Feb 07, 2023 05:32 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu; Qur'ani, Umaanawi na Umoja

Assalamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mnaponitegea sikio wakati huu. Nakukaribisheni kwa moyo mkunjufu kusikiliza mfululizo mwingine wa vipindi hivi maalumu tulivyokuandalieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Alfajiri Kumi za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambapo kwa leo tutazungumzia nafasi ya Qur'ani, Umaanawi, Uongozi wa Imam Khomeini na Umoja wa matabaka mbalimbali ya jamii ya Iran katika kufanikisha mapinduzi hayo. Endeleeni kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Tarehe 11 Februari mwaka 1979 ilitangazwa habari muhimu na ya kushangaza ambayo ilitoa mguso mkubwa kwa watu katika kila pembe ya dunia. Habari yenyewe ni: "Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamepata ushindi na kutamatisha umri wa utawala wa Kipahlavi".

Hata hivyo kulikuwa na sababu kadhaa na tofauti zilizochangia kufanikiwa na kupata ushindi mapinduzi hayo makubwa na ya umma; sababu ambazo kwa kushikamana na kusaidiana kwa pamoja ziliwezesha kuuangusha utawala wa kidikteta wa Kipahlavi, ulioonekana kidhahiri kuwa wenye nguvu na huku ukiungwa mkono kwa kila hali na madola makubwa ya ulimwengu, hasa Marekani. Ukweli ni kuwa, umoja na mshikamano wa wananchi wakakamavu wa Iran wakiongozwa na shakhsia shujaa, mwerevu, mpenda watu na mwenye huruma, ambaye ni Imam Khomeini (MA), ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi zilizochangia kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu. Umoja halisi na wa watu wote, daima huwezesha kupatikana nguvu na matumiani na hatimaye ushindi. Mshikamano na kuwa kitu kimoja Wairan, nao pia ulikuwa na taathira hiyo katika vipindi tofauti vya harakati ya Mapinduzi pamoja na mafanikio na ushindi uliokuja kupatikana. Na ni dhahir pia kuwa, kiongozi wake mkuu alikuwa na nafasi muhimu zaidi katika kuleta na kuimarisha umoja wa wananchi, ambapo katika jumbe na hotuba zake, Imam Khomeini, alikuwa kila mara akiwatahadharisha wananchi juu ya mifarakano na kuhitilafiana. Katika muda wote wa mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala mwovu wa Pahlavi, umoja usiolegalega ndio uliowafanya wananchi hao wawe kitu kimoja, wasaidiane katika shida na matatizo yaliyowakabili na kulifanya taifa lipaze sauti moja ya kutaka utawala huo uondoke.

Umoja imara na madhubuti wa wananchi wa Iran wakati wa vuguvugu la mapinduzi ulitokana na sababu mbili: moja ni watu wote kuchoshwa na kuchukizwa na utawala kandamizi na wa kiimla wa Shah; na nyingine ni imani kubwa waliyokuwa nayo wananchi juu ya Uislamu, uliokuwa fikra kuu na dira iliyoongoza Mapinduzi.

Utambulisho muhimu zaidi wa vuguvugu la mapinduzi ya wananchi wa Iran. Nara na kaulimbiu za wananchi na misimamo iliyokuwa ikibainishwa na kiongozi mkuu wa mapinduzi, Imam Khomeini (MA), vyote hivyo vilionyesha kuwa, harakati hiyo ya taifa la Iran iliyoweka historia, ilitokana na dini na imani safi ya wananchi wake, yaani Uislamu; kiasi kwamba ulipopita mwezi mmoja na nusu tu baada ya ushindi wa mapinduzi, zaidi ya asilimia 98 ya Wairani walioshiriki kwenye kura ya maoni, waliunga mkono kuasisiwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ili nchi yao iongozwe kwa hukumu na tunu za Uislamu.

Uungaji mkono huo mkubwa na usio na kifani, na kwa hakika usiosahaulika ulioonyeshwa na wananchi kwa uamuzi wa kuasisiwa mfumo wa Kiislamu ulidhihirisha wazi kwamba mapinduzi ya Iran, kinyume na mapinduzi mengineyo, yana asili ya umaanawi na Uislamu; na muelekeo na malengo yake yanaendana na mafundisho na thamani za dini hiyo adhimu ya mbinguni. Katika kubainisha nafasi ya dini tukufu ya Uislamu katika kuleta umoja baina ya wananchi wa Iran, Imam Khomeini alisema: "Bila irada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu haiyumkiniki watu kufikia hatua ya kuwa na kalima ya umoja kama hivi".

Japokuwa wananchi wa Iran ni watu wenye imani kubwa ya dini, lakini kitu kilichowafanya wakubali kuifanya imani yao hiyo lengo la piganio tukufu la mapambano yao dhidi ya utawala wa Shah, ni miongozo ya kiongozi wao mpendwa, Imam Khomeini (MA). Kwa kuelewa vyema jinsi wananchi hao walivyokuwa wakiupa umuhimu umaanawi na dini, Imam Khomeini aliwatolea mwito wa kuungana pamoja chini ya mhimili wa mafundisho ya Uislamu yanayopiga vita dhulma na kumkomboa mwanadamu. Tab'an Kiongozi huyo mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliianza kazi hiyo ya uelimishaji umma tangu takriban mwaka 1963 pamoja na wanafunzi wake kadhaa na wanafikra na wanamapinduzi wenzake, kwa kuutambulisha Uislamu kuwa ni dini ya kupambana na dhulma na ubeberu na kutetea wanyonge na wapigania haki na uadilifu. Kwa hakika Imam Khomeini aliwataalamisha watu kwa mafundisho ya kijamii na kisiasa ya Uislamu na kuwasisitizia kuwa, kwa kuyatekeleza mafundisho hayo watapata radhi, auni na msaada wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya uokovu na ushindi wa Mapinduzi, kama inavyoeleza aya ya saba ya Suratu Muhammad ya kwamba: "Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu". 

