Kukataa Misri ombi la Marekani la kuipa silaha Ukraine
Misri imekataa ombi la Marekani la kuipa silaha Ukraine ikiwa ni katika sehemu ya mkakati wa Cairo ya kutopendelea upande wowote kwenye vita vya Ukraine na Russia.
Kwa mujibu wa gazeti la Wall Street Journal la Marekani, viongozi wa Misri wanaendelea kupinga ombi la kung'ang'ania la viongozi wa Marekani ambalo wamekuwa wakilirudia mara kwa mara kwa miezi mingi sasa la kuitaka Misri izalishe risasi za vifaru na silaha nyinginezo na kuipa Ukraine iishambulie Russia.
Viongozi wa White House wanaitaka Misri iipe Ukraine mizinga, makombora ya kupigia vifaru, mifumo ya kujilinda na mashambulizi ya anga na silaha nyepesi ili zitumike katika vita vinavyoendelea hivi sasa huko Ukraine. Kila wakati maafisa wa Marekani wanapoonana na maafisa wa Misri huwa wanatoa ombi hilo ikiwa ni pamoja na wakati wa mazungumzo ya waziri wa ulinzi wa Marekani, Lloyd James Austin na Rais Abdel Fattah el Sisi yaliyofanyika mwezi Machi mwaka huu mjini Cairo. Lakini viongozi wa Misri wamekuwa wakipinga vikali maombi hayo ya viongozi wa Marekani na wamekuwa wakisema waziwazi kuwa hawana nia ya kuipa silaha Ukraine. Pamoja na hayo lakini, viongozi wa Marekani wanajifanya hawajausikia msimamo huo wa viongozi wa Misri. Jared Malsin, mtaalamu na mwandishi wa habari wa nchini Marekani anasema: Kufeli Washington kuishawishi Misri ishirikiane nayo, kumetokea katika kipindi nyeti na hassas cha vita vya Ukraine. Hii ni katika hali ambayo, afisa mmoja wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amedai kuwa ana matumaini Misri itakubali maombi ya Washington ya kuipa silaha Ukraine. Amesema, mazungumzo yanaendelea baina yao na Misri kwa kuzingatia maslahi ya pande mbili na anataraji makubaliano yao yatailazimisha Russia kukomesha vita huko Ukraine.
Amma nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba, Misri ina uhusiano wa jadi na Russia, na hilo ndilo jambo linaloifanya Misri isifikirie kabisa kutekeleza maombi ya Marekani ya kupunguza kiwango cha uhusiano wa Cairo na Moscow au kuipa silaha Ukraine. Mwezi Mei mwaka huu, Marekani iliitaka Misri izuie ndege za kijeshi za Russia zisipite kwenye anga yake, lakini viongozi wa Cairo walilipuuza ombi hilo la Marekani. Ijapokuwa ni kweli Misri ni katika waitifaki wa zamani wa Marekani kiasi kwamba kila mwaka Washington inaipa Cairo zaidi ya dola bilioni moja kwa jina la msaada wa kijeshi, lakini wakati huu wa urais wa Abdel Fattah el Sisi, inaonekana wazi kuwa Misri imekuwa na uhusiano madhubuti zaidi na Russia. Kiujumla ni kwamba, kupuuzwa na kuachwa bila ya kujibiwa maombi ya mtawalia ya Washington huko Cairo ni ushahidi mwingine wa kuzidi kuporomoka ushawishi wa Marekani barani Afrika. Lililo muhimu zaidi hapa ni kwamba, hatua ya Misri ya kuruhusu anga yake itumiwe na ndege za kijeshi za Russia zinazoelekea nchini Syria, si hatua pekee inayoonesha ushirikiano wa Cairo na Moscow. Kabla ya hapo na kwa mujibu wa nyaraka za siri zilizofichuliwa hivi karibuni na wizara ya ulinzi wa Marekani, Pentagon, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri alikuwa na nia ya kuipa Russia makumi ya maelfu ya maroketi wakati wa vuguvugu la vita vya Ukraine. Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Rais el Sisi aliwaamrisha maafisa wake wafanye kwa siri mno zoezi la kuiuzia maroketi hayo Russia ili uhusiano wa Misri na Magharibi usiharibike. Tab'an hatimaye Misri haikuiuzia Russia maroketi hayo kutokana na mashinikizo ya Marekani kama zinavyosema nyaraka hizo.
Rais wa Misri amekuwa akijaribu sana kuweka mlingano katika uhusiano wa nchi yake na Russia na Marekani wakati huu wa kuendelea vita vya Ukraine na ndio maana anakataa katakata maombi ya Marekani ya kuipa silaha Ukraine na kupunguza uhusiano wake na Russia.
Kiujumla ni kwamba nchi za Kiarabu waitifaki wa Marekani kama vile Misri zimekuwa zikionesha wazi kukaidi amri za Marekani. Kuna sababu mbalimbali za kushuhudiwa hali hiyo. Miongoni mwake ni dharau ya Marekani na madola ya Magharibi na kutotekeleza madola hayo ya Magharibi ahadi zao za kiusalama kwa nchi hizo za Kiarabu. Vilevile kuongezeka nguvu za wapinzani wa ubeberu wa Marekani hasa nguvu za Russia na China. Ongezeko hilo la nguvu na ushawishi wa maadui wa Marekani kumetia kasi mchakato wa nchi hizo za Kiarabu wa kujitenga na Washington na kutafuta waitifaki wapya hasa Russia na China. Nchi hizo ikiwemo Misri, zimeonesha waziwazi kwamba haziko tayari tena kutoa muhanga maslahi yao ya kitaifa kwa faida ya dola la kibeberu la Marekani.