Maiti 27 za wahajiri zapatikana jangwani karibu na mpaka wa Tunisia
Mamlaka za Libya zimetangaza habari ya kugunduliwa miili 27 ya wahajiri wa Kiafrika katika jangwa la magharibi karibu na mpaka wa nchi hiyo na Tunisia.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Libya imesema katika taarifa kuwa, uchunguzi wa kubaini utambulisho na uraia wa wahamiaji hao umeanza.
Mohamed Hamouda, Msemaji wa Serikali ya Libya katika mahojiano na shirika la habari la Associated Press amethibitisha habari ya kupatikana maiti hizo za wahajiri, pasi na kutoa maelezo zaidi.
Duru za habari zinaarifu kuwa, wahajiri hao walioaga dunia katika mazingira ya kutatanisha wakiwa jangwani katika mpaka wa Libya na Tunisia ni raia wa nchi za eneo la chini ya jangwa la Sahara barani Afrika.
Hali ya mamia ya wahajiri wa Kiafrika waliokwama katika eneo la mpaka wa Tunisia na Libya inazidi kuwa mbaya baada ya kufukuzwa na mamlaka ya Tunisia kutoka kwenye mji wa Sfax, ambao ni wa pili kwa ukubwa katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Haya yanajiri siku chache baada ya wahajiri wasiopungua 11 kupoteza maisha baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama katika maji wa Bahari ya Mediterrania, pwani ya Tunisia.
Tunisia iko kwenye eneo la katikati mwa Bahari ya Mediterania, na ni moja ya njia kuu zinazotumiwa na wahamiaji haramu wenye tamaa ya kufika barani Ulaya.