Wakati wa mapambano yao dhidi ya Shah na hata baada ya ushindi wa mapinduzi, wananchi Waislamu wa Iran walijionea kwa macho yao tena mara kadhaa ishara za auni na msaada wa Mwenyezi Mungu, pale walipotawakal na kumtegemea Yeye na kupiga hatua katika njia yake ya nuru. Maandamano na mikusanyiko mikubwa zaidi ya watu na iliyokuwa na taathira kubwa zaidi, ilifanyika katika minasaba ya kidini hususan ile iliyohusiana na mapambano dhidi ya dhulma na uonevu ya Imam Hussein (AS), mjukuu mtukufu wa Bwana Mtume SAW. Katika siku za Tasua na Ashura pamoja na Arubaini, ambazo zinakumbusha mapambano hayo matukufu ya kidini, yalifanyika maandamano makubwa na ya hamasa, ambayo yalidhihirisha nguvu na umoja wa wananchi wa Iran chini ya kivuli cha mafundisho ya Uislamu ya kupiga vita dhulma, na kumstaajabisha kila mtu.

Tunapozungumzia suala la wananchi wa Iran kufuata mafundisho ya Uislamu, tunazikusudia thamani na hukumu zilizobainishwa ndani ya kitabu cha mbinguni cha Qur'ani. Muujiza huo usio na kifani wa Bwana Mtume Muhammad SAW, ni mwongozo uliokamilika wa amali na matendo ya mtu binafasi na jamii nzima katika nyanja mbalimbali. Mafunzo ya Qur'ani tukufu, yalikuwa daima yakitoa mwanga wa ufumbuzi na kujenga matumaini katika vipindi vigumu vya mapinduzi. Katika kukabiliana na utawala kama wa Kipahlavi, ulioonekana kidhahiri kuwa wenye nguvu na ambao ulikuwa umejizatiti kwa zana za kisasa za kukandamizia raia huku ukiungwa mkono na maajinabi, kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuomba msaada kwake Yeye Mola, kuliwapa wananchi Waislamu wa Iran nguvu za kimaanawi, faraja na tumaini la ushindi. Ndani ya kitabu hicho kitukufu cha mbinguni, wananchi hao walikuwa wakiisoma aya ya tatu ya Suratul-Ahzab isemayo: "Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa". Sambamba na hayo, katika mapambano yao magumu na mazito, wananchi Waislamu wa Iran walitawakali na kutegemea nguvu na uwezo wa Mola Mwenye enzi, aliye Mweza wa kumwangamiza dhalimu yeyote yule; na wakaendesha mapambano yao kwa imani kamili ya bishara ya ushindi aliyowapa Yeye Mola. Hayo yameelezwa kwa uwazi katika aya ya 30 ya Suratu-Fuss'ilat isemayo: "Hakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa".

Imam Khomeini (MA) ambaye alikuwa kiongozi mtajika wa kidini na mfasiri wa Qur'ani, alikuwa akiwahimiza na kuwatia raghaba kila mara wananchi Waislamu wa Iran ya kushikamana na kitabu hicho cha wahyi na kutekeleza mafundisho yake. Kwa kweli Qur'ani, ramani ya njia ya kuasisia jamii inayotamaniwa na iliyokusudiwa na Mapinduzi ya Kiislamu, ni kitabu kilichoteremshwa na Mola mwenye hekima, kisicho na ila wala dosari yoyote. Na ndio maana kiongozi huyo mkuu wa vuguvugu hilo kubwa la umma wa Wairani alikuwa akisisitiza kila mara kwamba, thamani zote za Mapinduzi zimetoka kwenye chemchemi ya maneno ya wahyi. Imam Khomeini alikuwa akisema: "Sisi tumeendesha harakati ili Uislamu na sheria za Uislamu na Qur'ani zitawale ndani ya nchi yetu na kusiwepo na wala haitakuwepo sheria yoyote ya kusimama mkabala na sheria ya Uislamu na Qur'ani". Kwa hakika Imam Khomeini aliyatambulisha mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni harakati iliyofungamana na malengo kama ukombozi, kujitawala na kuongoza kwa matakwa na ridhaa ya wananchi; tab'an kulingana na mafunzo na mafundisho yaliyotukuka na ya asili ya Uislamu, si kwa kufuata vigezo vya Kimagharibi. Kwa maelezo hayo, Jamhuri ya Kiislamu, inatambulika kama mfumo mpya wa uendeshaji utawala kwa mujibu wa umaanawi na mafundisho ya Uislamu na Qur'ani. Na ni kwa sababu hiyo, madola ya kiliberali ya Magharibi yameamua kuipinga vikali na kuipiga vita na kuiwekea mashinikizo kwa visingizio mbalimbali. Hata hivyo malengo matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu yanayotokana na thamani za kidini za Uislamu na Qur'ani, yamegeuka kuwa nuru ya tumaini kwa watu wanaokandamizwa na kwa watu waliochoshwa na maisha ya kujali vitu tu ya umaada na ya ufuska na ufisadi ya Magharibi. Thamani hizi za kimaanawi na zenye kuhuisha nyoyo, hivi sasa zimepenya na kuenea katika jamii nyingi na zingali zinaendelea kusambaa na kupokewa katika kila pembe ya dunia. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/

 

Tags