Oct 19, 2022 08:57 UTC
  • Tafakuri katika matukio ya hivi  karibuni nchini Iran (2-Kuigawa Iran, lengo kuu la kistratijia la maadui)

Moja ya malengo ya kistratijia ya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu tangu ushindi wa mapinduzi hayo Februari 1979 limekuwa ni kuuangusha mfumo wa Kiislamu na kuigawa Iran.

Maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wamekuwa wakitumia kila fursa inayojitokeza kutoa pigo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kiwango hiki cha uadui na njama za kutaka kuipindua serikali halali iliyochaguliwa na wananchi hakijawahi kuonekana popote pale duniani. Serikali na mapinduzi mengi duniani yameporomoka au kukengeuka kutoka kwenye njia na malengo yao ya awali na asili kwa kutekelezwa tu moja ya kumi ya uadui na njama kama hizo, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu imefanikiwa kukabiliana na uadui wote huo na kuendelea na njia yake ya kufikia malengo yake aali na matukufu.

Kadiri Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavyozidi kufifisha na kuzima moto wa njama za maadui zake za kutaka kuidhoofisha na kuigawanya Iran na kuendelea kuwa imara zaidi ndivyo juhudi za maadui za kuihujumu na kutoa pigo dhidi yake zinavyozidi kuongezeka. Matukio ya hivi karibuni nchini Iran na vita laini vya vyombo vya habari vinavyofanywa na Marekani, nchi za Ulaya na Kiarabu pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel ili kuchochea machafuko nchini Iran ni muendelezo wa njama zao katika kipindi cha miaka 43 iliyopita kwa madhumuni ya kutoa pigo dhidi ya Iran. Cheche za kwanza za kuvuruga usalama na kutaka kuigawa ardhi ya Iran zilizuka siku chache baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo Februari 1979 ambapo mikoa ya mpakani ya Iran ilifanywa kuwa kitovu cha shughuli za makundi yanayotaka kuigawa Iran katika maeneo kadhaa ya kikabila na yanayopinga Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa hakika mapinduzi ya Kiislamu ya taifa hili yalikuwa yangali machanga, na watu wakishiriki katika kura ya maoni ili kubainisha aina ya serikali waliyoitaka, wakati cheche za shari na ukosefu wa usalama zilipopamba moto miongoni mwa makabila na maeneo ya mpakani. Maeneo ya Turkmen hadi Kurdistan na Khuzestan hadi Azabajani yaligeuzwa kuwa ya uchochezi wa kikabila na harakati za kutaka kujitenga na magenge ya wauaji ambao waliua watu kikatili kwa madai eti ya kutetea haki zao za utaifa. Cheche hizo za fitina zilizoibuliwa na wachochezi wa vita vya ndani na wanaotaka kujitenga zilikuwa bado hazijazimika ambapo ghafla kulijitokeza dikteta mwendawazimu na asiye na busara nchini Iraq na kutekeleza njama ya uchokozi na umwagaji damu mkubwa hapa nchini. Dikteta huyo, Saddam ambaye alipata uungaji mkono mkubwa na wa pande zote wa nchi fasidi za Magharibi na Mshariki na vilevile za watawala wenye fikra mgando wa Kiarabu katika Mashariki ya Kati, ukiwemo wa kifedha, silaha na kisiasa katika asasi za kimataifa, na huku jamii ya kimataifa na mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu yakiwa yamenyamaza kimya na kufumbia macho uchokozi huo, dikteta huyo alishambulia bila kusita ardhi ya kusini na magharibi mwa Iran, akidhani kuwa angeweza kufikia ndoto yake eti ya kuuteka mji mkuu wa Iran, Tehran, katika kipindi cha wiki moja na hivyo kuyasambaratisha Mapinduzi machanga ya Kiislamu.

