Feb 06, 2023 10:55 UTC
  • Alfajiri Kumi; Mapinduzi ya Kiislamu na mafanikio ya kiuchumi

Katika kipindi cha leo, tutaangalia kwa kifupi mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana nchini Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na hasa katika uwanja wa nishati.

Hamjambo wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhutri ya Kiislamu ya Iran. Tumo katika siku za maadhimisho ya Alfajiri Kumi za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Huku tukikupongezeni kwa mnasaba wa siku hizi za mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu, tutatizama kwa ufupi mafanikio makubwa yaliyoletwa na Mapinduzi katika uwanja wa uchumi na hasa nishati.

*********

Ili kuwa na picha sahihi ya mafanikio ya Mapinduzi katika uga wa uchumi, ni lazima turudi nyuma kidogo katika miongo iliyopita na hasa siku za mwisho za utawala wa kitaghuti wa Pahlavi nchini Iran. Wakati wa utawala wa Shah, uchumi wa Iran ulikuwa uchumi wa kutegemea bidhaa moja na hasa mauzo ya mafuta. Mamilioni ya mapipa ya mafuta yasiyosafishwa yalisafirishwa nje ya nchi kila siku kwa ajili ya kuagiza nchini bidhaa za matumizi ya kawaida, zilizogharimu mamia ya mamilioni ya dola. Moja ya matukio muhimu zaidi ya kiuchumi yaliyotokea katika muongo wa mwisho wa utawala wa Shah (miaka ya 50 Shamsia Hijiria) ilikuwa ni ongezeko kubwa la bei ya mafuta na ukuaji wa mauzo ya mafuta nje ya nchi. Kwa kadiri kwamba mapato ya mafuta yalifikia karibu asilimia 86 mwaka 1974 ikilinganishwa na jumla ya mapato ya serikali. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mnamo 1968, mapato ya mafuta hata hayakufikia dola bilioni moja, lakini mnamo 1977, yalifikia zaidi ya dola bilioni 20. Pamoja na hayo, lakini utajiri huo haukuwa na faida yoyote chanya katika maisha ya watu wala ustawi wa nchi. Francis Fitzgerald, mwandishi wa Marekani, aliandika katika miaka hiyo kwamba: “Shah hajawahi kufanya jitihada za dhati za kuendeleza nchi... utajiri wa nchi umetumika zaidi katika kununua magari yake binafsi na si kwa ajili ya kununulia mabasi ya usafiri wa umma, bidhaa za matumizi ya kawaida na si kwa ajili ya afya ya umma, na kwenye mishahara ya askari na polisi na si kugharamia mishahara na matumizi ya walimu."

*************

Kinachoweza kusemwa kuhusu hali ya kiuchumi ya Iran katika miaka hiyo (miaka ya 1970) ni kwamba mipango ya kiuchumi ya utawala wa Shah, bila ya kujali hali halisi ya jamii, hatimaye ilipelekea kusambaratika uchumi wa Iran. Kwa kuwa uchumi wa Iran ulitegemea sana mafuta, na kufuatia kushuka  bei ya mafuta katika miaka miwili ya mwisho ya utawala wa Shah (1976-1978), serikali ilikabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti kadiri kwamba ilianza kukopa na hatimaye kukabiliwa na matatizo kama vile uhaba wa wafanyakazi wenye utaalamu na uzoefu, mitandao ya mawasiliano kama vile barabara na bandari, ukosefu wa umeme, wawekezaji kukimbia nchi, mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira, nyumba za makazi na kadhalika. Mgao usio wa kiadilifu wa mapato na utajiri wa nchi kati ya maeneo ya mijini na vijijini, na vile vile kati ya matabaka mbalimbali ya watu, uliacha pengo kubwa la kitabaka kati ya matabaka mbalimbali ya jamii. Kwa utaratibu huo na licha ya kuongezeka bei ya mafuta katika masoko ya mafuta kimataifa na hilo kuongeza matumaini ya wananchi kwamba maisha yao yangeboreka kutokana na mauzo ya mafuta, lakini hilo halikutimia kutokana na siasa mbovu za utawala tegemezi wa Shah ambao ulishindwa kutumia fedha nyingi zilizopatikana kutokana na mauzo ya mafuta kwa ajili ya kuboresha maisha ya wananchi na uchumi wa nchi.

