Sep 16, 2023 10:59 UTC
  • UN: Baadhi ya watu nchini Libya wamepoteza wanafamilia 50 au zaidi

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA, Martin Griffiths amesema, umoja huo unaendelea kuhamasisha juhudi za utoaji misaada kwa nchi za Libya na Morocco kufuatia majanga mawili makubwa tofauti yaliyozikumba nchi hizo sambamba na machungu na maumivu makubwa yaliyozipata familia zilizofiwa na kupoteza wapendwa wao katika majanga hayo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Griffiths ametoa wito wa mshikamano na watu wa nchi hizo mbili na akazungumzia pia janga la watu wanaowasaka wapendwa wao kwa siku nyingi kwa kusema, nchini Libya, watu wengine wamepoteza wanafamilia 50 au zaidi.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, janga la kimbunga lililosababisha mafuriko nchini Libya ni janga tofauti kabisa, ambalo lilikuwa la kuogofya, la kushtua na lisilofikirika katika athari zake.

Tayari kuna tetesi kwamba inawezekana watu takribani 20,000 wamepoteza maisha katika mafuriko makubwa yaliyosababishwa na kimbunga Daniel kilichotokea mwishoni mwa juma. Hii ni pamoja na kwamba, fursa ya kuufikia mji wa Derna, ambao ni kitovu cha janga hilo, imebaki kuwa ngumu.

Martin Griffiths

Mkuu huyo wa OCHA ameongeza kuwa, watu 900,000 nchini humo wameathirika,  mbali na watu wengine 300,000 ambao tayari wanahitaji msaada wa kibinadamu.

Griffiths ameelezea mahitaji ya dharura zaidi nchini Libya kwa sasa kuwa ni vifaa vya kutafuta watu walionasa kwenye matope na katika majengo yaliyoharibiwa, malazi, chakula, maji safi na usafi wa mazingira, pamoja na huduma muhimu za matibabu, kwa sababu tishio la kipindupindu linazidi kuwa kubwa.

Pia mkuu huyo wa OCHA amesisitizia haja ya msaada wa kisaikolojia ambapo amesema ni tatizo kubwa na ni suala muhimu la kupewa uzito hasa ukizingatia athari zinazosababishwa na janga hilo.

Naibu Katibu Mkuu wa UN ameyaita majanga yaliyotokea katika nchi zote mbili za Morocco na Libya kuwa ni mshtuko mkubwa na kumbusho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi na uwepo wake.../

 

 

Tags