Lakini baada ya miaka minane ya vita vya hamasa vya watu wa Iran dhidi ya hujuma ya utawala wa dikteta Saddam na waungaji mkono wake wa Magharibi na Mashariki, Iran shupavu na yenye nguvu ilidhihiri katika eneo la Magharibi mwa Asia kuliko ilivyokuwa kabla ya vita. Vijana wa Kiirani wenye tajiriba ya miaka minane ya vita na wenye ari madhubuti kuliko miaka ya vita vya kujitetea kutakatifu, walichukua hatua kubwa zaidi kuelekea maendeleo na ustawi wa Iran katika nyuga mbalimbali za kiuchumi, kisayansi na kijeshi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi zenye viwango vya kwanza katika eneo la Asia Magharibi na dunia katika nyanja nyingi za sayansi, viwanda, anga na anga za mbali, nyuklia na masuala ya kijeshi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefikia kiwango cha kuzuia hujuma ya adui kiasi kwamba hakuna nchi yoyote inayoweza kuthubutu kuivamia Iran kwa sasa. Kwa msingi huo, maadui wamebadilisha mbinu za uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wanatumia visingizio mbalimbali visivyo na msingi kama vile eti kutetea haki za binadamu na kueneza uwongo kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran na kuiwekea vikwazo vikali vya kiuchumi kwa madhara ya wananchi wa kawaida hasa wagonjwa wanaougua magonjwa sugu nchini.

Katika moja ya hotuba zake, Ayatullah Khamenei ameashiria nukta muhimu kuhusiana na suala hilo na kusema kwamba katika miaka yote ya hamasa na umwagaji damu ambapo watu wa taifa hili walikuwa wakishughulika na suala la kutetea nchi yao, wanaodai kutetea haki za binadamu waliwawekea vikwazo vikali na vya kikatili bila kujali lolote ili kuwashinikiza wawachane na njia yao tukufu ya kutetea Uislamu na thamani za Kiislamu. Baada ya kumalizika vita na kuadhibiwa adui mchokozi, maadui walianzisha duru mpya ya vita vya kiuchumi na vikwazo dhidi ya Iran ili kulipigisha magoti taifa hili shupavu. Lakini bado hawakuweza hadi walipokubali na kukiri hivi karibuni kushindwa kwa mradi wao wa kutumia vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa la Iran.

Mnamo mwaka 2018, rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump aliitoa nchi hiyo katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia kati ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama pamoja na Ujerumani, na kuweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran. Hatua hizo za serikali ya Marekani ni ugaidi wa wazi wa kiuchumi dhidi ya taifa la Iran. Vikwazo hivyo vilizuia hata kuingizwa nchini dawa za wagonjwa. Mamia ya wagonjwa wanaougua magonjwa sugu walikufa kutokana na vikwazo hivyo. Lengo la adui ni kuvunja moyo  wa mapambano na uvumilivu wa wananchi wa Iran. Ayatullah Khamenei anasema kuhusu suala hilo kwamba: "Jitihada zote za ulimwengu wa leo wa kimaada na kiistijbari - yaani serikali hizi zenye kiburi zinazodhibiti uchumi na silaha duniani, na hata katika hali nyingi, utamaduni wa nchi nyingi - ni kubabaisha akili na busara popote pale palipo na upinzani dhidi yake. Kubabaika mbele ya adui ni jambo baya na kosa kubwa zaidi. Adui lazima azingatiwe katika mazingira ya uadui anaofanya; yaani hatupasi kumpuuza na kumchukulia kuwa si chochote wala lolote bali tunapasa kuwa waangalifu na kusimama imara mbele yake. Hatupasi kuogopa wala kubabaika mbele yake. Ni wazi kuwa adui anataka kuzibabaisha jamii."

