Nusu ya wakimbizi wa kambi ya Dadaab Kenya kurejeshwa Somalia mwakwa huu
Kamati ya pande tatu inayoshughulikia wakimbizi wanaoishi katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani ya Dadaab nchini Kenya imetangaza kuwa, nusu ya wakimbizi hao watarejeshwa nchini kwao ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2016.
Kamati hiyo imetangaza leo kwamba, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na pande husika, zoezi hilo litafanyika kwa kutumia mbinu za kuhamasisha na kutoa vivutio kwa wakimbizi hao.
Nusu ya wakimbizi wa kambi ya wakimbizi ya Dadaab ambayo ndiyo kubwa zaidi duniani ni Wasomali waliokimbilia Kenya katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Kambi hiyo iko umbali wa kilomita mia moja kutoka kwenye mpaka wa nchi mbili za Kenya na Somalia.
Wakati huo huo kamati ya pande tatu kuhusu wakimbizi wa Somalia inayoundwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohamed, waziri mwenzake wa Somalia Abdisalam Hadliye Omar na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa imekutana na kujadiliana suala la wakimbizi hao na imeunda timu ya utekelezaji sahihi wa mpango wa kurejeshwa nyumbani wakimbizi hao.
Katika upande mwingine Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa lmeitaka Kenya kujiepusha kuchukua hatua yoyote inayopingana na sheria za kimataifa kuhusu wajibu wa kuwalinda watu wenye haja.
Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wakimbizi laki 6 na 23 elfu wanaishi katika kambi za wakimbizi hususan kambi za Dadaab na Kakuma nchini Kenya.