa 238 kwamba: "Kwa hakika Yazid alikuwa kinara wa ufuska, kafiri na anayestahiki kulaaniwa."

Al Mas'udi anasema katika kitabu cha Murujud Dhahab kwamba: Yazid (bin Muawiya) alikuwa mtu dhalimu na fasiki na alihusika na mauaji ya mjukuu wa Mtume (saw) na masahaba zake, Mwenyezi Mungu awaridhie. Alikuwa akinywa pombe na kulewa waziwazi na kuketi na mbwa. Tabia zake zilikuwa kama za Firauni japokuwa Firauni alikuwa na tadbiri na insafu zaidi kuliko Yazid…". مروج الذهب : ۳ / ۸۲

Maulamaa wengine wengi wakubwa wa madhehebu ya Suni kama Qadhi Abu Yaala, Jalaluddin Suyuti, Ibn Hazm, Shaukani na Sheikh Muhammad Abduh pia wanamtambua Yazid kuwa alikuwa kafiri na fasiki na kwamba anastahiki kulaaniwa.

Tunapopitia kwa haraka haraka mitazamo ya maulama wa madhehebu za Suni tunaona kuwa, wengi miongoni mwao walisikitishwa mno na masaibu ya Imam Hussein katika siku ya Ashuraa na kumtambua Abu Abdillah Hussein bin Ali (as) kuwa alikuwa katika njia ya haki. Wafuasi wa maulama na wanazuoni hao pia walifuata nyayo zao na kuhuzunishwa mno na mauaji ya kutisha ya mjukuu huyo wa Mtume.

Kinyume chake, uwahabi ambalo ni tope lililojitokeza baadaye na wala si dhehebu la Kiislamu, una fikra za kiumawi na kiyazidi na unafanya jitihada za kueneza fikra hizo baina ya Waislamu na kuziuza kama fikra za wafuasi wa madhehebu za Suni. Wafuasi na vinawa wa kundi hilo la kiwahabi wanafanya kila wawezalo kulieleza tukio la Ashuraa na mauaji ya Imam Hussein bin Ali (as) kuwa ni suala linalowahusu Waislamu wa madhehebu ya Shia pekee na kwa njia hiyo wanapotosha falsafa na malengo ya harakati ya kimapinduzi na kimageuzi ya mtukufu huyo. Vilevile uchache wa maarifa ya historia sahihi ya Uislamu na mafundisho ya dini kwa ujumla umewafanya baadhi ya Waislamu watekwe na itikadi hizo za kundi la kiwahabi kuhusu harakati ya Imam Hussein na masuala mengine mengi.

Tunamalizia makala hii kwa tarjumi ya baadhi ya mashairi yaliyotungwa na kusomwa na Imam Shafi'i kuhusu mauaji ya Imam Hussein bin Ali (as).

Kiongozi huyo wa madhehebu ya Shafi'i anasema katika baadhi ya beti za shairi hilo kwamba: Tukio la Ashuraa na siku ya mauaji ya Hussein linanikosesha usingizi na kunizeesha kwa kutia mvi nywele zangu.

Nani atafikisha risala yangu kwa Hussein, japo zipo nafsi zitakazochukia?

Alichinjwa bila dhambi yoyote, na kanzu yake ikafanywa nyekundu kwa damu yake.

Inastaajabisha kuona tukimswalia Mtume Muhammad, na wakati huo huo tunawapiga vita watoto wake.

Kama dhambi yangu mimi ni kuwapenda Ahlubaiti wa Mtume, basi hiyo kwangu ni dhambi ambayo kamwe sitatubia. Wao ni shufa'a na waombezi wangu Siku ya Kiyama ...

Tags