Katika kuchambua hali ya uchumi wa Iran katika kipindi hicho, Andrew Duncan, mwandishi wa kitabu cha "The Robbery of Iran, Money Rush", anachambua hali ya kiuchumi ya Iran katika kipindi hicho na kusema kwamba mipango ya kiuchumi isiyo ya busara ya Shah ilitokana na ujinga wake pamoja na washauri wake ambao hawakuifahamu vizuri jamii ya Iran. Anasema katika sehemu ya kitabu hicho: "Shah alifikiri kwamba kila kitu kinawezekana kupitia pesa. Siku moja mnamo Agosti 1974, ghafla aliwaita wajumbe wa baraza lake la mawaziri na kutangaza kwamba alitaka bajeti ya mpango wa tano wa maendeleo (1973-78) iongezwe maradufu, yaani kutoka dola bilioni 35 na milioni 500 hadi dola bilioni 68 na milioni 800. Ukweli kwamba hakukuwa na wataalamu na wajuzi wa kutosha wa kuweza kutekeleza mpango mkubwa kama huo haukumshughulisha Shah. Kwa mfano, alitangaza kwamba watoto wote wanapaswa kwenda shule na kusahau kuwa kufanya hivyo kulihitaji kwa uchache walimu 30,000. Kuhusu hilo, Huwaida, Waziri Mkuu wake pia ilisema kijinga kuhusu changamoto hiyo: Ni sawa tu, tutafundisha kila mwanafunzi kupitia televisheni huku akisahau ukweli kuwa vijiji 65,000 nchini Iran havikuwa na umeme kabisa."

**********

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo Februari 1979 uliibua matumaini makubwa katika nyoyo za watu. Licha ya mashinikizo makubwa yaliyotolewa na maadui kwa ajili ya kupunguza kasi ya harakati ya Mapinduzi ili kuizuia Iran kufikia malengo yake matukufu, kama vile miaka minane ya vita vya kulazimishwa na kisha kuiwekea vikwazo vikali zaidi, juhudi kubwa zimefanyika nchini katika miongo minne iliyopita kwa lengo la kuuweka uchumi wa Iran katika njia na mwelekeo sahihi wa maendeleo. Uadilifu una nafasi muhimu katika mafundisho ya Uislamu. Kwa mujibu wa Aya za Qur'ani, moja ya malengo ya ujumbe wa Mitume Mtukufu (saw) ni kusimamisha uadilifu na usawa baina ya watu. Imepokewa kutoka kwa Amirul Momineen Imam Ali (as) akisema kwamba: “Miji na nchi hazistawi isipokuwa kupitia uadilifu”. Kwa msingi huo, ni wazi kuwa moja ya malengo ya serikali iliyosimama juu ya misingi ya dini ya Kiislamu ni kuiimarisha dini hii tukufu. Moja ya malengo muhimu ya viongozi wa serikali katika miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika uga wa uchumi limekuwa ni kuwapatia wananchi suhula za ustawi na kuboresha maisha yao na kuwaondolea umasikini vijijini na maeneo yaliyoachwa nyuma kimaendeleo. Kabla ya  ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, isipokuwa miji mikubwa na ya kati, miji midogo na vijiji vingi havikuwa na maji safi na salama ya kunywa kupitia mabomba. Katika hali ambayo ni asilimia 12 tu ya wakazi wa vijijini ndio walinufaika na mtandao wa usambazaji maji vijijini katika miaka ya mwisho ya utawala wa Shah (mwaka 1978), kiwango hicho sasa kimefikia zaidi ya asilimia 82.

***********

Leo hii, idadi ya watu wanaotumia maji safi na salama nchini Iran ni mara 8 zaidi ya kabla ya Mapinduzi. Urefu wa mabomba ya usambazaji maji safi sasa ni karibu kilomita elfu 31. Miongoni mwa maelfu ya miradi midogo na mikubwa katika uwanja wa usambazaji maji katika mikoa tofauti ya Iran, tunaweza kuashiria mradi mkubwa wa kuhamisha maji wa Ghadir huko katika mkoa wa Khuzestan, ambao umezinduliwa na kuanza kutumika hivi karibuni. Mradi huu, ambao unasemekana kuwa mradi mkubwa zaidi wa usambazaji maji katika eneo la Asia Magharibi, umetekelezwa katika mkoa wa Khuzestan ulioko kusini-magharibi mwa Iran, mkoa wa tano kwa idadi kubwa ya watu nchini, na unatoa huduma ya maji safi ya kunywa kwa miji 26 na zaidi ya vijiji 1600. Mtekelezaji wa mradi huu ni taasisi ya ujenzi ya Khatam Al-Anbiya, ambayo, kwa kufanya kazi kwa kijituma na kijihadi, usiku na mchana, na kwa kutegemea uwezo wa ndani, wa vijana na wafanyikazi waliobobea, imeweza kukamilisha na kufanikisha mradi huo uliopasa kuchukua miezi 36 katika kipindi kifupi kabisa cha minane pekee.

