Magaidi 25 wa kundi la al-Shabaab waangamizwa Somalia
Wanachama 25 wa kundi la kigaidi la al-Shabab la Somalia wameangamizwa akiwemo mmoja wa makamanda wao wa ngazi za juu.
Jeshi la Somalia limetangaza kuwa, Wanachama wasiopungua 25 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la nchi hiyo katika mji wa Hiran.
Vyombo vya usalama vya Somalia vimesisitiza kuwa, kuondoka kwa askari wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini humo (ATMIS) hakutaathiri operesheni hizo za kukabiliana na magaidi wa al-Shabab.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni wanachama wasiopungua 60 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab waliangamizwa katika operesheni ya pamoja ya jeshi la Somalia na vikosi vya kigeni kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Kundi la kigaidi la al Shabab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya kila liwezalo kuipindua serikali kuu ya Somalia tangu mwaka 2007; na hadi kufikia sasa kundi hilo limefanya mashambulizi mengi ya kigaidi na kuuwa wanajeshi na raia wengi.

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kilitangaza mwezi Juni mwakka huuu kwamba, kimekabidhi kambi ya kijeshi ya jimbo la Hirshabelle kwa vikosi vya Somalia na hivyo kuanza mchakato wa kuondoa kutoka nchini humo askari wake 2000.
Vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), ambavyo vinajumuisha takriban wanajeshi elfu 20, polisi na raia kutoka nchi za Uganda, Burundi, Djibouti, Ethiopia na Kenya, Aprili 2022 vilichukua nafasi ya vikosi vya AMISOM vilivyotumwa nchini Somalia tangu mwaka 2007 kupambana na uasi wa kundi la kigaidi la Al-Shabab.