Licha ya kukabiliwa na mashinikizo makubwa ya kiuchumi na kimaisha, lakini wananchi wa Iran wamefanikiwa kupunguza sehemu kubwa ya vikwazo hivyo. Pamoja na hayo, huo sio mwisho wa mgogoro kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya na Iran. Lengo lao kuu ni kuibua mgawanyiko katika jamii ya Iran na kuweka pengo kati ya watu wa Iran, hasa kati ya kizazi cha vijana na serikali. Lengo lao sio tu kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu, bali pia kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuisambaratisha Iran. Ayatullah Khamenei anasema: “Hawaipingi Jamhuri ya Kiislamu tu, bali wanaipinga Iran nzima. Marekani inapinga Iran yenye nguvu, Iran iliyo huru. Hoja na mijadala yao yote inahusu Jamhuri ya Kiislamu. Bila shaka wana chuki kubwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, hapana shaka juu ya hilo, lakini hata bila ya Jamhuri ya Kiislamu wanapinga Iran yenye nguvu, wanapinga Iran iliyo huru. Wanapenda sana Iran ya wakati wa Pahlavi ambayo ilikuwa ng'ombe wa kukamwa maziwa na kutii amri zao. Mfalme huyo alikuwa akilazimika kumuita balozi wa Uingereza au Marekani na kuwataka wampe ushauri na maoni yao kabla ya kuchukua uamuzi wowote ule muhimu nchini! Je, taifa la Iran linawezaje kuvumilia udhalili na aibu hii? Hivyo ndivyo wanavyotaka; Wanapinga Iran."

Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameanzisha vita vikubwa vya vyombo vya habari na propaganda dhidi ya Iran kwa kutumia fursa na hali zote zilizopo ikiwemo mitandao ya kijamii. Hali yoyote, ikiwemo ya kifo cha msichana mdogo, inaweza kuwa kisingizio cha kuibuliwa machafuko nchini. Hapana shaka kuwa nchini Iran kuna hali ya malalamiko kuhusu utendaji wa serikali na hali ya kiuchumi nchini. Kuna malalamiko kama hayo kuhusu utendaji wa serikali na hali ya kiuchumi katika nchi nyingine pia. Nchi hizo hizo za Ulaya zinakabiliwa na maandamano makubwa na migomo kutokana na mfumuko wa bei na hali mbaya ya kiuchumi. Lakini hakuna hata moja ya nchi hizo inayokabiliwa na ukosoaji wa serikali za kigeni kuhusu maandamano hayo.

Marekani, Kanada na nchi nyingi za Ulaya hujifanya kama yaya aliye na huruma kuliko mama mzazi kwa mwanaye kwa kukosoa na kulaani juhudi zinazofanywa na vikosi vya kulinda usalama kwa ajili ya kurudisha amani na usalama katika pembe tofauti za Iran na kuchukua misimamo ya kuingilia na kuibua migogoro ya kijamii na kisiasa nchini. Hii ni katika hali ambayo nchi hizo zinastahili kukosolewa kuliko nchi nyingine yoyote kwa vitendo vyao vya kinyama dhidi ya ubinadamu. Katika miezi ya hivi karibuni, makaburi ya halaiki ya watoto wa makabila ya kiasili yaligunduliwa nchini Kanada, jambo ambalo liliumiza moyo wa kila mwanadamu aliye huru. Katika hali hiyo, Waziri Mkuu wa Kanada ametisha na kuiwekea vikwazo Iran kwa kisingizio cha kifo cha binti mmoja wa Kiirani. Sasa mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa la kubuni na kuibua migogoro nchini Iran. Mitandao hiyo inaweza kutumika kama mahali pazuri pa kubadilishana mawazo na maoni kuhusu namna ya kurahisisha biashara na maisha ya watu. Lakini serikali za Magharibi zinatumia vibaya mitandao hiyo kama wenzo wa kubuni na kuibua migogoro na uvumi miongoni mwa tabaka la vijana wa Iran ili kuwachochea wakabiliane na serikali. Bila shaka taifa la Iran hususan kizazi cha vijana shupavu wa Iran mara hii pia litaweza kuvuka kwa mafanikio kipindi hiki kigumu cha fitina na uchochezi wa serikali za Magharibi.

Tags