***********

Mafanikio mengine makubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni katika ujenzi wa mabwawa. Leo hii idadi ya mabwawa ya Iran ikilinganishwa na ya kabla ya Mapinduzi imeongezeka mara kumi zaidi ambapo kwa sasa ina mabwawa yapatayo 195. Mabwawa yana faida na matumizi mengi kama vile kuepusha mafuriko, matumizi ya kilimo, katika viwanda, ufugaji wa wanyama na viumbe vya majini na kadhalika. Moja ya kazi za mabwawa ni kuzalisha umeme unaotokana na nguvu za maji. Asilimia 14.1 ya umeme wa Iran huzalishwa kutokana na mitambo ya maji. Bila shaka, kuna vyonzo vingine tofauti ambavyo vinatumika katika kuzalisha nishati ya umeme nchini. Vyanzo hivyo ni pamoja na gesi, nishati mbadala kama vile vinu vya upepo na jua na vile vile kinu cha nyuklia cha Bushehr. Uwezo wa kawaida wa vinu vya nishati ya Iran unafikia zaidi ya megawati 86,000, jambo ambalo limeiwezesha Iran kuwa moja ya nchi 10 bora katika utengenezaji wa vituo na mitambo ya kuzalisha nguvu za umeme duniani. Mafanikio haya yamepelekea asilimia 100 ya wakazi wa mijini Iran na zaidi ya asilimia  99.5 ya wakazi wa vijijini kunufaika na neema ya umeme. Hii ni katika hali ambayo wastani wa usambazaji umeme vijijini na mijini duniani kwa utaratibu huo ni asilimia 79 na 96. Ni muhimu kutaja hapa kuwa kwa mujibu wa utabiri wa wataalamu, Iran itahitajia megawati elfu 20 hadi 30 za umeme katika miaka ijayo kwa ajili ya matumizi katika nyanja mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na za matumizi ya nyumbani. Gharama ya uzalishaji umeme katika mitambo ya nyuklia ni ndogo. Pia, mitambo hii ya umeme haina uchafuzi wa mazingira kama inavyoonekana katika sekta ya uzalishaji umeme kwa kutumia nishati ya mafuta. Kwa hivyo, uwekezaji katika vinu vya nyuklia kama jambo la dharura, unazingatiwa na kufuatiliwa zaidi na viongozi wa ngazi za juu nchini Iran kuliko wakati mwingine wowote.

**************

Miongoni mwa shughuli nyingine za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa nishati, tunaweza kuashiria maendeleo yaliyopatikana katika uwanja wa uzalishaji mafuta na gesi, pamoja na ujenzi wa viwanda vya petrokemikali nchini. Zaidi ya asilimia 70 ya matumizi ya nishati nchini Iran inahusu gesi asilia. Hivi sasa, zaidi ya asilimia 98 ya miji na asilimia 84 ya vijiji vya Iran vimeunganishwa na mtandao wa gesi asilia. Kuna karibu mashirika elfu 2 ya uchimbaji mafuta yanayojishughulisha na uzalishaji mafuta na gesi na kustawisha visima vya mafuta na gesi nchini. Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, sehemu kubwa ya tasnia hii ilisimamiwa na mashirika ya kigeni, lakini hii leo, wataalamu wa Iran wameweza kutengeneza ndani ya nchi asilimia 80 ya vifaa na vipuri vinavyohitajika katika tasnia hii. Vingi vya vifaa hivyo ni vya kisasa kabisa na vilivyotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya juu. Mashirika 50 yanayozalisha vifaa hivyo yako katika daraja la kimataifa kuhusu ujuzi wa kiufundi, na huuza bidhaa zao katika masoko ya kimataifa. Vile vile juhudi kubwa zinafanyika katika uwanja wa kuongeza viwanda vya kusafisha mafuta na bidhaa za petrokemikali ili kuimarisha uzalishaji wa bidhaa zilizoongezwa thamani na hivyo kupunguza mauzo ya mafuta na gesi ghafi. Leo, idadi ya viwanda vya petrokemikali imeongezeka zaidi ya mara 10 ikilinganishwa na kabla ya Mapinduzi ambapo sasa imefikia viwanda 68. Kwa wastani, kati ya lita milioni 90 na 100 za petroli huzalishwa nchini Iran kila siku. Kiasi hiki kinajumuisha asilimia 27 ya uwezo wa usafishaji mafuta wa Iran, kiwango ambacho ni cha juu kuliko wastani wa dunia na kinaonyesha mafanikio ya Iran katika kuzalisha bidhaa za mafuta zilizosafishwa.

*************

Ndugu wasikilizaji, kwa kuwa muda wa kipindi hiki maalumu umekwisha, tutaendelea kujadili maendeleo ya Iran katika sekta nyingine za kiuchumi wakati mwingine panapo majaaliwa. Hivyo basi hadi wakati huo tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

Tags